Zakaah Inafaa Kupewa Mwalimu Anayefundisha Qur-aan

 

SWALI:

Nashukuru sana kwa biddii na kazi ambazo mnazifanya, Allah awazidishie Ilimu na maisha mema hapa duniani na akhera ulizo langu ni hili nimetaka kutoa zaka ya mwaka huu. ila nina shule mbili za quran ambazo na zisimamia, zina wanafunzi zaidi ya 100 na walimu wawili ambao kupata pesa za kuwalipa kila mwezi huwa ni shida kwa sababu wazazi wahao watoto wengi ni maskini na wengine hawaipi thamani kisomo ca Quran.

kwa hiyo kuna wakati tunabaki na deni la walimu na tunakhofea kuwa wanaweza wakaacha kufundisha na madrasa ikasimama. nilikuwa na jiuliza kuwa ni kashika pesa zangu za zakaa za huu mwezi ni kaziwalipa wakati wa mwaka mzima. hizi pesa za zakaa zinakubaliwa kulipwa ndani mwalimu wa Quran.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa Zakaah zilizofaradhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) zinapatiwa watu maalumu waliotajwa katika Aayah ifuatayo: Wakupewa sadaka (Zakaah) ni mafakiri, masikini, wanaozitumikia, wa kutiwa nguvu nyoyo zao, katika kukomboa watumwa, wenye madeni, katika Njia ya Allaah na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Allaah. Na Allaah ni Mwenye kujua, Mwenye hekima” (9: 60). Hao ni aina nane ya watu ambao wanatakiwa kupewa Zakaah.

 

Mas-ala ya mwalimu wa Qur-aan kulipwa mshahara ni jambo muhimu ambalo sisi Waislam tunatakiwa tulitazame kwa darubini la karibu sana kwani faida ni kwa watoto na wazazi wao. Ni ajabu kuwa waalimu wa Madrasah hawalipwi au wanalipwa mshahara mdogo ilhali wazazi hao hao wanalipa pesa nyingi kuwalipia watoto wao wanaosoma shule. Inatakiwa sisi tuhimizane katika hilo ili tunyanyue kiwango cha maisha cha waalimu wetu na kuipa thamani kubwa elimu ya dini yetu.

 

Ama tukija katika kiini cha swali lako ni kuwa kipengele na fungu analoingilia mwalimu wa Qur-aan ni: “Katika Njia ya Allaah”. Ibara hiyo inamaanisha kuwapatia Mujaahidina na pia ma-Du’aat (walinganizi), hivyo waalimu wa Madrasah wanaingia katika fungu hili kwa ujumla wake. Kwa hiyo Zakaah yako ambayo waitoa kwa mwaka unaweza kuiweka katika akaunti mbali ya kuweza kuwasaidia hao waalimu.

 

Lakini ingekuwa bora zaidi kama wako watu kadhaa ambao wana uwezo ambao wanatoa Zakaah washirikiane katika kufanyia wakfu Madrasah hiyo ambayo inaweza kuwasaidia waalimu wao na wengine kwa miaka mingi inayokuja.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share