Zingatio: Ikhlaasw Ndio Mafanikio Yetu

 

Naaswir Haamid

 

Ikhlaasw (kumtakasia nia) katika kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kukhofu shirki na kupinga machafu ndio msingi mkuu wa kuimarika Uislamu. Yanapokosekana haya ndio huzama mizizi ya Uislamu na kutositawi matawi yake. Hii ndiyo Ikhlaasw aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakaishughulikia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) katika kuithibitisha na kuimakinisha. Kinyume chake ni kufanya Shirki.

 

Shirki ni kwa mtu kumjaaliya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) mshirika katika mambo ambayo ni haki Yake peke Yake, kama kujifanyia mungu au miungu mingine pamoja Naye, anayaabudu au kuitii au kuitegemea au kuipenda na mambo kama haya ambayo hayastahiki kufanyiwa mwengine ila Yeye tu.

 

Na hili ni dhambi lisilosamehemwa kwa njia yoyote ile:

 

{{Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe (dhambi ya) kushirikishwa na kitu, (kukifanya ni mungu na ukakiabudu, ukakiomba…). Lakini Yeye Husamehe yasiyokuwa hayo kwa Amtakaye}} [An-Nisaa: 116]

 

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa nyuma katika kupinga ushirikina, kwani ameeleza ya kwamba shirki ni miongoni mwa mambo saba yenye kuangamiza.[1] Halikadhalika, amesema: Mwenye kumwendea mpiga bao (mpiga ramli) akamuuliza kuhusu jambo lolote, kisha akamsadiki aliyoyasema, hazikubaliwi Swalah zake kwa siku arobaini” (Muslim).

 

Hapana shaka yoyote kwamba ujumbe aliokuja nao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwa ulimwengu wote. Ni kwa sababu hii, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliusambaza ujumbe wa Uislamu kwa Kosroisi – Mfalme wa Fursi na Kaizari – Mfalme wa Rumi. Alikuwa akiwaandikia:

 

{{Sema: “Enyi watu mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Mayahudi na Manaswara)! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na yenu, ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu (au pamoja na Mwenyezi Mungu). Wakikengeuka, semeni: “Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu, (tumenyenyekea amri za Mwenyezi Mungu).”}} [Al-‘Imraan: 64]

 

Inashangaza mno kuona Muislamu anamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliye Mmoja na Asiye na Mshirika. Utakuta Muislamu anapiga bao kujidanganya kuona yaliyo ghaibu! Subhaana min dhaalik. Tunaziweka nafsi zetu wapi enyi Waislamu? Ghadhabu za Mola wetu twazijua? Wasiokuwa Waislamu wamshirikishe Mola, basi hadi sisi Waislamu? Lahaula! Tuelewe kuwa mwenye kumwendea kahini na akamsadiki aliyoyasema, huwa amekanusha yale aliyoteremshiwa Muhammad.[2]

 

Sehemu tofauti na wenye rika kadha wa kadha, wanashiriki kwenye vitendo hivi vichafu. Si mashamba wala mijini, si masikini wala tajiri, wote wamedhalilishwa kwa kumuachia Ibiliys kuwa ndie nahodha wa jahazi yao. Tukumbuke kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam ameeleza: “haingii Peponi mwenye kuamini uchawi.” (Ibn Hibbaan).

 

Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) na wale waliowafuata kwa wema (Rahimahum Allaahu), walikuwa wakiitambua ikhlaasw hii na wajibu wao juu yake, kwani wakati Rustum mkubwa wa jeshi la Kifursi alipomuuliza Rab’i bin A’amir kwenye vita vya Qaadisiya: “Nani nyinyi na nini ujumbe wenu?” Rab’i alimjibu kwa kumwambia kuwa: “Sisi ni watu tulioletwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwatoa watu kwenye ibada ya waja kuwatia kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kutoka kwenye dhiki ya dunia kuwatia kwenye wasaa na nafasi yake, na kutoka kwenye jeuri za dini kuwatia katika uadilifu wa Uislamu.”

 

Hayo ndio malengo yetu ya kuufuata Uislamu, sio sisi Waislamu kuwa ni wenye kumshirikisha Mola kwa uganga na uchawi, kuwa na mashaka ya ulimwengu huu na kushughulika mno na kuchuma mali bila ya kubagua halali wala haramu. Uislamu ndio njia yetu iliyo nadhifu inayokubalika na nyoyo zetu, tuwe na Ikhlaasw madhubuti ili tupate kuondokana na dhulma tunayotendewa Waislamu.

 

[1] Imepokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim

[2] Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na al-Bazzaar.

 

 

Share