Hadiyth Za Maamrisho Ya Kulala Upande Wa Kulia Na Hikmah Zake

 

 

Hadiyth Za Maamrisho Ya Kulala Upande Wa Kulia Na Hikmah Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Yote tunayoyapata kutoka katika Sunnah ya mwalimu wetu, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mafunzo yenye faida kwetu; ima faida ya nafsi zetu, au faida katika mwili wetu, au faida katika maisha yetu na faida kwa ujumla, bali kuna hikma kubwa kwenye mafunzo hayo. Kuhusu Hadiyth ifuatayo inayotoa mwongozo wa kulala upande wa kulia:

 

 

عن البراء بن عازب رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه و قال صلى الله عليه وسلم : ((إذا أتيت مضجعك فتوضأ وضوءك للصلاة ثم ثم اضطجع على شقك الأيمن ثم قل أللهم  أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت"   واجعلهن آخر كلامك فإن مت مت على الفطرة)) – البخاري و مسلم

Kutoka kwa Al-Baraa Bin 'Aazib (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah  kasema; “Utakapofika wakati wa kulala, tawadha kama wudhuu wa Swalaah, kisha lala upande wako wa kulia, kisha sema:

 

 

أللهم  أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت" 

 

 "Allaahumma aslamtu nafsiy Ilayka, wa-fawwadhwtu amriy Ilayka, wa-wajjahtu wajhiya Ilayka, wa-aljaatu dhwahriy Ilayka, raghbatan wa-rahbatan Ilayka, laa maljaa wa-laa manjaa Minka illa Ilayka, aamantu bi-Kitaabikal-ladhiy Anzalta, wa-bi-Nabiyyikal-ladhiy Arsalta"

 

“Ee Allaah, nimeisalimisha nafsi yangu Kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu Kwako na nimeutegemeza mgongo wangu Kwako, kwa matajarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako, nimekiamini kitabu Chako Ulichokiteremsha na Rasuli Wako Uliyemtuma.” Na fanya hivyo iwe ni maneno yako ya mwisho kwani ikiwa utafariki, utakufa katika Fitwrah (Uislamu]))”  [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

 

Hatuna shaka na tunaamini na kuyafuata mafunzo yake kadiri tuwezavyo kwani nani msemaye kweli kuliko Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) na Rasuli Wake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Rasuli ambaye hasemi kwa matamanio yake ila ni wahyi utokao kwa muumba wetu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anayesema:

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

Na wala hatamki kwa hawaa. Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa. [An-Najm: 3-4]

 

 

Basi hebu tuone hikma ya kutufunza kulala upande wa kulia kama wasemavyo wataalamu wa sayansi ya somo hili.

 

 

Ubongo (Brain)

 

Ubongo sehemu yake huwa upande wa kulia na ndio ambao unauongoza moyo ulioko upande wa kushoto.

 

 

 

Mapafu (Lungs)

 

Pafu la upande wa kulia wa mwili ni kubwa kuliko pafu la upande wa kushoto, kwa kuwa pafu la upande wa kulia lina sehemu tatu wakati ambapo la upande wa kushoto lina sehemu mbili tu.

 

 

 

Ini (Liver)

 

Ini liko upande wa kulia na ndilo tezi (gland) kubwa kubwa kabisa mwilini.

 

 

 

Nyongo (Gall Bladder)

 

Nyongo nayo ipo upande wa kulia na ina majukumu ya kutengeneza utomvu ambao unameng’enyua (digest) mafuta.

 

 

 

Matumbo (Intestines)

 

Matumbo (Intestines) Na Sehemu Ya Mwisho Wa Utumbo (Colon).

 

Sehemu ya 'mwisho wa Utumbo mkubwa' (Colon) na mwisho wa matumbo (Intestines) yako upande wa kulia. (Appendix) 

 

 

 

Moyo 

 

Moyo uko upande wa kushoto na ndio pampu la taratibu ya mzungukuo (Circulatory system).

 

 

Tumeona kwamba kwamba viungo vya mwili vikubwa viko upande wa kulia katika mwili, kwa hiyo mtu anapolala upande wa kushoto, huathiri viungo hivi na huleta madhara katika siha ya Bin-Aadam. Na juu ya hivyo mtu anapolala upande wa kulia huwa haileti shinikizo katika vyumba vya mapumziko ya moyo ambazo hufanya wepesi kazi ya Taratibu ya Mzunguko (Circulatory cycle).

 

 

Kwa hiyo mtu anayelala upande wa kulia anapoamka asubuhi huamka akiwa mwenye nguvu na mchangamfu.

 

 

Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tulizoamrishwa na mapendekezo ya kulala upande wa kulia:

 

 عن أبي  هريرة رضي الله عنه قال :" رأى رسول الله صلى الله عليه و سلم رجلاً مضطجعاً على بطنه فقال ((إن هذه ضجعة يبغضها الله و رسوله))". رواه الترمذي  .

 

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye kasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu amelala kifudifudi, akasema: “Kulala huku kunachukizwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli Wake”.  [At-Tirmidhy]

 

 

Pia,

 

عن  عائشة أن رسول الله  صلى الله عليه وسلم   "كان   إذاصلى  ركعتي    الفجر    (يعني سنتها)  اضطجع على شقه   الأيمن"  - صحيح البخاري

Imetoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akishaswali rakaa mbili za Alfajiri, (yaani Sunnah za Alfajiri) hulala upande wa kulia. [Al-Bukhaariy] 

 

 

Pia,

 

عن أبي أمامة قال: مر النبي صلى الله عليه وسلم على رجل نائم في المسجد منبطح على وجهه فضربه برجله وقال: (( قم أو اقعد فإنها نومة جهنمية))  مسند أحمد وسنن ابن ماجه

Kutoka kwa Abu Amaamah kasema; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipita kwa mtu mmoja ambaye alikuwa amelala kifudifudi msikitini akamshitua kwa mguu akasema: “Inuka au kaa kwani kulala huku ni kama kulala kwa watu wa motoni” [Musnad Ahmad na Sunan Ibn Maajah]

 

 

Na vile vile,

 

وعن حفصة رضي الله عنها قالت:" كان النبي صلى الله عليه وسلم إذا أخذ مضجعه جعل يده اليمنى تحت خده الأيمن" رواه الطبراني، صحيح الجامع  

Kutoka kwa Mama wa Waumini Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye kasema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kulala huweka mkono wake katika shavu la kulia. [At-Twabraaniy katika Swahiyh al-Jaami'y]

 

 

Hikmah Ya Kuwezesha Qiyaamul-Layl (Kisimamo Cha Usiku Kutekeleza 'Ibaadah)

 

Amesema Imaam Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah): "Kulala kwake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ubavu wake wa kulia kuna siri, nayo ni kuwa moyo unakuwa juu kwa upande wa kushoto, kwa hivyo, ikiwa atalalia ubavu wake wa kushoto basi usingizi utakuwa mzito; kwani atakuwa katika hali ya utulivu na ushwari na hivyo kuwa usingizi wake ni mzito. Na kama atalala kwa upande wa ubavu wake wa kulia, basi atakuwa katika hali ya wasiwasi na usingizi wake utakuwa si mzito kwa kuwa moyo utakuwa katika hali ya wasiwasi na atahitajia utulie na moyo kupondokeka kwake. Ndio sababu madaktari walipendelea kulala upande wa kushoto kwa sababu ya kupata usingi mnono na kupumzika vizuri kwa raha. Amma Swahibu wa Shariy’ah (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapendelea mzuri kulala upande wa kulia ili usingizi wake usiwe mnono akaja kupitwa na Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usikku kuswali).  Kwa hivyo kulala upande wa kulia kunafaidisha zaidi moyo, na upande wa kushoto ni faida zaidi kwa mwili. Na Allaah Anajua zaidi [Zaad Al-Ma’aad: (1/321)]

 

 

 

Share