Kuswali Swalah Ya Safari Kwa Sababu Ya Udereva

 

 

SWALI:

Mimi nafanya kazi ya udereva hapa ulaya wa kuendesha basi la abiria wa town bus (DALADALA). Swala langu ni kwamba INAFAAA KWA mimi kuswali safari??? kwa sababu time nyingine ninakua sipati nafasi kwa sababu ukianza unakua unaenda kwa timu hadi unamaliza sasa time nyingine unachelewa hata timu ya   kujinyoosha hamna yaani ukiingia kwenye usukani hadi 4 hrs later ndio unapata nafasi ya  kutoka, au sipati maji ya kutia udhu au  sehemu yenyewe inakua haisihi kuswali je inafaa   kwa mimi kuswali safari?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu kuswali Swalah ya safari katika shughuli yako hiyo ya udereva. Hakika ni kuwa swali lako si kamili hivyo inakuwa ni vigumu kukujibu kikamilifu. Hata hivyo, tutajaribu kulitazama swali lako hilo katika kila upande.

 

Mwanzo hukutuambia uendeshaji wako wa daladala unakuwa kutoka wapi hadi sehemu gani. Je, kama ulivyosema katika suala lako ni uko mjini ambao wewe unaishi? Ikiwa jawabu ni ndio, basi itabidi ukamilishe Swalah kwani hutakuwa ni msafiri bali ni mkazi. Ikiwa safari yako inakupeleka mji mwengine basi hapo utakuwa umeingia katika wasafiri na unaweza kuswali kwa kuchanganya na kufupisha. Katika kuchanganya unaweza kuchelewesha Swalah au kuleta mbele, yaani unaweza kuswali Swalah za Adhuhuri na Alasiri wakati wa Adhuhuri au Alasiri.

Ama katika kadhia yako ikiwa uko mjini, basi unaweza baadhi ya nyakati kwa dharura hizo, kuunganisha Swalah mbili kwa pamoja, yaani Adhuhuri na Alasiri, au Magharibi na 'Ishaa lakini kwa kuziswali zote kamili na si kwa kuzifupisha. Ila usilifanye hilo kuwa ni ada ya kila siku.

 

Hakika wakati ni mtu kujipanga kwani hakuna uzito aina yoyote. Ikiwa una hima ya kweli unaweza hata kuzungumza na waajiri wako wakuweke ile zamu ya asubuhi ambayo itakupatia wewe fursa ya kuweza kutekeleza jukumu la Swalah kwa wakati wake. Inabidi uwaelezee waajiri umuhimu huo ili waweze kuelewa. Ikiwa wameelewa utapata afueni kubwa lakini usikae tu bila kujieleza ni lazima ufanye juhudi katika hilo.

 

Sijui hayo masaa bayo unasema unafanya mfululizo huwa ni namna gani? Je, unapoanza huwa hakuna hata ile nafasi ya kwenda chooni kujisaidia au kufika kituo na kubeba watu kwa dakika chache au ni vipi? Ikiwa zipo hizo nyakati basi hakutakuwa na shida yoyote kwani unaweza kutumia fursa hiyo.

 

Ama hakika kuswali si lazima maji yapatikane. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameifanya Swalah kuwa ni nguzo isiyokuwa na udhuru wa aina yoyote. Muislamu akikosa maji basi ameruhusiwa na sheria kutumia mchanga ili afanye tayamamu. Hivyo, ikiwa maji hakuna utatumia vumbi au mchanga kwa ajili ya kushika wudhuu na kisha kuswali.

 

Lakini tunayofahamu kama wewe ni dereva na unapoanza kazi zako unatokea nyumbani kwako, basi hatuoni kwanini unashindwa kuweka maji kwenye galoni na ukayachukua ndani ya daladala lako kwa ajili ya kutumia katika wudhuu? Hilo linawezekana kama ambavyo mnaweza kuweka maji ya akiba kwa ajili ya kujazia gari wakati yanapopungua! Tusitafute dharura ambazo si za msingi sana za kuifanya 'Ibaadah zetu ziwe ngumu. Na kwa hapo Ulaya ndio rahisi zaidi kwani kila pembe kuna sehemu zenye maji. Na ikiwa hakuna maji kabisa maeneo hayo, na akiba kwenye gari imekwisha kwa sababu moja au nyingine, basi rukhsa ya kutayamamu ipo hapo.

 

Ama sehemu kutosihi haipo katika Uislamu kwani ardhi yote imejaaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa ni twahara. Kwa hiyo, Muislamu akifikiwa na wakati wa Swalah anaweza kuswali popote ila tu ikiwa ataona najisi ya dhahiri. Hivyo usitie wasiwasi kabisa kuhusu sehemu ya kuswalia.

 

Na pia kuna uwezekano wa kuchukua wudhuu katika maeneo vilivyopo vyoo huko kwenye vituo vya ma-bus au daladala kwa inavyojulikana, na hata humo mnapoanzia kuchukua daladala. La kufanya ni kuingia na kikombe chako cha kutumia na kutupa 'disposable cups' na kutumia kuwekea maji na kujisafisha nayo baada ya kujisadia, kisha ukaenda kuchukua wudhuu kwenye beseni (sink) zilizopo nje ya vyoo na ukifika sehemu ya miguu na ikiwa unachelea kuweka miguu yako kwenye hizo beseni kwa kuwa utawakera wengine ambao si Waislam, unaweza kupaka maji juu ya viatu vyako au soksi zako na ukaswali nazo, kwa sharti tu uhakikishe kuwa ulishanuia kufanya hivyo na kuchukua wudhuu wote na miguu kabla hujaamua kupangusa hivyo viatu au soksi baadaye (unaweza kuchukulia huo wudhuu kamili nyumbani kabla hujatoka, kisha baadaye utakuwa unapungusa tu juu ya viatu au soksi ukiwa uko kazini au njiani).

Soma Swali katika kifungo kifuatacho upate maelezo ya kuchukua wudhuu huo unaoitwa mashul-kufayn (kupangusa juu ya soksi/viatu):

 Mtu Mgonjwa (Kilema) Afanye Wudhuu Vipi Na Aswali Vipi?

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akufanyie sahali suala lako hilo na Awafanye waajiri wenye kukupatia wakati muafaka wa kuweza kufanya kazi kwa njia nzuri na kuabudu kwa wakati wake. Na ukiwa na nia yote hayo yatakuwa mepesi kwa uwezo wa Allaah.  

Na Allaah Anajua zaidi

Share