Anatangaza Kuwa Mke Wake Ni Bikra

 

SWALI:

 

Kwa uwezo wa Allah (S.W) naomba niulize swali langu kama ifuatavyo. Kuna uhalali gani wa mwanaume kutangaza kwa watu kama baba yake mama yake na dada zake kama mke alie muoa ni Bikira?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo juu ya uhalali wa mwanamume kutangaza kuhusu ubikira wa mkewe.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu. Pia Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa.

 

Tukirudi kwenye swali lako Ni kitu kinachojulikana na kila mmoja katika mji/ jiji/ kijiji kuhusu hali mwanamme au mwanamke pindi anapooa au anapoolewa. Hili si jambo ambalo ni geni kwa kila mmoja kwani watu huwa wanajua kuanzia anapoposa mwanamme na kuposwa mwanamke.

Hivyo, si sawa kabisa kwa mwanamme kuanza baada ya harusi kuanza kumwambia kila mmoja au watu wake wa karibu kuwa mkewe ni bikra. Na hasa kuwa hawa ni watu wake kama ulivyosema kama baba, mama na dada zake inatakiwa kuwa kijana amewaeleza jamaa zake kuanzia mwanzo sio baada yake na kutangaza si sawa.

Ama lile jambo linalofaa ilikuwa ni kujibu kwa suali ambalo utakuwa umeulizwa na mtu ambaye labda ni mzazi wako au ndugu yako, na si kwa kila mtu kwani wengine hawahitaji kufahamu hilo wala kujulishwa kwani hawastahiki kuyajua hayo. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye anatueleza kuwa alikutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kuoa kwake (akatambulika kwa ishara ya rangi). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuuliza: “Je, Jaabir umeoa?” Akajibu: “Ndio”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza tena: “Bikra au mke mkuu (thayyib)?” Akajibu: “Mke mkuu…” (al-Bukhaariy na Muslim).

Ifahamike hapa lengo la Mtume kumuuliza Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ni katika kutaka kumshauri lenye faida na manufaa naye zaidi na si kutaka tu kujua kwa ajili ya kujua tu! Na mbele ya Hadiyth hiyo ametaja sababu hiyo ya kumuuliza, ambayo ni ‘Kwa nini usioe bikra .

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share