Zingatio: Kitabu Kitukufu

 

Naaswir Haamid

 

Yareti kama Vitabu vyote Duniani vitabaki na uasili wa Kitabu cha Mola Mtukufu! Yareti kama wangelipata angalau Aayah moja tu yenye kufanana na Kitabu cha Mola Mtukufu! Wangelitakabari na katu Waislamu wasingelikuwa na nafasi tena ya kujinasibu kwa uzuri wa Kitabu hichi. Juu ya hali zote, twamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kukihifadhi Kitabu hichi, kwani sisi hatuna nguvu wala uwezo wa kuhifadhi japo aya moja.

 

{{Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio Tutaoulinda}} [Al-Hijr: 9]

Ndugu zangu Waislamu, hatukai kukiangalia kwa makini Kitabu hichi cha Qur-aan? Namna kilivyo kitukufu. Kilichojaa miujiza, Subhaana-Allaah! Kitabu ambacho ndani yake kina kila aina ya raha na utulivu. Wa-Allaahi naapa kwa Mola wa Mbingu na Ardhi, hakuna Kitabu chenye utamu na mazingatio kama Qur-aan. Mpangilio wa Aayah zake hakika ni maridhawa, wamepita washairi na washairi lakini ushairi uliomo ndani ya Qur-aan hakuna mfano wake.

 

{{Je, Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipokuwa Allaah, ikiwa nyinyi mnasema kweli}} [Yuwnus: 38]

Hakikupata kuwepo wala hakitatokea Kitabu chengine. Kwa nini hatukipi heshima Kitabu hichi namna ambayo inastahiki? Ni furaha iliyoje kuwa na Kitabu namna hichi kwetu sisi Waislamu.

 

Yatosha kwetu kuwa na heshima kwa kuamini kuwa Kitabu hichi kimeshushwa kwa asiyejua kusoma wala kuandika. Huo ni miujiza tosha. Binaadamu tumejaaliwa na akili ya kufahamu, inakuwaje hadi milima ikawa bora kuliko binaadamu? Kwani yareti hii Qur-aan ingelishushwa kwa milima, ingelinyenyekea na kupasuka. Yote kwa sababu ya sisi binaadamu kukosa khofu kwa Mola wetu. Anasema Mola Mtukufu:

 

{{Lau kama Tungaliiteremsha hii Quraan juu ya mlima, ungaliuona ukinyenyeka (na) kupasuka kwa sababu ya hofu ya Allaah. Na hii ni mifano Tunawapigia watu ili wafikiri}} [Al-Hashr: 21]

 

Utukufu wa Qur-aan ni wa kwake pekee, katu kalamu haiwezi kuiandika Qur-aan. Thamani yake ni kubwa kuliko vyote duniani. Tunachofanya sisi wanaadamu ni kukopia tu kutoa nakala zake. Lakini uasili wake katu hatuupati.

 

{{Sema: “Hata bahari ingalikuwa ndio wino kwa (kuyaandika) maneno ya Mola wangu, basi bahari ingelikwisha kabla ya kwisha maneno ya Mola wangu, hata kama Tungalileta (bahari) kama hiyo kuongezea}} [Al-Kahf: 109]

 

Basi kwa hakika hichi si kitabu cha kukifanyia mzaha wala masikhara (At-Tawbah: 9:64-65). Kitabu ambacho ndani yake kimejaa mawaidha juu ya mawaidha. Allaah Anatuuliza Hatufahamu? (Al-Anbiyaa: 21:10). Nawausia ndugu zangu kukisoma kwa mazingatio.

 

Share