Mume Ana Tatizo La Kumaliza Kabla Ya Mkewe Kwenye Tendo La Ndoa

 

SWALI: 

NAOMBA MSAADA WENU JUU YA TATIZO HILI. NASUMBULIWA NA KUFIKA HARAKA WAKATI WA JIMAI. MARA NYINGI NATOA MBEGU ZA UZAZI WAKATI WA KUMPASHA MOTO MWENZANGU. HII HUMFANYA MKE WANGU KUWA MZITO KATIKA KUSHIRIKI IPASAVYO KATIKA JIMAI KWANI ANACHELEA KUACHWA NJIANI KABLA HAJAFIKIA KILELE. JE KUNA NJIA GANI YA KUTUMIA ILI KUONDOKANA NA TATIZO HILI. NINAISHI DAR ES SALAAM TANZANIA. 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran sana kwa swali lako hili muhimu sana katika mas-ala ya unyumba. Hakika ni kuwa huko sikutoa siri bali ni njia ya kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Na tatizo kama hili au jingine lolote baina ya mume na mke hafai mmoja wao kumuogopa mwengine kwani kufanya hivyo ni kumeza ushingo bila kupata usaidizi aina yoyote.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) wametupatia njia za kuweza kutatua matatizo yetu ili tuwe ni jamii na familia bora za kuweza kuzungumza kwa hali ya uwazi, hivyo, kuweza kutazama njia bora na kusuluhisha mzozo au kutatua tatizo. Mke hafai kumuogopa mume ila tu anatakiwa amuheshimu au kwa usahihi zaidi waheshimiane. Lau kama mke angeweza kuzungumza na mumewe basi hili tatizo lingepata ufumbuzi. 

Tatizo la kukosa nguvu za uume lipo na lina sababu nyingi zinazopelekea hilo. Na pia mara nyengine mke pia naye hukosa shauku ya kulala na kustarehe na mumewe. Tatizo hili si kuwa haliwezi kutatuliwa, laa! Jambo hili lina dawa.  

Nasaha zetu ni kuwa mwanzo mume aende kwa daktari huenda ikawa ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa kufanyiwa operesheni au kwa madawa. Japokuwa madawa ya kuongeza nguvu za kiume mengi yana madhara kwa mwanamume mwenyewe yakitumiwa kwa muda. Ikiwa njia hii haikuweza kutatua tatizo hilo basi aende kwa matabibu ikiwa wapo katika sehemu anayoishi nao dawa zao zimejaribiwa. Mojawapo ya dawa hizo ni ile inayoitwa hawlinjaan. Hii anaweza kuchemshiwa na maji au ikatiwa katika maziwa akanywa nusu saa kabla ya jimai.  

Ikiwa njia zote hizo hazikufaa, mke na mume au wazazi wao wanaweza kukaa na kuzungumza jambo hilo ili mume amuache mke wake. Ikiwa haitafanyika hivyo mke atakuwa anadhulumika jambo ambalo halifai katika Uislamu. Kwa msingi wa Kiislamu mtukufu ni ile kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):

" Haifai kudhuru wala kulipana madhara" Ibn Maajah, Maalik na ad-Daraqutwniy). Kudhulumu na kudhulumiwa ni mambo ambayo hayafai kabisa katika Uislamu.  

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amuonyeshe dawa ndugu yetu na waendelee na ndoa katika hali iliyo nzuri kuliko awali na utesi na husma zote ziondoke na waweze kuridhishana kimapenzi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share