Jina La Nasra Linafaa Kutumika? Kwani Ni Jina La Sanamu Wa Zama Za Nuuh

SWALI:

 

Assalaykum warahmatullahi wabarakatuh.

 

Mtume wetu Muhammad (SAW) ametuusia kupeana majina mazuri na tusiitane majina mabaya. Swali liko hivi jina la Nasra ni zuri lakini ukiaangalia katika surat Nuh, aya ya 23 inasemekena kuwa ni moja katika majina ya masanamu waliyokuwa wakiabuadia watu wa Nabii Nuh kama aya inavyosema

 

وَقَالُوا لاَ تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلاَ تَذَرُنَّ وَدّا ً وَلاَ سُوَاعا ً وَلاَ يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرا

 

23. Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra.

 

Sasa jee inafaa kumwita mtoto jina la Nasra au haina neno naomba nifafanuliwe zaidi. wabilahi tawfiq.

 


 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuitwa mtoto msichana kwa jina la Nasra. Tunapenda awali ya yote mwanzo kueleza yafuatayo, ifahamike kuwa majina haya Wadd, Suwaa', Yaghuuth, Ya'uuq na Nasra yalikuwa ni majina ya watu wema waliokuwa kabla ya Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam). Hawa Waumini walikuwa msitari wa mbele katika kufanya mema na kusaidia wenziwao pamoja na kufanya Da'wah. Walipokufa Ibliys alikuja kwa jamii hiyo na kuwachezea mpaka wakaanza kuwaabudu.

 

Kwa ajili ya 'Ibadah hiyo ambao walifanyiwa hao, ndio Uislamu ukawa ni wenye kufunga njia ya kuyaendea maovu kwani mtoto akiitwa jina hilo huenda watu au yeye mwenyewe kupotoka na kupotea pamoja na kuwapoteza wengine. Hivyo, kuziba na kufunga madhara ambayo yanaweza kupatikana Muislamu hafai kumuita mtoto wake kwa majina hayo.

 

Baada ya kusema hayo inaonekana kuhusu jina hilo la Nasra ni sisi ndio tunakosea katika kuliandika, kwani kuna tofauti baina ya jina tunaloita wasichana wetu na hilo ambalo limetajwa katika Aayah hii. Hebu tuliandike tuone tofauti yake:

 

نَسْرا (Nasra)

نَصْرة (Naswrah)

 

Tukitizama majina hayo mawili juu tutaona tofauti ya wazi kabisa. Jina linalotumika katika majina wanayoitwa au kupewa mabint lina Swaad, Naswrah (la kike) na Naswr au Naaswir (la kiume), na sio Nasr kama kwenye majina ya hao walitajwa katika Surat Nuuh.

 

Tuna imani kuwa ufafanuzi huo utakuwa umesaidia kuondoa utata huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share