Tashahhud: Kutikisa Kidole Katika Tashahhud Nini Hikma Yake?

 

 

 

SWALI LA KWANZA

 

 

Assalaam aleykum, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawaweza ili muweze kutusaidia.  Mwenyezi Mungu atawalipa InshaAllaah.

Swali langu ni hili, nini hikma ya kutikisa kidole wakati wa kutoa shahada, jee kuna dalili zozote. tafadhali naomba nifafanuliwe.

Ahsanteni

 

SWALI LA PILI:

salam alykum.ustadh  

swali jingine katika haitaiyatu yoyote ya kwanza au ya pili kukitetemesha kidole cha taiyatu ile ya fa au nimakosa?shukran

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tuangalie Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanyaje kwenye Tahiyyaatu kama inavyosimulia Hadiyth hii:

عن وائل بن حجر‏:‏  "أن رسول اللَّه صلى اللَّه عليه وآله وسلم  رفع إصبعه فرأيته يحركها يدعو بها"‏ - أبو داود والنسائي

Imepokewa na Waail bin Hujr kwamba, “Hakika (Mtume) (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinyanyua kidole chake (katika Tahiyaatu) na nikamuona akikitikisa, na akiomba kwacho.” [Imekusanywa na Abu Daawuud na An-Nasaaiy]

Hadiyth hii ndio ambayo inayowafanya wafuasi wa madhehebu ya Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) Kutikisa kidole katika Swalah zao na hili sio geni kwa mtu yeyote aliyesafiri pande za Sudan au kaskazini na Magharibi ya Afrika. Hadiyth hii baadhi ya Wanachuoni kama Imaam Al-Albaaniy kaiona ni sahihi lakini wengine wameiona ni dhaifu. Imaam huyo mkubwa wa Elimu ya Hadiyth Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake, “Sifa ya Swalah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika ukurasa wa 140 amesema hivi:

“Na ile Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akitikisa kidole, haikuthibiti upokezi (Isnadi) yake kama nilivyohakikisha katika kitabu (Dhwa’iyf Abi Daawuud) Hadiyth Namba 175, na hata kama ingethibiti basi ni Hadiyth yenye kukanusha (tendo) na Hadiyth (ya Waail) inathibitisha (tendo), na inayothibitisha siku zote inatangulizwa mbele ya inayokanusha kama ijulikanavyo na Wanachuoni.”

Kwa ufafanuzi zaidi angalia kitabu “Subulus-Salaam” cha mwanachuoni mkubwa wa ki-Shaafi’iy Amiyr Swan'aniy Juzuu ya 1 ukurasa 367.

 

Vilevile ni muhimu kufahamu kuwa, Hadiyth hiyo ya kutikisa kidole, imedhoofishwa na Wanachuoni wengine.

 

Hekima ya jambo lolote lililotajwa au kuharamishwa au kuhalalishwa, ni hayo maelezo yenyewe au uharamisho wake au uhalalisho wake maadam hakuna pahala palipotajwa hekima.

Tunajua hekima ya kuharamishwa pombe ni kuwa kuna madhara mengi ndani yake kuliko manufaa. Tumelijua hilo kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Amelieleza Mwenyewe. Na hatujui hekima ya kuharamishwa nyama ya nguruwe kwa sababu Allaah wala Mtume hawajalitaja ingawa watu wanajaribu kuchambua hoja mbalimbali, na wanasayansi wanagundua madhara mbalimbali.

 

Hivyo, tutabaki sisi kufuata hekima zile tu zilizotajwa, na kama hakukutajwa, basi tutajua hekima ni utiifu wa maelezo au uharamisho au uhalalisho uliotajwa ambao ni sahihi.

 

Katika suala hili la kutikisa kidole, kuna Hadiyth inayotaja hekima hiyo lakini ina utata. Na kwa kuwa ina utata kuhusu usahihi wake, basi sisi tunatakiwa tuamini kuwa hekima yake ni kule tu kujua kuwa zile Hadiyth za juu ambazo ni sahihi zinazothibitisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameonekana na Maswahaba akitikisa. Hiyo ni hekima tosha kabisa.

 

Kabla ya kukutajia Hadiyth hiyo yenye utata hapa chini, tunapenda kuwashauri Waislam kuwa wasiwe na tabia ya kutafutatafuta hekima na sababu na ‘kwa nini?’ na ‘vipi’  pale anapopata mafundisho ya jambo lolote la Dini yake ambayo ni sahihi. Maadam habari ni sahihi kama vile Qur-aan au Hadiyth, basi usitake kupekua sababu au hekima n.k.

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):

“Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi” [Al-Ahzaab: 36]

 Hadiyth hii ya kwanza inazidi kuelezea:

Kutoka kwa Abu Tha'alabah Al-Khushani Jurthuum bin Naashib (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye kapokea kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amefaridhisha mambo ya Dini kwa hivyo usiyapuuze. Vile vile kaweka mipaka usiikiuke. Amekataza baadhi ya mambo kwa hivyo usifanye.  Yale Aliyoyanyamazia ni kwa ajili ya huruma Zake kwako wala Hakusahau kwa hivyo usiyadadisi” Imesimuliwa na Daaraqutniy na wengineo.  Hadiyth Hasan

 

Na hii ya pili:

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah Abdur-Rahmaan bin Swakhr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

“Kile nilichokukatazeni kiepukeni, Na kile nilichokuamrisheni fanyeni kwa wingi kadiri muwezavyo. Hakika kilichowaangamiza watu wa Umma zilizopita, ni masuala (mahojiano) mengi na kupingana na Mitume yao. Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim

 

Hukufanya vibaya kuuliza, na unapouliza ndipo unapojua kuliko kunyamaza. Lakini sasa utakuwa umejua kuwa hakuna umuhimu wa kutafuta hekima katika mafundisho ya Allaah na Mtume Wake.

Hadiyth tuliyokwambia ina utata ni hii hapa chini japo kuna Wanachuoni walioisahihisha kama Imaam Al-Albaaniy, na hivyo ni bora kutoitumia kama dalili ya hekima ya kutikisa kidole.

 

النبي صلى الله عليه و سلم كان يحركها، و يقول : "(( لهي أشد على الشيطان من الحديد))  (يعني السبابة )  أخرجه احمد و البزار و غيرهما بسند حسن

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akinyanyua kidole chake cha shahada na kukitikisa akisema: ((Hichi ni kina nguvu zaidi kwa shaytwaan kuliko chuma)) [Ahmad na Al-Bazaar na wengineo kwa sanad hasan]

Pamoja na Ma-Imaam hao kuona ni Hadiyth nzuri, lakini wengine kama Imaam An-Nawawy katika Al-Khulaaswah na Adhw-Dhwiyaau Al-Maqdasiy katika Sunan Ak-Ahkaam wameona ni dhaifu.

Wa Allaahu A'lam

 

 


Share