Je, Nabii 'Iysa Alisulubiwa?

SWALI:

ASALAM ALEYKUM

Swali langu naomba mnisaidie ni kwamba eti Isa Bin Maryam alisulubiwa kweli? Na tafadhali kama inawezekana naomba aya inayohakikisha swala hii. MWENYEZI MUNGU AZIDI KUTUONGOZAJIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako hili. Hili kwa hakika ni jambo ambalo lipo wazi kabisa katika Uislamu na halina utata wowote. Allaah Aliyetukuka Anatuelezea dhahiri shahiri kuwa ‘Iysaa bin Maryam (‘Alayhis Salaam) hakuuliwa na Mayahudi wala hawakumsulubu. Allaah Aliyetukuka Anasema:

((وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُواْ فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلاَّ اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا))

(( بَل رَّفَعَهُ اللّهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا))  

((Na kwa kauli yao kuwa: ‘Tumemuua ‘Iysaa mwana wa Maryam, Mtume wa Allaah’. Hakika ni kuwa hawakumuua wala hawakumsulubu, lakini walishabihishiwa kwao. Wale wanaotofautiana katika hilo wako katika shaka wala hawana ilimu ya uhakika kuhusu hilo, wanafuata tu dhana. Hakika ni kuwa hawakumuua))

((Bali Allaah Alimnyanyua Kwake, na hakika Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima)) [An-Nisaa: 157-158]

 

Waislamu inapasa tuthibitishe 'Aqiydah yetu Swahiyh baada ya kupata maelezo na uongofu katika Qur-aan, tusiwe kama wengine wasioamini baadhi ya kauli za Allaah kwa kuleta shubuhaat na kubadilisha maana za Aayah. Wasioamini kuwa Nabii ‘Iysaa alinyanyuliwa na Allaah ni wapotofu ambao wameshindwa kutambua dalili kadhaa zinazohusiana na kupandishwa kwake mbinguni akiwa hai kama zifuatazo:

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda safari ya Israa Wal-Mi'raaj alikutana na Mitume katika kila mbingu hadi mbingu ya saba. Hivyo alikutana na Nabii ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) akiwa katika mbingu ya pili akiwa pamoja na Nabii Yahya bin Zakariyyah ('Alayhimas-Salaam) akiwa ni binamu yake. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Nilikutana na ‘Iysaa bin Maryam. Alikuwa na umbo la wastani na uso wake ni mwekundu kama vile katoka kuoga…)) [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647] Jibriyl alisema,  “Hawa ni Yahya bin Zakariyyah na ‘Iysaa  ('Alayhimus-Salaam) wasalimie”, na Mtume aliwasalimu na wote wawili walijibu salamu zake na wakamwambia, “Unakaribishwa Ewe ndugu yetu Mtume Mtukufu” na kisha wakamwombea du’aa njema.

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuthibitishia kutokufa kwake hapo mwanzo hadi karibu na Qiyaamah ndipo atakapofariki:

((وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلاَّ لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا))

((Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao)) [An-Nisaa: 159]

 

Hii ni kwa maana atateremka kutoka mbinguni na kuja ardhini kubakika miaka arubaini atekeleze mas-ala mbali mbali. Matukio haya ni katika matukio makuu ya kusimama Qiyaamah. Kuteremka kwake Nabii ‘Iysaa imeelezewa katika Hadiyth mbali mbali, tunanukuu hapa baadhi:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ   ((يَنْزِل عِيسَى اِبْن مَرْيَم فَيَقْتُل الْخِنْزِير وَيَمْحُو الصَّلِيب وَتُجْمَع لَهُ الصَّلَاة وَيُعْطِي الْمَال حَتَّى لَا يُقْبَل وَيَضَع الْخَرَاج وَيَنْزِل الرَّوْحَاء فَيَحُجّ مِنْهَا أَوْ يَعْتَمِر أَوْ يَجْمَعهُمَا))  أحمد

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((‘Iysaa mwana wa Maryam atateremka na kuua nguruwe, atavunja misalaba, ataimamisha watu katika Swalah ya Jama’ah, na kutoa mali hadi hakuna atakayetaka kupokea tena. Ataondosha jizya (kodi) na atakwenda Ar-Rawhaa ambako ataelekea kutekeleza Hajj, ‘Umrah au zote mbili)) [Ahmad]

 

 عن أبي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  ((كَيْف بِكُمْ إِذَا نَزَلَ فِيكُمْ الْمَسِيح اِبْن مَرْيَم وَإِمَامكُمْ مِنْكُمْ)) البخاري

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtakuwaje atakapoteremka Al-Masiyh, mwana wa Maryam (‘Iysaa) akiwa Imaam wenu ni miongoni mwenu wenyewe?)) [Al-Bukhaariy]

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ   ((الْأَنْبِيَاء إِخْوَة لِعَلَّات أُمَّهَاتهمْ شَتَّى وَدِينهمْ وَاحِد وَإِنِّي أَوْلَى النَّاس بِعِيسَى اِبْن مَرْيَم لِأَنَّهُ لَمْ يَكُنْ نَبِيّ بَيْنِي وَبَيْنه وَإِنَّهُ نَازِل فَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَاعْرِفُوهُ رَجُل مَرْبُوع إِلَى الْحُمْرَة وَالْبَيَاض عَلَيْهِ ثَوْبَانِ مُمَصَّرَانِ كَأَنَّ رَأْسه يَقْطُر إِنْ لَمْ يُصِبْهُ بَلَل فَيَدُقّ الصَّلِيب وَيَقْتُل الْخِنْزِير وَيَضَع الْجِزْيَة وَيَدْعُو النَّاس إِلَى الْإِسْلَام وَيُهْلِك اللَّه فِي زَمَانه الْمِلَل كُلّهَا إِلَّا الْإِسْلَام وَيُهْلِك اللَّه فِي زَمَانه الْمَسِيح الدَّجَّال ثُمَّ تَقَع الْأَمَنَة عَلَى الْأَرْض حَتَّى تَرْتَع الْأُسُود مَعَ الْإِبِل وَالنِّمَار مَعَ الْبَقَر وَالذِّئَاب مَعَ الْغَنَم وَيَلْعَب الصِّبْيَان بِالْحَيَّاتِ لَا تَضُرّهُمْ فَيَمْكُث أَرْبَعِينَ سَنَة ثُمَّ يُتَوَفَّى وَيُصَلِّي عَلَيْهِ الْمُسْلِمُونَ))  أبو داود و أحمد

Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mitume ni binamu, mama zao tofauti, lakini dini yao moja. Mimi ndiye mwenye haki zaidi kwa ‘Iysaa mwana wa Maryam kuliko yeyote mwengine, kwani hakukuwa na Mtume baina yake na mimi. Atateremka na mtakapomuona mtamtambua. Ni mtu aliyeumbika vizuri, (rangi ya ngozi yake) baina nyekundu na nyeupe. Atateremka akiwa amevaa nguo mbili ndefu, rangi ya njano isiyokoza. Kichwa chake kitakuwa kina michirizi ya matone ya maji, japokuwa umande haukugusa. Atavunja misalaba, ataua nguruwe, ataondosha jizyah na atawaita watu katika Uislamu. Wakati huu, Allaah Ataangamiza dini zote isipokuwa Uislamu na Allaah Atamuangamiza Masiyh-Dajjaal. Usalama utajaa ardhini, hadi kwamba simba watachanganyika na ngamia, chui na ng'ombe, fisi na kondoo, watoto watacheza na nyoka na hawatowadhuru. ‘Iysaa atabakia muda wa miaka arubaini kisha atafariki, na Waislamu watamswalia Swalah ya janaazah)) [Abu Daawuud, Ahmad]

 

Dalili hizo pekee zinatutosheleza kukinaika kuamini kuwa Nabii ‘Iysaa yu hai mbinguni na atarudi kuishi ardhini kisha ndio atafariki kama viumbe vinginevyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share