Kuzikwa Asiye Muislamu Ndani Ya Kaburi Alilozikwa Mtoto Muislamu

 

Kuzikwa Asiye Muislamu Ndani Ya Kaburi Alilozikwa Mtoto Muislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Bismillahi Rahamani Raheem

 

Asaalam Alykum Waramathullahi Wabarakatu.

 

Swali langu ni juu ya mazishi hapa Ujerumani hasa  kwa sisi ndugu zenu waaislamu tunaoishi huku. 

 

Awali nitaelezezea kisa chenyewe kwa ufupu ambacho kitaelezea swali halisi.

Mimi nimzawa wa Mombasa nimejuana na ndugu waislamu wengi sana hapa wengi wao usafirisha maiti zao makwao mfano ya ndugu wengi wanaotoka (North Africa) au Uturuki.

 

Sasa kunaeye kaka yetu mmoja MMerikani mweusi alisilimu zaidi miaka kumi na mbili sasa kaoa mke wakazaa mtoto wao wa kwanza bahati mbaya huyu mtoto alifariki hapa Ujerumani wakapewa sehemu ya kumzika imamu wa msikiti tunaoswali aliwongoza kwa kila jema la kisheria kwa kumzika mtoto huyo.  Hapa zipo sehemu zilizotengwa kwa waislamu lakini mitaa maalumu sasa yeye kwa ujiandikishaji wa ukaaji wa hapa mtaa wao hawakuwa na sehemu ya waislamu hakaomba kumzika mtoto wake kwa sehemu ya waislamu lakini walimkatalia kisheria lazima hamzike sehemu  ya mji wao.   Basi walifanya hivyo walimzika sehemu ya kuzikana hapo kwao mjini sehemu wanaozikwa wakristo, lakini alizikwa kiislamu.

 

Sasa mda mrefu sasa zaidi ya miaka minanae serikali imemletea bili ya kulipia kaburi sehemu aliyozikiwa aliyefariki huyo ya 500€  hii wanasema ni sheria hapa aliyefariki kulipiwa kaburi kwa umri wote litakapojulikana hili ni kaburi la fulani bin fulani.  Au kama hataki kulipa basi hiyo sehemu atazikwa mtu mwengine yeyote ambaye atafuatia ili hii sehemu ipate kulipiwa kodi.   Huyu ndugu yetu kanielezea kuwa yeye alikuwa anataka kuchimba na kutoa sehemu iliyobakia ya aliyefariki mtoto wake na kuisafirisha nchi yeyote ya kiislamu iliyoko karibu hawa watu wa serikali wanamshauri yakuwa huyo alikuwa mtoto mdogo na kufikia sasa sahau hapatapatikana lolote na pia patazikwa yeyote atakayejaliwa tena. kama hatalipia hiyo kaburi au kwa desturi  mtu yeyote atakaye shindwa kulipia kaburi basi mabaki ya aliyefariki yatatolewa na kuchomwa kisha jivu litupwe hili papatikane sehemu ya mtu mwingine.

 

Subuhana  Allaah   hii ni huzuni sana yeye kanieleza kisa hichi jana baada ya kupokea hii bili ya kulipia kaburi na mawazo duni ya makafiri waliyompa.

 

Ndugu zetu waaislamu wa alhidaaya naomba msaada wenu kwa kutufafanulia usawa wa kisa hichi kufuatia kurani tukufu na pia katika hadiyth za Nabiy wetu Muhammad (s.a.w).

 

Hapa huyu ndugu yetu kataka ushauri kutoka kwangu nami nikamuambia nitawauliza mashekhe wetu wa ukumbi wa alhidaaya kwani hata sisi hatujui lini mauti yatatufikia. 

 

Baraka lahu fik.

 

Barua Ya Pili:

 

Bismillahi Rahamani Raheem.

 

Asalaam Alykum Waramathullahi Wabarakatu. 

 

Ndugu zangu waislamu mimi tena nimerudia mara ya pili kuwaletea maombi yangu juu ya swali langu la jana nililolileta kwenu juu ya kulipia kaburi ama wazazi wanahitajika kutoa mabaki ya aliyefariki au pahala papo hapo mazikwe mtu mwengine.  

 

Tafadhali tupeni jawabu wasaa utakavyowezekana kwani huyu ndugu yetu ameletewa barua kwa mda wa wiki mbili sehemu hiyo akishindwa kulipia au kutoa kilochobakia basi serikali washadhaminiwa na watu wengine tayari kuzika maiti ya jamma yao  kwani mahala kama nilivyotangulia kueleza kuwa ni pa wakristo na hata huko kwa waaislamu lazima pia kulipia kaburi kisheria ya serikali umri wote wa kaburini.

 

Je huyu ndugu yetu ashike wapi pa sawa kufuatia  kurani tukufu na sunnah za Nabiy wetu Muhammad (s.a.w). Ninaomba msaada kutoka kwa Mashekhe wetu wa alihidaaya kwani hata yeye mwenyewe amenituma kuulizia kwani hafahamu kiswahili.

 

Masaalam.

 

 

Jibu:

  

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunasikitika sana kupata Swali hili la ndugu yetu aliyefikwa na janga hilo la maiti ya mwanawe, tunaanza na kumuombea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amfanyie wepesi jambo gumu hili na Ampe subira kwa hali yoyote itakavyomfika.

 

Kwanza tunapenda kuwatambulisha ndugu zetu popote walipo kwamba mtu anapofariki haipasi kuhamishwa maiti kupelekewa nchi nyingine ila ikiwa kuna sababu maalumu. Hakuna mwenye kujua wapi atafariki, ardhi yote ni ardhi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye Ametueleza kuwa:

 

وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

Na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34]

 

Sunnah ilivyokuwa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake ni kumzika aliyefariki katika makaburi ya mji huo aliofariki. Mashuhadaa walizikwa sehemu ile ile waliyofariki. Hakuna dalili yoyote au usimulizi kwamba Swahaba au Salafus Swaalih (Wema Waliotangulia) waliwahamisha watu wao waliofariki kuwazika miji mingine au nchi zingine.

 

Kwa sababu hii 'Ulamaa wengi wamekataza jambo hili ila tu ikiwa kuna sababu au dharura maalumu mfano; kama kuna khofu ya kuwa kaburi litatendwa vibaya hapo itakuwa ni bora kumzika sehemu ambako atasalimika na uovu wowote.

 

Vilevile zikiwa gharama za kuzikia maeneo hayo kama ilivyo huko Ulaya, Marekani na Japan, na akawa mtu huyo hana gharama hizo au hakuweza kupata msaada wowote kutoka kwa Waislam walio sehemu hizo, na kukawa kuisafirisha maiti ile ni nafuu mno kuliko kuizikia pale na hali hana uwezo, basi kwa hali hiyo Maulamaa wamejuzisha hali hiyo kwa dharura hiyo.  

 

Kwa hivyo, ndugu zetu wanaosafirisha maiti zao watambue hili. Ni bora wajiepushe na kwenda kinyume na sheria bali wakimbilie kumzika maiti wao mji huo huo aliofariki,  jambo ambalo linapendekezeka zaidi katika sheria. Hivi ni kumhifadhi maiti  kutokana na mateso na usumbufu wakati anatayarishwa na kufanyiwa maandalizi maiti kwa ajili ya kumsafirisha, na pia kujiepusha na taklifu kubwa za kifedha zinazowakabili watu kwa jambo ambalo halikuwekwa katika sheria.

 

Kuzikwa mtu mji wake hakutamsaidia maiti lolote katika kumzidishia mema kwenye kitabu chake wala haitomsaidia lolote kaburini, bali ni amali zake ndizo zitakazomfaa.

 

Ama kuhusu hali ya mtoto huyo aliyezikwa miaka minane nyuma katika makaburi ya wasio Waislamu na hivi sasa hali imefika kama hivyo ya kutaka kuzikwa asiye Muislamu juu yake, tunakuwekea hapa maelekezo ambayo anapaswa kufuata na kukubali kuyakabili kutokana na mafunzo ya sheria ya dini yetu:

 

1.      Kwanza ajaribu kuuliza na kutafuta msaada wa hali na mali katika Jumuiya za Kiislamu zilioko huko Ujerumani wampatie njia ya kumfukua maiti na kumzika katika makaburi ya Kiislamu.

 

2.      Pindi akishindwa kupata msaada huo, lililo bora kukabili ni kuwaacha Serikali wazike mtu mwingine juu yake, japo kama sio Muislamu kama ulivyoelezea, kwani baina ya kuchagua kufukuliwa kisha akachomwe na baina ya kumzika mtu juu yake, ni bora kumzika mtu juu yake kuliko kuchomwa kwa sababu kuchomwa maiti sio jambo lililo na asasi katika dini yetu, hayo ni mambo ya washirikina kama Mabaniani (Hindus). Ama kuzikwa watu wengi katika kaburi moja limepatikana dalili mfano katika vita vya Uhud. Japo katika suala hili azikwaye si Muislam, lakini kwa dharura hiyo hakuna budi.

 

3.      Ikiwa Serikali imegoma kufanya hivyo na imeshikilia kuwa lazima mabaki ya maiti yatolewe na yachomwe na kutupiliwa mbali, basi pia ndugu yetu asitaharuki na kukhofu kuwa atakuwa ameruhusu jambo ambalo haliko katika sheria, kwani hapa atakuwa yeye  hana makosa kabisa na ataangukia katika 'Mudhwtwarr' (asiye na budi) kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika hali ya kula visivyo vya halali :

 

إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَيْرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٧٣﴾   

Hakika Allaah Amekuharamishieni mzoga na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa katika kuchinjwa kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Lakini aliyefikwa na dharura bila ya kutamani wala kupindukia mipaka; basi si dhambi juu yake. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah: 173]

 

Vile vile kwa Rahma Yake Rabb wetu Mtukufu Hatukalifishi jambo tusiloliweza kwa uwezo wetu au lililo nje ya uwezo wetu: 

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ

Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. [Al-Baqarah: 286]

 

Juu ya hivyo mwanawe aliyezikwa hapo ni mtoto mdogo hana dhambi yeyote hivyo hata akizikwa asiye Muislamu juu yake hatoathirika kitu bali yeye ni wa kwenda Peponi moja kwa moja In shaa Allaah.

 

Kwa hivyo hali yoyote itakayomkabili hata ikiwa ni ya ubaya vipi hatohesabiwa kuwa amefanya makosa.  

 

Hayo juu ya kwamba mtoto mwenyewe amezikwa miaka minane nyuma, kwa hivyo bila shaka hivi sasa hatakuwa amebakia kitu bali labda ni mafupa tu kwa hiyo kumchimbua na kuyakusanya hayo mabaki yake haitokuwa jambo la busara kulingana na taklifu itakayopatikana; kwanza kujitia huzuni zaidi ya kumfufua mwanawe, pili taklifu ya gharama kubwa itakayomgharimu.

 

Tunamuomba ndugu yetu akinai na Qadhwaa (mipango) na Qadar (Makadirio) ya Mola wake Mtukufu na atambue kuwa kukubali makadirio na mtihani na kusubiri ni kupata thawabu kwake na ahli yake. Tunazidi kumuombea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuondoshee huzuni ya jambo hili na abakie katika kuridhika na haya majaaliwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi 

Share