Kupaka Rangi Ya Kucha Na Kutia Wudhuu Inafaa?

 

Kupaka Rangi Ya Kucha Na Kutia Wudhuu Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalam aleikum waramtullahi wabarakatu.

Mimi ninauliza jee mwanamke kujitia rangi ya kucha (cutex) nakisha huku ana shika udhu na kuswali ile swala yake ina faa?

shukran.

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

 

Rangi katika kucha ni kitu ambacho kinazuia maji kufikia ngozi ya sehemu hiyo, kwa hivyo wudhuu wa mtu na Swalaah yake itakuwa haifai! Na ikiwa utaweka rangi ya kucha itakupasa uitoe kila unapotaka kufanya wudhuu. Haya ni mashaka watakayojibebesha wanawake na kujikalifisha kwa jambo ambalo haliko katika ada za Kiislamu.

 

 

Wanawake wa Kiislamu ni bora kutumia hinnah katika mapambo ya miili yao kuliko rangi za kucha kwani hinnah ni katika vipodezo vya Kiislamu na kutumia ni kufuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake hivyo ni kupata thawabu. Na bila ya shaka wenye kupaka rangi kucha watakuwa wamefuga kucha, jambo ambalo halipasi katika desturi zetu za Kiislamu kwani tumeamrishwa zisipindukie siku arubaini iwe tumeshazikata kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo yenye kutaja mambo ya fitwrah (Maumbile ya asili 'Pure Nature of Creation') 

 

  عن أنس بن مالك رضي الله عنه، قال. "وقت لنا  وفي رواية، قال: وقت لنا رسول الله   في قص الشارب وتقليم الأظافر ونتف الإبط وحلق العانة. أن لا نترك أكثر من أربعين ليلة. أخرجه أبو داود والترمذي ومسلم والنسائي.

Imetoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituwekea muda wa kupunguza masharubu, kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapa, na kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu za siri (pubic hair), kwamba tusiziache zaidi ya siku Arubaini)) [Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy]

 

Dalili nyingineyo pia ni:

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه، عن النبي  قال: (( الفطرة خمسة، أو خمس من الفطرة . الختان، والاستحداد، وتقليم الأظفار، ونتف الإبط، وقص الشارب))  متفق عليه

 Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Fitwrah ni tano, au (vitu) vitano miongoni ni mwa Fitwrah, Kutahiri (Circumcision), kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu ya siri (pubic hair), kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapani, na kupunguza mashurubu))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share