Kumchezea Mke Mwenye Hedhi Katika Ramadhaan

 

SWALI:

ikiwa mwanamke yuko katika hedhi na hajafunga na mumewe akamtamani mkewe wakati yuko kwenye swaum lkn hawakufanya kitendo cha ndoa, mumewe akatokwa na manii kwa kumchezea je nini hukumu yake mwanamke? Na nini hukumu ya mume?

Asanteni na tunategemea jibu sahihi kutoka kwenu kabla mfungo haujesha...Allah awajaalie kila la khery kwa kutujibu maswali yetu ameen

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Mtu akiwa amefunga anaweza kumkumbatia mkewe, akambusu lakini inabidi awe ni mtu anayeweza kuyazuilia matamanio yake asiende zaidi ya hapo.

 Kumchezea mwanamke akiwa katika hedhi au bila ya kuwa katika hedhi hadi ukatokwa na manii ni jambo ambalo halipasi kutendeka Ramdhaani kwani hiyo itakuwa ni kufanya makusudi kuvunja sheria ya Swawm. Na  inabidi wewe kama Muislamu uliyefunga uwe na uwezo wa kujizuilia usije ukaingia katika dhambi.

Ikiwa kwa kukaa karibu na mkeo mchana wa Ramadhaan inakufanya wewe umtamani inabidi uchukue tahadhari za ziada ili usiingie katika dhambi kwa kujishughulisha kwa kusoma Qur-aan, kwenda Msikitini na kusikiliza mawaidha au kufanya mambo mengine ambayo yanaweza kukufaidisha hapa duniani na Kesho Akhera.

Ikiwa mume atatokwa na manii kwa kufanya jambo ambalo amekatazwa atakuwa na dhambi kwani ukiwa uko katika Swawm haifai kwako kumchezea mkeo. Hivyo unapotokwa na manii basi Swawm yako itakuwa imevunjika na hufai kula wala kunywa; unatakiwa ujizuilie na vitu hivyo mpaka Magharibi.

Baada ya Ramadhaan inafaa ulipe siku hiyo moja lakini hutakuwa na kafara yoyote.

Pamoja na kulipa siku moja unafaa urudi kwa Allaah Aliyetukuka, uombe maghfira, ujute na uweke azma ya kutorudia tena dhambi hilo. Mkeo pia naye atakuwa na dhambi kukuruhusu wewe kucheza nawe, hivyo anafaa naye aombe maghfira kwa kufanya hivyo wala hatakuwa na jingine lolote.

Na Allaah Anajua zaidi

Share