Nguo Za Kuswalia Zenye Picha Zinafaaa Kuswali Nazo?

 

SWALI:

 Nguo zenye picha kama vile picha ya mtu, mkono wa mtu n.k zinaswihi kuswalia?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali. Swali hili ni zuri hasa katika enzi zetu ambapo nguo zote zina mapicha ya hayawani.

Tufahamu kuwa picha zimekatazwa kwa kauli za wazi kabisa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baadhi yake ni:

  1. Imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika wanaotengeneza hizi picha wataadhibiwa Siku ya Qiyaama, wataambiwa vipeni uhai mlivyoviumba” (Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaa’iy).

 

  1. Amesema ama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifika, kutoka safarini, akanikuta nimeweka pazia yangu yenye mapicha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoiona uso wake ulibadilika rangi na kusema: “Ewe ‘Aaishah! Walio na adhabu kali kuliko watu wote Siku ya Qiyaama ni wale wanaoiga umbile Aliloliumba Allaah”. Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema: “Tukaikata, na tukafanya kutokana nayo mto, mmoja au miwili” (Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik na an-Nasaaiy).

 

  1. Amesema Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu): Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hakika aliye na adhabu kali zaidi ya wote Siku ya Qiyaama ni watengeneza picha” (Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy).

Picha zilizoruhusiwa ni zile za kuchorwa ni vitu vya visivyo na roho kama miti, milima, maporomoko ya maji, miji, majumba, magari na vitu vya namna hiyo kama tunavyoona katika Hadiyth ifuatayo:

Na amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Kila mwenye kutengeneza picha ataingizwa motoni, atajaaliwa kwa kila picha aliyochora nafsi itakayomuadhibu ndani ya Jahanamu”. Akasema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Na ikiwa huna budi ufanye (shughuli hiyo ya kuchora) basi tengeneza (picha ya) miti na vitu visivyokuwa na roho” (al-Bukhaariy na Muslim).

Kwa hiyo, picha za viumbe vyenye uhai havifai kutundikwa nyumbani, kuvaliwa kwenye nguo na kadhalika. Pia tufahamu kuwa Malaika hawaingii kwenye nyumba yenye picha hizo. Ama mtu akiswali na huku amevaa nguo yenye picha atapata madhambi kwa kufanya hivyo lakini Swalah yake itakuwa sawa na sahihi. Bila shaka, ikiwa picha au maandishi yatakuwa nyuma ya nguo yako madhambi yanazidi kwa kuwa yule anayeswali nyuma katika jamaa anashawishika kwa kuona yaliyo mbele yake. Na kumharibia Swalah madhambi yanarudi kwako.

Ni vyema sisi kama Waislamu tukaepuka na nguo kama hizo zenye picha zilizokatazwa.

Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

Hukmu Ya Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho

Malaika Hawaingii Nyumba Iliyotundikwa Picha Za Familia?

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share