Zingatio: Soma Kwa Jina La Rabb Wako Aliyekuumba

 

Zingatio: Soma kwa Jina La Rabb Wako Aliyekuumba

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Dakika zinakatika                       Mali unaitafuta

Wiki zinaanguka                         Elimu hutaikuta

Miezi inayeyuka                         Nafsi unaifuata

Miaka inachomoka                    Huna unachopata

Umri umemalizika                      Fadhila hujazipata.

 

Ewe mwenye macho ona           Ona yanayopasia

Ona mafunzo ya maana            Yayakayokusaidia

Ona ya kuonekana                    Yasiyokuwa na doa

Dini mukikamatana           Atakupenda Jalia

Upate kukutana                         Mola Kakufurahikia.

 

Hapana uficho wowote kwa Muislamu ambaye moyo wake umesalimika na fikira zilizonyooka, kwamba utukufu wa elimu haupingwi, na yaliyopokelewa katika fadhila zake hiyo elimu, katu hayadhibitiki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ

Sema: Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua? Hakika wanakumbuka wenye akili tu. [Az-Zumar: 9]

 

Allaah pia Anaelezea daraja ya wale waliopata elimu:

 

 ۖ وَإِذَا قِيلَ انشُزُوا فَانشُزُوا يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ ۚ 

Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu. [Al-Mujaadilah: 11]

 

Tusiache kukumbuka kwamba kutafuta elimu ni faradhi kama ilivyo ‘Ibaadah ya Swalaah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu.” [Ibn Maajah na at-Tirmidhiy]

 

Fadhila za kutafuta elimu ni kurahisishiwa njia nyepesi ya kuingia Jannah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Mwenye kufuata njia katika kutafuta ndani yake elimu, Allaah Atamrahisishia njia ya Jannah (Peponi).” [Al-Bukhaariy]

 

Waislamu tunajiona tumetosheka na elimu, kushughulishwa sana na pumbazo za dunia kama vile sinema, mipira, miziki n.k. Wengine wanafurutu ada kwa kudharau tu elimu kama ilivyo ibada ya Swalaah. Imaam ash-Shaafi’i (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) anasema: ‘Kujishughulisha na elimu ni bora zaidi kuliko Swalah za Sunnah.’ Imaam anaendelea kusema kwamba; ‘Hapana baada ya faradhi kitu kilicho bora zaidi kuliko kutafuta elimu.’

 

Ajabu zaidi, elimu kwa siku za leo inapatikana kwa urahisi na uwepesi zaidi. Alhamdulillaah kuna mitandao ya kila aina kuhusu masuala ya Kiislamu. Wapo baadhi ya wanaharakati wanatumia wakati wao bila ya malipo kuwatumia wenziwao barua pepe kuhusu elimu hii. Lakini ni wachache wanaotumia rasilimali hizi. Baadhi yao, hufikia kuzifuta tu barua pepe zinazoletwa kwao bila hata kuzipitia.

 

Tambua ya kwamba, utukufu wa elimu ulio na cheo na ufakhari kuisoma, ni Elimu ya Fiqhi yenye kuchimbuliwa katika Qur-aan na Sunnah. Iko dhamana kwa mwenye kupita njia hiyo kuingia Jannah. Kwa elimu hii, ndio Muislamu huweza kupambanua halali kutokana na haramu.

 

Akili zimetekwa nyara kutafuta rizki zaidi na anasa, hadi kufikia kuidharau elimu ya Kiislamu.

 

Basi tunamwomba Allaah Atuzindushe katika Diyn na Atufungulie ufunguzi wa wenye kujua, Atupe hekima na busara mfano wa mbora wa Manabii na Mursaliyna, na ziwe pia juu ya ‘ali zake na Swahaba zake wote. Aamiyn.

 

Share