Nini Hukmu Ya Wudhuu Wangu Ikiwa Natokwa Na Pumzi Kila Mara?

SWALI:

Asalam Aleikum

Mimi ninatatizo la kutokwa na pumzi   kila mara.  Wakati wa sala inanibidi niache sala nikatawadhe upya maana ukijamba udhu umetenguka hali hii inanichukua zaidi ya mara nne mpaka tano kukata sala na kwenda kutawadha upya. Nimekwenda hospitali tatizo wameniambia nina gesi ya tumbo. Dawa nimeshatumia sana sana lakini nafuu sikupata. Naomba unipe ushauri nifanyeje hali hii.  Kuna jambo lolote ambalo ninaweza kulitanguliza ili hata nikitoa pumzi niendelee na sala na hiyo sala itakubalika?

WABILAHI TAUFIQ

 


 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya udhu na Swalaah. Hili ni jambo ambalo linaonekana kuwa dogo lakini ni kubwa kwa sababu ya umuhimu wake kama nguzo ya msingi ya Uislamu. Kutokubaliwa Swalaah zetu ni kumaanisha ya kwamba tumekhasirika sana hapa duniani na kesho Aakhirah.

Hili swali linaonyesha muamko wa kidini ambao upo katika ulimwengu hasa kwa vijana mbali na mitihani na vikwazo chungu nzima. Inafahamika kuwa hapana udhuru kwa Swalaah kwani tunatakiwa tuswali katika hali zote isipokuwa kwa wanawake wakiwa katika hedhi au nifasi. Na wengine ambao hawachukuliwi ni wenda wazimu na watoto wadogo (japokuwa wanatakiwa wafundishwe).

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametusahilishia mambo mengi na hasa katika mas-ala ya Swalaah. Muislamu anatakiwa aswali kwa kusimama, lakini ikiwa hawezi basi kwa kukaa, kwa kulala na hata kwa ishara. Hii yote ni kuonyesha cheo, daraja na umuhimu wa Swalaah katika Uislamu. Kwa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hataki kututia katika uzito Anatuelezea: “Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito” (2: 187).

Na tena, “Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo” (2: 286).

Na pia, “Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibraahiym” (22: 78).

Katika matatizo wapo wale wanawake wenye kutokwa na damu isiyo ya kawaida na kupita mipaka (inayojulikana kama Istihaadhah), au wale wasioweza kuzuia mikojo. Hawa huwa wanatakiwa watawadhe kwa kila Swalaah na wafunge kitu ambacho kitazuilia damu au mikojo kuingia katika nguo. Baada ya kutawadha kabla kidogo ya kuswaliwa na kuingia katika Swalaah damu au mkojo unaotoka hauathiri chochote Swalaah yenyewe. Na Swalaah inakuwa sahihi. Tatizo lako ni kama la hao, hivyo unatakiwa nawe utawadhe tu kabla ya Swalaah na kisha uingie katika Swalaah. Wakati huo ukitokwa na gesi utaendelea na Swalaah pia kuirudia tena. Ikiwa kuna kitu ambacho kinaweza kuwekwa katika sehemu yako ya siri ili sauti isitoke ya nguvu au harufu itakuwa bora zaidi ikiwa haiwezekani basi utaswali hivyo hivyo.

Nasaha yetu kwako ni kuwa usivunjike moyo na uwe na hakika kuwa utapona, kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hakuleta maradhi yoyote isipokuwa Ameweka na dawa yake”. Muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika du'aa na ‘Ibaadah zako nyenginezo (katika Swalaah na unapofunga) na kwa idhini ya Allaah utapona.

Jaribu sana usile vyakula vya hamidhi (vikali) na utumie vitu ambavyo ni tiba kwa magonjwa tofauti kama Habbatus Sawdaa na asali. Habbatus Sawdaa inaweza kutiwa katika chai, supu na vinywaji vyengine na inasaidia sana katika magonjwa tofauti, kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa Habbatus Sawdaa ni dawa ya kila ugonjwa isipokuwa mauti.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akupatie shifaa ya haraka na Atuweke sote katika siha na afya nzuri.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share