Du'aa Maalum Katika Sijda Ya Mwisho Ya Swalah ya Alfajiri Ya Kuomba Haja

 

SWALI:

Kwanza nakupongezeni kwa kuiboresha website hii na kutuwezesha sisi wanafunzi wenu kujua mengi kutokana na uchambuzi muliotuwekea kwenye site hii mpya, Inshaalah Allah atakulipeni mema hapa duniani na kesho akhera - amiin.

Suali langu ni, nilisikia shekhe mmoja kupitia radio ya kiislamu akisema, Sala ya sunna kabla ya alfajiri ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani yake, na akasema kua unasaliwa rakaa mbili, rakaa ya mwanzo ni AL fatiha na Suratul Kaafiruun, na rakaa ya pili ni Al fatiha na Ikhlas. Pia akasema kwenye sijdah ya mwisho kuna dua'a unasoma ili Allah akutatulie matatizo yako, na dua yenyewe ni hii "YA WADUD, YA DHUL ARSHIL MAJID, YA FA'ALUL LIMA YURID..." na utaomba ile shida yako halafu ndio utanyanyuka utasoma Attahiyyatu na utaishia na salamu.

Je, hii ni kweli? na kama ni kweli naomba nifahamishe uzuri pamoja na hiyo dua manake sikuifahamu uzuri kuiandika siku niliyoisikia kwenye radio.

Shukran.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya du’aa. Hakika ni kuwa Hadiyth hiyo uliyoitaja ni sahihi kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

Rakaa mbili kabla ya Alfajiri ni bora kuliko dunia na viliyomo ndani yake” (Muslim na at-Tirmidhiy kutoka kwa ‘Aaishah [Radhiya Allaahu ‘anha]).

Kwa fadhila na ubora huo ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuziacha daima (al-Bukhaariy).

Ibn al-Qayyim anatueleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiziswali akiwa mjini au katika safari.

Ama kuhusu kisomo ni kama ulivyosikia mbali na kwamba vipo visomo vyengine kama tutakavyoeleza. Visomo sahihi ni kama vifutavyo:

  • Katika rakaa ya kwanza utasoma Suratul-Faatihah na al-Kaafiruun na ya pili al-Faatihah na al-Ikhlaasw (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

  • Hadiyth nyingine inatufahamisha: Rakaa ya kwanza utasoma al-Faatihah na ayah ya 136 ya Suratul-Baqarah na rakaa ya pili al-Faatihah na ayah ya 64 ya Surat al-‘Imraan (Muslim na an-Nasaa’iy kutoka kwa Ibn ‘Abbaas [Radhiya Allaahu ‘anhuma]).

  • Au pia katika rakaa ya pili akasoma baada ya al-Faatihah, ayah ya 52 ya Surat al-‘Imraan (Muslim na Abu Daawuud kutoka kwa Ibn ‘Abbaas [Radhiya Allaahu ‘anhuma]).

Ama kuhusu du’aa hiyo uliyotaja zipo Hadiyth nyingi zinazozungumzia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma ima baada ya Swalah, au usiku anapoamka kwa Tahajjud au katika Sunnah ya alfajiri bila kusema ni katika rakaa ya ngapi, au katika Qunuut ya Swalah ya Witri lakini zote ni dhaifu. Ama ile iliyopatikana katika sijdah ya rakaa ya mwisho ilisomwa na Swahaba aliyeshikwa na jambazi na akaomba aruhusiwe kuswali Swalah kabla ya kuuliwa. Aliruhusiwa naye akaswali sunnah ya rakaa nne na katika sijdah ya mwisho akawa ni mwenye kusoma du’aa ndefu kikiwemo kifungu hiki lakini hii ni Mawdhuu‘ (ya kutungwa/ kubuni kama anavyosema Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn al-Albaaniy).

Hakika ni kuwa du’aa za kusoma ukiwa katika sijdah zipo nyingi ambazo zinaweza kusomwa katika Swalah yoyote ile – iwe ni ya faradhi au ya Sunnah katika rakaa ya kwanza au ya pili na hiyo uliyoitaja si miongoni mwazo. Hivyo ni bora kutumia zile zilizosuniwa kuliko kutumia hiyo ila papatikanwe mapokezi yaliyo sahihi kuhusu hilo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share