Kufuata Rai Katika Mas-ala Ya Dini

 

Kufuata Rai Katika Mas-ala Ya Dini

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Ndugu zangu, Assalaam alaykum,

 

Katika kujibu swali linalohusu "Mas-hul-khufayn" Mlijibu kama kuna tafauti ya Rai  miongoni mwa ‘Ulamaa. Katika kuendelea kujibu swali hilohilo mlielezea kama katika masaala ya ibada Dini yetu hii haiendi na Rai zetu bali ni juu yetu kufuata alivyofanya mtume Muhammad (swalla allahu alayhi wa sallam).

 

Naomba ufafanuzi zaidi kuhusu masaala haya ya kufuata rai.   Natumai nimefahamika. Ahsanteni sana.

 

 

Jibu:

  
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tulipokusudia kuwa Dini yetu haifuati rai ni pale rai zinapokosa ushahidi uliothibiti kutoka katika   Qur-aan na Sunnah. Hivyo, panapokuwa na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   au maneno ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi rai  yoyote ile  haichukuliwi, kwani kuna watu wanataonguliza akili zao   pale ambapo tayari Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wameshatoa hukmu, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:  

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36]

  

Na ndipo ukaona maneno ya 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliposema:

 

"لو كان الدين بالرأي لكان أسفل الخف أولى بالمسح من أعلاه  لقد رأيت رسول الله صلى الله عليه وسلم يمسح على ظاهر خفيه"  رواه أبو داود والدارقطني

 Ingelikuwa Dini inakwenda kwa rai ingelikuwa kupangusa chini ya khuff (soksi za ngozi) ni bora zaidi kuliko juu. Hakika nimemuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) anapangusa juu ya khuff (soksi za ngozi)” [Imepokelwa na Abu Daawuwd na ad-Daaraqutwniy]

  

Japokuwa inaweza isiingie kwenye akili za hao wenye kutumia rai zao   wakaona kuwa kwa nini kusipanguswe chini yaani nyayoni penye kukanyagiwa ambapo ndipo panapokusanya uchafu? Na akamalizia 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwa kusema kuwa hivyo ndivyo alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwa maana hata kama haingii akilini kwa baadhi ya watu, lakini maadam ndivyo alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi hakuna tena rai hapo.

 

Ama rai katika Dini inakubalika pale ambapo hakuna dalili iliyo wazi katika masuala fulani. Na kwa upande mwengine hujulikana hizo rai kama ni Ijtihaad na pia kama Qiyaas katika upande wa Uswuwl. Na hivyo ni kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ مُعَاذٍ  أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم  حِينَ بَعَثَهُ إِلَى الْيَمَنِ ، فَقَالَ (( كَيْفَ تَصْنَعُ إِنْ عَرَضَ لَكَ قَضَاءٌ؟)) قَالَ : أَقْضِي بِمَا فِي كِتَابِ اللهِ ، قَالَ  (( فَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِي كِتَابِ اللهِ؟)) قَالَ : فَسُنَّةُ رَسُولِ الله ، قَالَ : ((فَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِي سُنَّةِ رَسُولِ الله؟)) قَالَ : أَجْتَهِدُ رَأْيِي لاَ آلُو ، قَالَ : فَضَرَبَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم   صَدْرِي ، ثُمَّ قَالَ : ((الْحَمْدُ ِللهِ الَّذِي وَفَّقَ رَسُولَ رَسُولِ اللهِ لِمَا يُرْضِي رَسُولَ الله)) سنن أبي داود

Kutoka kwa Mu’aadh kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alipomtuma Yemen alimuuliza: ((Utafanyaje yatakapokufikia mas-ala?)) Akasema: “Nitahukumu kwa Kitabu cha Allaah”. Akauliza: ((Ikiwa hutopata katika Kitabu cha Allaah?)). Akasema: “Kwa Sunnah ya Rasuli wa Allaah.” Akauliza: ((Ikiwa hukupata katika Sunnah ya Rasuli wa Allaah?)) Akasema: “Basi nitajitahidi rai yangu na sitovuka mipaka, Akasema: “Rasuli wa Allaah (Swallah Allaahu ‘alayhi wa sallam) akanipiga katika kifua changu akasema: ((AlhamduliLLaah  Ambaye Amemuwafikia mjumbe wa Rasuli wa Allaah katika yale aliyoyaridhia Rasuli wa Allaah)) [Sunan Abi Daawuwd]

 

Ingawa Hadiyth hii wamekhitilafiana ‘Ulamaa   kuhusu usahihi wake, ila baadhi yao wamesema ni Swahiyh kwa njia zake nyingi zenye kuitilia nguvu. Na wakasema kuwa inaungwa mkono na kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuhusiana kutii kiongozi wa Dini:

  

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59] 

 

Na pia,

 

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٣﴾

Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wangelijua wale wanaotafiti wakabainisha ya sahihi miongoni mwao. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake kwa yakini mngelimfuata shaytwaan ila wachache tu.[An-Nisaa: 83]

 
Hivyo masuala ya rai yanakubalika pale ambapo hiyo rai haitapingana na  Qur-aan au Sunnah. Na ndio maana Imaam wakubwa wa Madhehebu manne  wakawa wanatofautiana katika mas-ala mbalimbali ya ki-Fiqhi. Lakini Imaam hao wote wanaheshimiwa kwa elimu zao na Ijtihaad zao, kwa kuwa vilevile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) keshaeleza kuwa atakayejitahidi miongoni mwa Imaam au  'Aalim, akapatia katika ijtihad yake, atapata ujira mara mbili,  na atakayekosa atapata  ujira mmoja [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Yote hayo ni katika kuonyesha kuwa rai ambayo inawafikiana  na  Qur-aan na Sunnah inakubalika katika Dini.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share