Mkiristo Anataka Kujua Kama Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Ana Miujiza Kama Ya Nabii ‘Iysa

 

SWALI:

NDUGU ZANGU WAISLAM NINAWAPENDA, KWA MAANA MUNGU, WANGU ANAHIMIZA SANA UPENDO. KITU KIMOJA AMBACHO NINATAKA NIJUE KUTOKA KWENU, MIMI NI MKISTO AMBAYE NINAMPENDA MUNGU NA NAMUAMINI YESU, YESU ALIFANYA MIUJIZA AMBAYO HAKUNA, AMBAYE ALIYE WEZA KUFANYA, NA MUNGU ALIIRUHUSU HIYO MIUJIZA ILI WATU, WAAMINI, MUNGU ANAWEZA NA PIA YUPO, JE? MTUME MUHAMMADI NI KITU GANI AMBACHO, MUNGU ALIKIDHIHIRISHA KWAKE ILI WATU WAMUAMINI, MAANA. SHERIA AMBAZO ANAZOZIELEZE NI ZILE ZILE ZA ENZI YA KINA MUSSA.NAOMBA JIBU TAFADHALI

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwako na swali ambalo umetuuliza. Nasi kwa upande wetu mwanzo twakualika kujiunga na Uislamu, Dini ambayo ndiyo aliyokuja nayo Nabii Aadam, Ibraahiym, Muusa, ‘Iysa na Muhammad (Amani ya Allaah iwe juu yao wote).

 

Katika Itikadi yetu, ni kuwaamini Mitume na Manabii wote waliotumwa, pasi na kufanya hivyo mtu huwa hajakuwa Muumini. Mwenyezi Mungu Anasema: Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume Wake(2: 285).

 

Ama mas-ala ya Miujiza ni kuwa Nabii au Mtume hawezi kufanya lolote pasi na amri ya kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ndio Qur-aan inatuelezea kuhusu yale yaliyofanywa na Nabii ‘Iysa,

Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini (3: 49). Bali katika mambo ambayo alishindwa kuyafahamu ni kushindwa kwake baada ya kuwa na njaa ni kujua kama mti uliokuwa mbele yake una matunda au hauna. Alikuwa na njaa sana lakini alipowasili kwenye mti akaukuta hauna matunda, akaulaani na kuanzia wakati huo haukumea tena matunda.

 

Lakini ukitizama katika Biblia utakuta muujiza wa kwanza wa Nabii ni kugeuza maji kuwa pombe safi (Yohana 2: 2 – 11) ilhali Qur-aan inatufahamisha kuwa muujiza wake wa kwanza ni kuzungumza akiwa mchanga,

(Mtoto – ‘Iysa) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Swalah na Zakaah maadamu ni hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu (Maryamu (19): 30 – 32).

 

Na tufahamu kuwa Yesu hakuleta lolote jipya katika sheria isipokuwa kwa uchache sana kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi (3: 50).

 

Mtume Muhammad aliridhiwa na mengi na Mwenyezi Mungu, ikiwa moja ni kufanywa yeye ni Nabii wa mwisho ambaye kuondoka kwake hakutakuja Nabii mwengine yeyote,

Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu (33: 40).

 

Kisha yeye ametumwa kuwa ni rehma kwa walimwengu wote, kama alivyosema Mwenyezi Mungu,

Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote (21: 107).

 

Mwenyezi Mungu Alimdhihirishia na kumteremshia Qur-aan ambacho ni kitabu cha mwisho kitukufu ambacho hakijabadilika na kimebakia kama kilivyoteremshwa mwanzo. Mwenyezi Mungu Anasema,

Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho huu (Qur-aan), na hakika Sisi ndio tutakao ulinda (15: 9).

Qur-aan ndio iliyo na sharia ya kufuatwa na Muislamu, nayo imekuja kusahilisha katika mazito mengi yaiyopatikana katika sharia zilizotangulia. Hivyo, yapo mambo yanayofanana na ya Nabii Muusa kwani wote wameteremshiwa ufunuo na Mwenyezi Mungu huyo huyo mmoja.

 

Kwa minajili hiyo, jumbe za Manabii wote ni hii,

Na kwa hakika kwa kila ummah tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani(16: 36).

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Alete tawfiki Yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share