Kuomboleza Katika Misiba Kwa Kujipiga Na Kuchana Nguo

   

SWALI:

 

Asalam aleykum warahamtullah wabarakatu.

Ndugu katika Imani mimi ni mmoja wa wale wenye kufuatilia na kupata vipeperushi vyenu mnavyotoa kila mwezi,ninaishi Muhoro Rufiji, swali langu je Uislamu unasema nini kuhusu mtu anapofiwa akalia kupita kiyasi na wengine wanafikia kuchana nguo zao, kijimwagia machanga,unga na kuna watu wananyoa nywele zao kwa ajili ya kuomboleza hili jambo linajuzu? Na je kuomboleza imethibiti ni siku ngapi?

 

 

  

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran sana ndugu yetu kwa swali lako zuri. Uislamu unakataza kabisa mtu kulia kupita kiasi, kujichania nguo, kunyoa nywele na kuomboleza maombolezo ya kijahiliya.

 

Dalili: Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Si katika sisi (Waislamu), mwenye kulia kwa kujipigapiga, kujichania nguo na kuomboleza kwa maombolezo ya kijahiliya” (al-Bukhaariy na Muslim)

 

Dalili: Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) “Jambo hili la kulia kwa kelele si katika mwenendo wangu, bali moyo unahuzunika na macho yanatoa machozi na wala asikasirikiwe Mwenyezi Mungu. (al-Haakim na Ibn Hibbaan)

 

Dalili: Amesema Mtume Swalla (Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), “Si katika sisi mwenye kulia kwa kelele, kupasua nguo na anayejipiga uso na akatamka maneno ya kijahiliya” (Tuhfatul-Ahwadhiy, Mj. 4, Uk. 40-41)

 

Dalili: Swahaba Abu Muusa alipokuwa mgonjwa taabaan ghafla alizimia, mkewe akapiga kelele kulia kwa sauti, alipozinduka akasema kumwambia mkewe mimi nimeepukana na matendo aliyokataza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani Mtume ameepukana na yule mwenye kulia na kupayuka sababu ya msiba, mwenye kunyoa nywele zake na mwenye kupasua nguo zake sababu ya msiba. (al-Bukhaariy na Muslim)

Dalili: Amesema Swahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Anas Bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) ya kuwa amesema Mtume, “Subira inatakikana pale mwanzo wa msiba [tatizo/pigo]”, (al-Bukhaariy, Muslim na Abu Daawuud)

 

Na kuhusu idadi ya siku za kuomboleza kunatakikana kusizidi siku tatu tu Dalili: “Amesema Swahaba Abdullaah bin Ja‘afar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) hakika Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapa muda wa siku tatu watu wa Ja‘afar bin Abi Twaalib kwenda kufarijiwa kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaendea (siku ya tatu) akasema msilie juu ya ndugu yangu baada ya leo” (Abu Daawuud na an-Nasaaiy)

 

Na kumfariji mfiwa kuna fadhila kubwa Dalili: “Amesema Swahaba Anas Bin Malik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenye kumfariji ndugu yake muumini katika msiba wake, Mwenyezi Mungu Atamvisha vazi zuri takatifu siku ya Qiyaamah” (Al-Khatwiyb Mj. 7, Uk. 397)

 

Kwa shahidi hizo sahihi, ni bora na ndio salama kwa Dini yako Muislamu kujiepusha na mambo hayo yasiyo ya Kiislam ambayo yameigizwa kutoka katika Jahiliya ya mwanzo na Jahiliya hii ambayo bado wamo ndani yake wasio Waislam.

 

Na yasiwaghuri yalke yanayofanywa na baadhi ya watu wanaojiita Waislamu kama Mashia ambao hufanya mambo haya ya kujipiga na kujikatakata pale wanapoadhimisha vifo vya wanaodai ni Maimamu wao katika mwezi wa Muharram! Hayo ni mambo potofu yanayopingana na khulqa njema na upole, huruma, na usamahevu wa Dini yetu hii safi ya Kiislam.

 

Wa Allaahu A‘alam

 

 

Share