113-114-Asbaabun-Nuzuwul: Mu ‘awwidhataan: قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ . قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ

 

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

113-114- Asbaabun-Nuzuwl Al-Falaq, An-Naas

 

 

 

 Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

1. Sema: Najikinga na Rabb wa mapambazuko.

 

 

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ﴿٢﴾

2. Kutokana na shari ya Alivyoviumba.

 

 

وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ ﴿٣﴾

3. Na kutokana na shari ya giza linapoingia.

 

 

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ﴿٤﴾

4. Na kutokana na shari ya wanaopuliza mafundoni.

 

 

وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ ﴿٥﴾

5. Na kutokana na shari ya hasidi anapohusudu.

 

Na pia:

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

1. Sema: Najikinga na Rabb wa watu.

 

 

مَلِكِ النَّاسِ ﴿٢﴾

2. Mfalme wa watu.

   

 

إِلَـٰهِ النَّاسِ ﴿٣﴾

3. Muabudiwa wa haki wa watu. 

 

مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ ﴿٤﴾

4. Kutokana na shari za anayetia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma akinyemelea.

 

 

الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ ﴿٥﴾

5. Ambaye anayenong’ona kutia wasiwasi vifuani mwa watu.

 

 

مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ ﴿٦﴾

6. Miongoni mwa majini na watu.

 

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

 

Al-Mu’awidhataan ambazo ni:

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

Na

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

 

 

Wafasiri wa Qur-aan wamesema kwamba kijana wa kiyahudi alikuwa akimhudumia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaja Myahudi na kumlaghai kijana huyo hadi akachukua kitana cha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumpa huyo Myahudi baadhi ya meno ya kitana hicho na kukitumia kumlogea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

Aliyefanya uchawi huo ni Myahudi aliyeitwa Labiyd bin Al-A'swam ambaye alikitumbukiza katika kisima cha watu wa Zurayq kilichoitwa 'Dharwaan'. Akaumwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) zikanyonyoka nywele zake (ukapita muda wa miezi sita) akihisi kuwa anaonana na wake zake (kwa kujimai) lakini kumbe hajimai nao. Akaanza kugeuka bila ya kutambua yaliyomuathiri.

 

Siku moja alipokuwa amelala, walimjia Malaika wawili; mmoja akaketi mbele ya kichwa chake, na mwengine miguuni mwake. Akauliza aliyeketi kichwani mwake: Mtu huyu ana nini? Malaika mwengine akajibu: Twubb. Akauliza: Ni nini hiyo Twubb? Akasema: Amerogwa. Akauliza: Nani aliyemroga? Akasema: Labiyd bin Al-A'swam Myahudi. Akauliza: Amemroga kwa nini? Akasema: Kitana na nywele.  Akauliza: Viko wapi? Akasema: Katika ganda la mtende na jiwe chini ya kisima cha Dharwaan.

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatanabahi ugonjwa wake akasema: “Ee 'Aaishah! Nimehisi kwamba Allaah Amenijulisha ugonjwa wangu.” Kisha akamtuma 'Aliy na Az-Zubayr na 'Ammaar bin Yaasir, wamwage maji yote ya kisima, wakamate jiwe na kutoa ganda la mtende na meno ya kitana yaliyofungwa mafundo kumi pamaoja na sindano. Hivyo Allaah Akateremsha Suwrah mbili Akajaaliwa kila akisoma Aayah fundo moja lilifunguka hadi mafundo yote yakafunguka akarudisha siha yake. Kisha Jbiryl (عليه السلام) akasema:

 

بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ، مِنْ كُلِّ شَيْءٍ يُؤْذِيكَ، مِنْ شَرِّ كُلِّ نَفْسٍ أَوْ عَيْنِ حَاسِد، اللَّهُ يَشْفِيكَ بِاسْمِ اللَّهِ أَرْقِيكَ 

 

BismiLLaahi arqiyka, min kulli shay-in yu-udhiyka, min sharri kulli nafsin aw ‘aynin haasidin, Allaahu Yashfiyka BismiLLaahi arqiyka

 

((Kwa Jina la Allaah nakusomea ruqyah, kutokana na kila jambo linalokudhuuru, na kutokana na kila nafsi au jicho la hasidi, Allaah Akupe shifaa, kwa Jina la Allaah, nakusomea ruqyah)) [Muslim]

  

Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah, Je tuwaue makhabithi? Akajibu: “Kwa vile Allaah Amenipa shifaa, nachukia kuwadhuru watu.

 

Hivyo ndivyo alivyokuwa mpoke na mwenye huruma Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hata juu ya makafiri.

 

 

Ikhtilaaf Za ‘Ulamaa:

 

Ikhtiliaaf za rai zimepatikana kutoka kwa ‘Ulamaa mbali mbali kuhusu sababu ya kuteremeshwa Suwrah hizi. Kuna wanaopinga sababu hiyo ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kurogwa, na kuna wanounga mkono. Sababu mbali mbali zimetolewa, tutanukuu hapa rai na hoja za pande hizo.

 

Wanaopinga wanasema:

 

 

Kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hawezi kumfanya Rasuli Wake alogwe kwa vile yeye ni kigezo cha mfano mzuri wa maisha ya Kiislamu, na pia inapingana na Qur-aan.

 

 

Wanaounga mkono wanajibu:

 

Wamekanusha hivyo kwani wanaona kwamba mas-ala ya uchawi na kuathirika imewasibu Manabii wengineo kama Nabiy Muwsaa (عليه السلام) kama tunavyoona kwenye Suwrah Al-A’araaf na Suwrat Twaahaa.

 

Wanaona kwamba ni tukio la hakika ambalo limethibiti kwa Hadiyth Swahiyh na kulikanusha itakuwa ni kukanusha Hadiyth nyingi zinazotoa mafunzo ya du'aa mbali mbali za kujikinga na shari, wasiwasi, sihri (uchawi), majini, maradhi, mfano du'aa unapoingia kulala kusoma Suwratul-Ikhlaasw na Al-Mu‘awwidhataan huku unapuliza katika viganja vya mikono na kujipangusa mwilini. Hali kadhaalika unapoumwa. Vile vile Hadiyth iliyotaja watu sabini alfu watakaoingia Jannah wakiwa miongoni mwao ni wale ambao wanapoumwa au wanapofikwa na madhara yoyote hawatafuti tiba ila kuwa na Tawakkul na Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa).  [Muslim]

 

 

Na Riwaayah hiyo ya kulogwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) imepokewa na wapokezi wengi wa kuaminika hivyo haina mashaka yoyote. Waliopekea ni Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, Imaam Ahmad, Abdur-Razzaq, Humaydiy, Al-Bayhaqiy, Atw-Twabaraaniy, Ibn Sa’d, Ibn Mardayah, Ibn Abi Shaybah, Al-Haakim, Abd bin Humayd na wasimulizi wengi kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah, Zayd bin Arqam na Abdullaah bin ‘Abbaas.

 

Ama madai ya wanaoipinga Hadiyth hii miongoni mwa Waislam, kama ambavyo wasio Waislam wanaitumia kutaka kumfanyia istihzai na kudhalilisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)    kwa kusema kama anarogeka basi hata atakayosema yatakuwa ni maneno ya aliyelogwa na hivyo si Wahyi tena! Na kama yatakuwa si Wahyi, basi iweje Rabb wake aruhusu hilo?

 

Jibu la madai kama hayo ya kiakili tu bila ushahidi, ni kuwa, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) yeye kama Rasuli hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea kwake alipologwa kwa upande wa utekelezaji wake wa majukumu na wajibu wake kama Rasuli. Hakuna mapokezi yoyote yaliyoeleza kuwa labda kwa kulogeka kwake, basi alisahau Aayah za Qur-aan au kuzigeuza au kuzikosea n.k. katika hayo masiku aliyodhurika na uchawi. Wala hakuna popote panaposemwa kuwa labda alikuwa akipayuka katika Khutbah zake, au kutoa maelezo ya wahyi ambayo hakushushiwa au japo kusahau kuswali na huku akidhani keshaswali au mengi ya mfano wa hayo. Na kama yangetokea hayo au mfano wake, basi yasingefichikana na Bara Arabu zima lingejua hilo au angalau Madiynah na Makkah wangepata habari hizo, lakini hakukutokezea lolote. Kwani pamoja na kupewa mitihani hiyo na Mola wake, kama ambavyo Manabii wengine walivyopata mitihani mbalimbali, haikuwa na maana zaidi ya kupewa majaribio na pia kuwe ni mafunzo kwetu sisi Ummah wake. Na vilevile tupate kujua namna ya kujitibu kwa kutumia Mu‘awwidhatayn kama ambavyo alivyofundishwa yeye Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  na Jibriyl (عليه السلام) mafunzo yaliyotoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).

 

Tukio hili kwa wale wenye Iymaan thaabit na wenye kukubaliana na mapokezi yaliyothibiti na ambao hawatangulizi akili zao mbele ya nuswuws zilizo Swahiyh ni tukio sawa sawa na matukio mbalimbali yaliyowahi kumpata Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  na ambayo yamesimuliwa katika Hadiyth mbalimbali Swahiyh na hata hao wenye kupinga la kulogwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  nao wamekubali hizo Riwaayah zingine za kudhurika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Mfano wa hizo, ni kama alivyojeruhiwa na kuumizwa vibaya katika vita vya Uhud, au alivyoshambuliwa kwa mawe kule Twaaif, au alivyodungwa na nge, au kupewa sumu katika nyama na kuila, na mengine ambayo yamethibiti usahihi wa mapokezi yake kwenye vitabu vya kuaminika. Iweje wakubali baadhi na wakatae baadhi! Bila shaka ni kuchezewa na akili zao zenye mipaka.

 

Hapa tutakuwa tumejua sababu ya kuteremshwa Suwrah hizo; Al-Falaq na An-Naas au maarufu kama Al-Mu‘awwidhataan.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share