Mtu Mgonjwa (Kilema) Afanye Wudhuu Vipi Na Aswali Vipi?

SWALI:

Ndugu yetu mwanamume ni  mgonjwa (kilema)  yuko kwenye wheelchair, na mwenye kumuangalia hawezi kumuogesha kila siku, anamkogesha siku moja na siku ya pili anapumzika.    Maswali ni haya:

1)  Hawezi kila mara (au tabu sana)  kumpeleka mswalani  na kumtilisha wudhuu. Je, afanye nini? Na hawezi kukaa na udhuu muda mrefu. Je, anaweza kuunga Sala?

2) Wakati mwingine huamka mgonjwa   akiwa  ameota  (Ndoto ya kutokwa manii)

Je, lazima aoge josho?  na kama hawezi afanye nini

 


 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allah Anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza, kabisa ALHIDAAYA inamuombea mgonjwa huyu kwa Allaah سبحانه وتعالى  Amuondoshee maradhi aliyonayo na ampe uzima na afya kamili kisha Amlinde na kila maradhi pamoja na wagonjwa wote wa Kiislamu. 

Pili tunapenda kumpa bishara mgonjwa na jamaa zake kuwa huo ni katika mitihani ya Allaah سبحانه وتعالى   ambao amekwisha andikiwa binaadam na kila anaposhukuru na kusubiri hulipwa thawabu bila ya hesabu kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى    

 ((إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ))

 ((Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu)) [Az-Zumar:10]

 Ni muhimu tufahamishane ya kwamba Swalah ni lazima ziswaliwe kwa wakati wake mahsusi uliowekwa, Allaah سبحانه وتعالى   Anasema:

((Kwa hakika Swalah  kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi)) (Suratu An-Nisaa 4:103).

Kwa hivyo, miongoni mwa masharti ya kuswihi Swalah ni kuingia kwa wakati. Haifai kuswali kabla au baada ya wakati wake makhsusi ila kwa hali za dharura zilizo tajwa katika sheria, kama kujumuisha Swalah katika safari, kunyesha kwa mvua au baridi kali au kuweko kwa khofu.

 

Ama kulingana na hali ya mgonjwa huyo uliyomtaja, inahitajika awe anavalishwa hafadha (pampers) ambazo zitamsaidia yeye ili anapokwenda haja kubwa au ndogo isiwe ni yenye kuenea na hata kumpunguzia mwenye kumhudumia  kazi nyingi zaidi.

 

1.   Kwa sababu ya shida hiyo ya kuweza kumpeleka chooni kila mara anapokwenda haja itakuwa ni bora kutumia hafadha ambazo tumezitaja hapo juu. Kitu ambacho anapokwenda haja, ile hafadha inasaidia sana na hivyo kazi yake itakuwa ni kumtoa na kumtwahirishwa haja yake ndogo na/au kubwa kwa karatasi ya chooni (toilet paper) kwa kuchukulia hukmu ya ‘istijmaar’.  Si lazima amuinue hasa wakati ambapo huwa hakuna mtu wa kumsaidia kwa kuwa hamuwezi au ni shida kufanya hivyo. Kinachohitajika ni kumtoa hafadha na kumsafisha kama kiasi anachoweza mwenye kumuangalia,  baada ya hapo kumvalisha hafadha safi. Kwa hali aliyokuwa nayo mgonjwa  anaweza ima kutatawadhishwa au kutayamamishwa kulingana na hali inavyo wezekana.

Wepesi mwingine wa kufanya wudhuu ni kufanya mas-hul-khufayn (Kupangusa juu ya soksi). Nayo ni kufanya hivi:

Kuvaa soksi baada ya wudhuu na kukaa nazo kwa muda wa siku nzima yaani masaa 24.

Wudhuu huu katika miguu utabakia kuwa ni wudhuu humo hata kama atakuwa anakwenda haja kubwa au ndogo. Ila sehemu nyingine za viungo vya wudhuu ndio itahisabika kuwa wudhuu umetoka, ama katika miguu utabakia tu kuwa upo.

Kila anapofanya wudhuu atakuwa anafanya wudhuu kamili kote isipokuwa kwenye miguu hatovua soksi bali atapangusa tu juu yake mara tatu miguu yote miwili.

SHARTI ZA MAS-HUL-KHUFAYN:

  • Lazima zivaliwe katika hali ya Twahara (akiwa na wudhuu).
  • Zifunike hadi kifundo cha mguu.

Kuna tofauti ya rai miongoni mwa Maulamaa kuhusu ikiwa mtu atakapovua soksi au khuff zake basi wudhuu wake utatenguka au kubakia. Rai iliyo sahihi ni kuwa wudhuu utakuwa bado upo na haujatenguka kwa kuwa hakuna katika mapokezi ya kisheria yaliyoeleza kutenguka kwa wudhuu katika hali hiyo ingawa mapokezi yameeleza jinsi ya kufanywa wakati wa kuchukua wudhuu. Rai hiyo ni ya wema waliotangulia na Maulamaa wakubwa, nao ni: Qataadah, al-Hasan al-Baswriy na Ibn Abi Layla. Na imeungwa mkono na Ibn Hazm na ndio rai ya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah na Ibn al-Mundhir na katika wanachuoni wa karibuni ni Shaykh Ibn 'Uthaymiyn. Imaam An-Nawawiy kasema kuwa hii ndio rai yenye nguvu.

Na kuhusu soksi kuwa na tundu dogo au kubwa, au ni nyepesi inaonyesha mwili, ingawa tulitumia rai ya nyuma kuwa hazifai, lakini rai iliyo sahihi ni kuwa hazina neno kwani sheria haikuweka masharti hayo na kama kungekuwa na matatizo katika hayo, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angesema na kuweka wazi hilo. Rai hii wamekubaliana Maulamaa wengi wakiwemo; Imaam Ash-Shafi'iy, Imaam Ahmad, Imaam Sufyaan ath-Thawry, Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam an-Anawawiy, Ibnul Mubaarak, Ibn Uyaynah, Abu Thawr na wengineo. Ama Imaam Abu Haniyfah na Imaam Maalik wao wamekwenda kwenye msimamo wa kuwa soksi zikiwa na matundu makubwa katika sehemu zenye kupaswa kutiwa wudhuu zinakuwa hazifai.

YANAYOVUNJA MAS-HUL-KHUFFAYN

·   Muda wake ukitimia – nao ni masaa 24 kwa aliye nyumbani, na masaa 72 (siku tatu) kwa msafiri.

·  Pindi atakapokuwa mtu katika hali ya Janaba, Hedhi au Nifaas.

 

    2.      Ama kuhusu kujumuisha baina ya Swalah ya Adhuhuri na Alasiri au Magharibi na 'Ishaa, hii inajuzu kwa sababu ya udhuru wa ugonjwa kama huu ulioutaja, au kama mgonjwa ambae hawezi kuzuia mkojo (Salisul Bawl), mwanamke anae kuwa katika hali ya Istihadha, na kadhalika. Hivyo, kwa hali ya mgonjwa anaweza kuswali Adhuhuri na Alasiri katika wakati wa Adhuhuri au wa Alasiri na hivyo hivyo kujumuisha baina ya Magharibi na ‘Ishaa. Na pindi anapovalishwa hafadha mpya na ameingia katika Swalah ikiwa atatokwa na mkojo anasamehewa hilo.

     3.      Ikiwa mgonjwa ameamka akiwa amehtalam (ndoto na kutokwa na manii) inabidi aogeshwe kabla ya kuweza kuswali. Lakini ikiwa kwa wakati huo kuogwa kwake ni shida au inaweza kumletea matatizo basi anaweza kutayamamu na kuendelea kuswali. Allaah سبحانه وتعالى  Anasema:

“Enyi Mlioamini! Msikaribie Swalah, hali mmelewa, mpaka myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake (mume kutana kimwili na wake zenu) – na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allah ni Msamehevu na Mwenye Kughufiria” (4: 43).

 Na katika aya ambayo ipo wazi kabisa katika mas-ala hayo ni maneno ya Allaah  سبحانه وتعالى          

 “Enyi Mlioamini! Mnapo simama kwa ajili ya Swalah basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka viwikoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake (mume kutana kimwili na wake zenu) – na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Allah kukutieni katika taabu” (5: 6).

 

 MAELEZO KUHUSU KUTAYAMMAM

Kusihi tayamum ni lazima kuwe na vumbi/ mchanga bila kujalia mchanga au vumbi linapatikana sehemu gani. Ikiwa lipo kwenye ukuta au sakafu iliyopakwa rangi au kochi au juu ya vigae (tiles) au zulia. Na hili ni jambo jepesi kwani hakuna sehemu ambayo vumbi halipatikani. Ikiwa nchi inayoishi familia hakuna vumbi kabisa lakini kunaweza kupatikana changarawe au tofali au jiwe kubwa likawekwa ndani ya nyumba kwa ajili hiyo.

Kunatakikana kutayamamu kisheria kwa sababu zinazofuata:

1)      Kukosa maji kabisa.

2)      Ugonjwa, hivyo kutoweza kuyatumia.

3)      Kuogopa kuyatumia maji, kwani ukifanya hivyo huenda ugonjwa ukazidi au kuchelewa kupona.

4)      Kutoweza kutaharaki na asipate mtu wa kumtawadhisha.

   NGUZO ZAKE:

1)        Kunuia, kwani matendo yote yanachukuliwa kwa nia.

2)        Kutumia mchanga ulio tohara

3)      Pigo la kwanza, nalo nikuweka mikono miwili juu ya mchanga. Allaah سبحانه وتعالى Anasema: “Basi ukusudieni mchanga safi (4: 43).

4)      Kupaka uso na vitanga (mikono) miwili. Allaah سبحانه وتعالى Anasema: “Basi tayamamuni vumbi lilio safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu” (5: 6).

    NAMNA YA KUTAYAMMAM NI KAMA IFUATAVYO:

 

1)     Kusema Bismillahi hali ya kunuia moyoni

2)    Kupiga kwa viganja viwili ardhi, miongoni mwa mchanga au changarawe au mawe na mfano wake, na si vibaya kukung'uta vumbi kutoka katika vitanga vyake.

3)    Kuupaka uso mpako mmoja.

4)   Kisha atapaka viganja vyake viwili.

Tunamuombea sana mgonjwa, Allaah سبحانه وتعالى   Ampe subira na Amuweke  katika hali hiyo hiyo na Imani na ‘Ibadah, Amuafu mgonjwa huyo na kila Muislamu. Pia tunamuombea mwenye kumuangalia Allaah سبحانه وتعالى   Ampe huo huo moyo wa kumhudumia mgonjwa huyo, Amlipe malipo mema na jazaa nzuri hapa duniani na kesho Akhera.  

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share