Du'aa Gani Asome Mkewe Apate Kizazi? Je, Kusoma Majina Allaah Mara Kadhaa na kupuliza Katika Maji Inafaa?

 

SWALI:

ikiwa mwanamke hazai, afunge siku saba na kila anapofuturu ataje majina haya mara 21 (YA KHALIQ (MUUMBAJI) YA BARI (MWENYE KUENDELEA) NA YA MUSAWWIR (MUUNDAJI) nimeandika maana zake katika mabano ili kurahisisha kuelewa ni neno lipi maana nimeshindwa kuyanakiri kiarabu), kisha atoe pumzi kwenye glass ya maji na afungue saumu yake kwa maji haya na Allaah atamruzuku mtoto.

je nini hukmu ya funga hii na je halali kufunga hiyo saumu na kutamka maneno na matendo kama ilivyoelekezwa hapo ama ni bid'aa dua zipi aombe mja kuomba apate mtoto?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa muulizaji swali nasi tungependa kusema yafuatayo. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: ”Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allaah; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia Amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia Amtakaye watoto wa kiume, au huwachanganya wanaume na wanawake, na Akamfanya Amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza” (42: 49 – 50).

Hivyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuambia kuwa watoto ni neema na tunu kutoka Kwake Yeye na katika uwezo Wake Anampa Amtakaye miongoni mwa waja Wake.

Kukosa kuzaa mtoto au watoto si kuwa una kasoro yoyote ile bali unatakiwa uzidishe kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa kufuata maagizo Yake pamoja na kuacha makatazo Yake.

Hakika ni kuwa hakuna funga (Swawm) wala majina matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ambayo mtu anafaa ayataje idadi fulani ili atunukiwa mtoto. Mambo yote uliyotaja hayamo katika Dini nayo ni mambo ya Bid’ah, hivyo ushauri wetu ni kuwa uachane nayo.

Hata hivyo unaweza kufanya yafuatayo:

Mwanzo, kutopata kwako mtoto huenda ikawa ni kwa sababu ya ugonjwa kwa upande wako au kwa mumeo. Hivyo, tunawashauri kuwa wewe na mume muende mukapime kwa daktari aliyebobea katika masuala hayo ili wawapatie ushauri muafaka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ”Allaah Hajaleta ugonjwa wowote isipokuwa Ametoa dawa yake”. Ikiwa baada ya kupima imeonekana ni ugonjwa kweli daktari huyo atawapatia dawa muafaka ya maradhi yenu.

Pili, ikiwa hakuna kati ya nyinyi wanandoa mwenye maradhi basi inatakiwa kwenu nyinyi wawili kumuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa njia mbali mbali za twaa. Kwa kufanya hivyo, huenda mkapata mtoto. Miongoni mwazo ni kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa dua kwani Yeye Ameahidi kutujibu kama Alivyosema: ”Na waja Wangu watakapokuuliza habari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji Anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka” (2: 186). Katika kuomba Muislamu anaweza kutumia majina Yake Allaah yaliyo mazuri. Pia waweza kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa amali mzuri ulizofanya kama walivyofanya wale watu watatu waliokuwa katika shida na Allaah Akawajibu na kuwatimizia haja yao. Hadithi hiyo sahihi inapatikana katika kitabu Riyaadh asw-Swalihiin, Hadithi nambari 12.

Pia mnaweza kusoma du'aa zifuatazo katika Qur-aan:

 

رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنْكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاء 

 

Rabbi Hab Liy Mil-Ladunka Dhurriyyatan Twayyibatan Innaka Sami'ud-Du'aa

Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi  [(Al-'Imraan: 38]

رَبِّ لاَ تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ  

 

Rabbi La Tadharniy Fardaw-Wa Anta Khayrul Waarithiyn

Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanaorithi [Al-Anbiyaa: 89]

رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَاماً   

 

Rabbanaa Hab Lanaa Min Azwaajinaa Wa Dhurriyaatinaa Qurrata A'yuniw-Waj'alnaa Lilmuttaqiyna Imaamaa.

Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu [Al-Furqaan: 74]

Tatu:

Manapaswa mtambue kila jambo lina kheri yake, ikiwa majaaliwa yenu kutokupata watoto basi pia ni kheri kwenu kwani huenda kukawa na shari kupata kwenu watoto, shari ambazo hamuwezi kuzitambua. Pengine watoto waje kufariki baada ya tabu zote za kubeba mimba, kuzaa, kulea n.k. au pengine wawe watoto wasio na kheri pengine wafike hadi kuingia katika kufru na shari nyinginezo ambazo ni mambo ya ghayb hakuna ayajuae ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Naye Ametutanabahisha hili:

   ((وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تُحِبُّواْ شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ))

((Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allah Anajua na nyinyi hamjui)) [Al-Baqarah: 216]

Hii ni mojawapo wa nguzo za Iymaan ambayo Muislamu anapaswa kuamini ili awe na sifa ya Muumini kama tulivyofunzwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Iymaan:

 

  ((أَن تُؤمِنَ باللهِ، وملائِكَتِهِ وكُتُبِهِ، واليَوْمِ الآخِرِ، وتُؤمِنَ بالْقَدَرِ خَيْرِهِ وشَرِّهِ)) مسلم

Ni kumwamini Mwenyeezi-Mungu, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume yake na siku ya Kiyama, na  kuamini ya kuwa kheri na shari zinatoka Kwake)) [Muslim]

Kuamini majaaliwa, amri na mipango Yake Mola Mtukufu itakupeni ridha ya nafsi na kumshukuru na hakuna ubaya kuomba vile vile ikiwa kizazi kitakuwa na kheri na nyinyi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share