Hijaab Na Hoja Za Mwanamke Kutokutekeleza Hijaab

 

Hijaab Na Hoja Za Mwanamke Kutokutekeleza Hijaab

 

Ummu ‘Aliy

 

Alhidaaya.com

 

 

Ingelikuwa kaka zetu na dada zetu wa Kiislamu wana hayaa, basi jamii yetu ingeongoka katika njia ya haki. 

 

Maadui wa waislamu wanapotaka kuangamiza kitu, kitu cha kwanza wanachoathiri ni mwanamke! Kwasababu mwanamke akipoteza stara yake, ni rahisi kwa vijana pia kupotea, hivyo basi ni rahisi kwa jamii nzima kupoteza stara yao. Kwahivyo tukisema stara kwa mwanamume ni waajib, basi kwa mwanamke pia ni waajib. Kwa ajili ya kuwajibika mwanamke kuwa na hayaaa, ni rahisi kwake kuwa karibu na stara. Na kitu muhimu kabisa kwa mwanamke ni nini?

 

Ni kujihifadhi na kujifunika mwili wake. Kitu kikubwa anachomiliki mwanamke, ni Hijaab yake. Kwa kaka na dada wanaosoma haya, someni na muwafahamishe dada zenu na jamaa zenu. Na dada yangu katika Uislamu, ikiwa unasoma haya, ilihali wewe ni muhajjabah (mwenye kutekeleza vazi la Hijaab), basi eneza risala hii kwa dada zako wa kiislamu, na ikiwa wewe sio muhajjabah, basi jaribu upate faida kutokana na haya.
 

Kitu kilichotukuka kabisa ambacho mwanamke anamiliki, ni stara. Na kitu cha thamani katika stara ni Hijaab. Nikikuuliza kitu gani cha thamani unachomiliki, itakuwa ni nini? Ukiwa na kitu cha thamani, utakitunza na kukihifadhi? Utakificha au la? Ukiwa na lulu au johari, je, utaihifadhi mahali pazuri au la? Kila thamani yake ikizidi, basi utazidi kutaka kuihifadhi. Kwa hiyo je, si, utaificha watu wasiione? Au utaionyesha na kuiweka wazi mbele ya kila mtu aione na achukue atakacho kutokana nayo?

 

Hakika utaihifadhi! Vile vile, mwanamke ni kiumbe mwenye thamani kubwa kwa hivyo inampasa ajihifadhi.

 

 

Ee dada yangu, je, unajua kama lulu inahifadhiwa na kaka (ganda) lake? Kweli au si kweli? Kwa hivyo huwezi kuwa bila ya Hijaab kwani Hijaab inakuhifadhi na fitna nyingi.

 

 

Mwanamke ni lazima ajistiri kwa kuvaa vazi la  Hijaab kwasababu ni rahisi sana mwanamume kumtongoza yeye kwa uzuri wake.

 

 

Kabla ya Uislamu kutujia, mataifa mengi yaliamini kuwa uzuri wenye thamani unapatikana katika mwili wa mwanamke peke yake. Uislamu ulipokuja ulibadili fikra hizo kwa kufundisha watu kuwa uzuri wa mwanamke sio wa mwili peke yake, bali ni wa tabia, fikra na mengineyo mengi.

 

 

Haijaandikwa kabisa Shariy’ah ya kuwa mwanamke lazima ajioneshe uzuri wake. Hakuna apasae kuuona wala kuufaidi uzuri wake ispokuwa mumewe.

 

 

Watu aina gani wanampa mwanamke heshima anayostahiki? Watu ambao wanamfanya mwanake ajioneshe uzuri wake, au wenye kumfundisha ajistiri uzuri wake ila kwa wale wanaostahiki kumuona uzuri wake? Wengine wanadai kuwa Hijaab sio wajibu. Tuangalie Qur-aan inasema nini kuhusu Hijaab. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59].

 

 

Tuzingatie kuwa Allaah ('Azza wa Jalla)  anapozungumzia kuhusu Hijaab kuwa ni waajib, Amejumuisha wanawake wenye kuamini pia, sio wake za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    peke yake, kwa hivyo ni wazi kuwa Aayah hii haikuteremshwa kwa jamii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) peke yao, bali imeteremshwa kwa ajili ya kuhifadhi wanawake wote. Kwa hivyo wanawake wote wenye kuamini ni lazima watekeleze vazi la Hijaab ili waheshimiwe na wajulikane kuwa ni wenye hayaa. Hakuna atakayemdhuru kwa ajili ya heshima aliyojiwekea juu ya mavazi yake.
 

 

Hijaab ni lazima! Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu.  [An-Nuwr: 31].

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Aliposema wanawake wavae Khimaar, Hakumaanisha kuwa wavae leso (kanga) kubwa tu, bali ni kuwa mwanamke akivaa hiyo Khimaar, itamfunika mapambo yake muhimu, nayo ni masikio, shingo na kifua. Kwa hivyo, mwanamke akivaa kitambaa kidogo ambacho hakimsitiri mapambo yake hayo tuloyataja, basi hiyo sio Hijaab .

 

 

Baada ya kuona katika Qur-aan kuwa Hijaab ni waajib, inampasa mume kumhimiza mkewe na kumshawishi atekeleze vazi la Hijaab ili aheshimiwe na athaminiwe kuwa ni mchaji Allaah.

 

 

Katika Aayah  nyengine Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anawaamrisha wanawake wa Kiislamu wasioneshe mapambo yao kama walivyokuwa wakifanya wanawake wakati wa ujaahiliyyah (kabla Uislaam). Wanawake wa ujaahiliyyah walikuwa wakivaa nguo ndefu lakini mapambo yao yote yalikuwa yakionekana, kama vile shingo, masikio, nywele na kadhalika.

 

 

Aayah ya Hijaab ilipoteremka tu, wanawake wote walitoka huku wamejifunika kwa vazi la Hijaab. Wanaume waliposikia aya hiyo waliwaeleza wanawake maana yake, basi wanawake walikuwa tayari kufuata shariy'ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   kama Alivyoiamrisha katika Qur-aan. Madhali walikuwa hawana uwezo wa kununua nguo mpya, walinyanyua nguo zao kwa sehemu mbili ili watumie kama Hijaab.

 

 

Hiyo ni kinyume na vile wanawake wakisasa walivyo. Wao hutoa visingizio kwa kutovaa vazi la Hijaab inayotakikana. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  "Kikundi cha wanawake  hawatoingia Jannah. Hao ni miongoni mwa wale wanaovaa nguo za kubana, za kuonyesha mwili na hawafuati amri ya Allaah  ya kuvaa vazi la Hijaab. Hawataingia tu Jannah bali hata hawatasikia harufu ya Jannah ambayo  harufu yake husikilizana masafa ya mwendo wa miaka 500." [Muslim].    

 

Kutilia mkazo umuhimu wa kujifunika, Ilimbidi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lipige vita kabila moja la Kiyahudi ambalo lilimchezea shere mwanamke wa Kiislamu sokoni. Walimfanyia hila huyo mwanamke kwa kuifunga nguo yake ili akitembea aanguke na nguo yake ipasuke kisha awe uchi. Basi mwanamume mmoja aliyeshuhudia hayo, alipigana na kumuuwa yule Yahudi aliyefanya mambo hayo. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   aliamrisha jeshi lake liwafukuze kabila hilo la Kiyahudi nje ya Madiynah.

 

Baadhi Ya Hoja Za Kutovaa Vazi La Hijaab.

 

 

1-Sijakinaika Na Amri Ya  Hijaab

 

 

Jibu:

 

Sasa nitakuuliza wewe ni nani? Utajibu wewe ni Muislamu. Uislamu unaamanisha nini? Uislamu ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa mambo yote Aliyotuamrisha. Na kuvaa vazi la Hijaab ni mojawapo ya maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Na ukiulizwa je, unakula nyama ya nguruwe? Utajibu: “Allaah Ameamrisha tusiile ni haraam.” Basi  na hijaab pia ni jambo Aliloamrisha Allaah ('Azza wa Jalla) na kutokuvaa vazi la hijaab ni inakuwa ni jambo Aliloharamisha. Kwa hiyo wewe utakuwa ni wale wanaofuata baadhi ya amri za Allaah ('Azza wa Jalla) na kuacha baadhi yake kama Anavyosema:   

 

أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ ۚ فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ ۗ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٨٥﴾

 Je, mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakanusha baadhi yake? Basi hapana jazaa ya anayefanya hayo miongoni mwenu isipokuwa hizaya katika dunia, na Siku ya Qiyaamah watapelekwa kwenye adhabu kali zaidi, na Allaah si Mwenye kughafilika kuhusu myatendayo.   [Al-Baqarah: 85]

 

 

2. Muhimu Ni Niyyah Yangu Nzuri Naswali Nafanya Mema Na Kadhaalika;

 

 

Jibu:

 

 

Mwanamke ambaye anadai kuwa kitu muhimu ni niyyah yake, na kuwa dhamira yake sio mbaya na kuwa yeye ni mtu mzuri, na kuwa Hijaab ni ya moyo. Mwanamke huyo huyo anadai kuwa anaswali Swalaah tano, Swalaah za Sunnah  na Swalaah za usiku na anatoa swadaqah. Kweli anafanya yote hayo, lakini kisha anasema ‘ibaadah hizo zinatosha, Subhaana Allaah!  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

قُل لَّا يَسْتَوِي الْخَبِيثُ وَالطَّيِّبُ وَلَوْ أَعْجَبَكَ كَثْرَةُ الْخَبِيثِ ۚ فَاتَّقُوا اللَّـهَ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿١٠٠﴾

Sema: Haviwi sawasawa viovu na vizuri japokuwa utakupendezea wingi wa viovu. Basi mcheni Allaah, enyi wenye akili ili mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 100]

 

 

Kwa hivyo tufanye hisabu, unasema unafanya mengi mema, kuwa niyyah yako ni nzuri na moyo wako ni msafi. Sawa, lakini kila siku unapotoka, wanaume wangapi wanakuangalia nywele zako, na uzuri wako wote, je unakusanya madhambi tele au la? Hakika unakusanya madhambi kwasababu hukufuata amri ya Allaah ('Azza wa Jalla). Na huyu mwanamke atashindana kuwa sio makosa yake wanaume wakimuangalia kwasababu niyyah yake sio mbaya, bali atasema kuwa wanaume ndio watakaopata madhambi. Laa hasha! Wewe ndio chanzo cha hao wanaume kukuangalia kwasababu hujavaa vazi la Hijaab na unawavutia wanaume. 

 

Mwanamke ambae havai vazi la Hijaab bila shaka anakusanya madahmbi mengi, kwasababu, wanaume wana nyoyo zenye matamanio na macho yenye kutamani. Hebu fikiria madhambi mengi vipi  anayakusanya mwanamke huyu. Je, yale mema yote yanamtosha yakilinganishwa na madhambi yake? Fikiria akitoka, ndani ya mabasi, ndani ya treni, kazini, barabarani, na kila pahali, madhambi mangapi atapata kwa kila mwanamume anaemuangalia uzuri wake akamtamani?

 

Allaah ('Azza wa Jalla) Hakukuamrisha uvae Hijaab? Nakuogopea kuwa mema yako yanaporomoka kutoka kwenye mfuko uliopasuka. Yale mema yanaingia kwa juu na kutoka kwa chini.

 

 

3-Joto Kali Mno Na Kuvaa Hijaab Inazidisha Joto Na Kunisababishia Madhara Mengineyo.

 

 

Jibu:

 

Mwanamke anaweza akalalamika kuwa nywele zake zinadondoka akivaa vazi la Hijaab kwa ajili ya joto. Baadhi yao husema: “Je, unataka niwe kipara sasa?” Ee dada, tambua kwamba kutokuvaa vazi la hijaab ni katika madhambi makubwa na hivyo Moto hautakuepuka na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema  kuwa Moto wa Jahannam ni mkali kuliko moto wa duniani:

 

  قُلْ نَارُ جَهَنَّمَ أَشَدُّ حَرًّا ۚ لَّوْ كَانُوا يَفْقَهُونَ﴿٨١﴾

Sema: Moto wa Jahannam ni mkali zaidi lau wangelifahamu. [At-Tawbah: 81]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  "Moto umezungukwa na matamanio yetu, na Jannah imezungukwa na juhudi zetu."

 

 

4-Kuvaa Hijaab Si Hoja Ya Kuwa Ndio Heshima:

 

 

Jibu:

 

Wengine husema kuwa wapo wanawake ambao wanavaa vazi la Hijaab lakini wana tabia mbaya kabisa. Kwa hivyo hawataki kuvaa Hijaab wakaonekana kama wao. Sasa basi kwa yule mwanamke anaedai  hayo:  Tunajua watu tele wanaoswali lakini wanafanya maasi. Je, basi  hiyo   inamaanisha sisi pia tusiswali? Wengine ni Hujaaji na wanafanya madhambi. Je, inamaana nasi tusiende kutekeleza Hajj? Kwa hivyo dada yangu Hijaab sio mbaya, bali mwenye kuivaa na kuiharibia sifa zake ndio mbaya.

 
5-Allaah Hajanihidi Bado Kuvaa Hijaab  

 

 

Jibu:

 

Laa dada yangu! Hiyo  ni makosa kabisa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa Habadili hali ya   watu mpaka wale watu     wabidili yaliyomo mwao:

 

  اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ  

Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao.   [Ar-Ra’d: 11]

 

Huwezi kuvaa  vazi la Hijaab mpaka ujitahidi. Haikubaliki kusema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hakunihidi bado, bali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekuongoza kiasi ya kuwa  unasoma makala haya. Sababu ya wewe kusoma haya ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anakufungulia njia ya kuhidika, Naye Hamuachi mja Wake ispokuwa Anamuonesha mwongozo. Kwa hiyo ni juu ya mja kufuata au kukanusha.

 

6. Nikiolewa Nitavaa Vazi La Hijaab.

 

 

Jibu: 

 

Wanaume wengi wanapotaka kuoa, hutafuta wanawake wanaojisitiri wenye taqwa na heshima kwa kufuata amri ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تُنْكَحُ الْمَرْأَةُ لأَرْبَعٍ: لِمَالِهَا  وَلِحَسَبِهَا   وَجَمَالِهَا  وَلِدِينِهَا. فَاظْفَرْ بِذَاتِ الدِّينِ تَرِبَتْ يَدَاكَ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah  (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Mwanamke huolewa kwa sababu nne; Kwa mali yake, nasaba yake [ukoo], uzuri wake na Dini yake. Tafuta mwenye Dini ubakie salama)). [Al-Bukhaariy na Muslim] (yaani usiharibikiwe katika maisha yako). 

 

Basi mwanamke asiyejisitiri kwa vazi la hijaab yuko mbali kupata mume atakayemlinda heshima yake. Kwa hivyo dada yangu tekeleza vazi la hijaab na chagua mume atakayelinda heshima yako na ambaye atafurahiwa kuwa wewe ni mutahajjibah.    

 

7. Mimi Bado Kijana Nataka Kustarehe Ujana Wangu!

 

 

Jibu:

 

Je, unajua lini utaiaga hii dunia dada yangu? Vifo vya vijana vimeenea! Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

Hakika Allaah Ana elimu ya Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34]

 

 

Na mshairi anasema katika beti zake:

 

 

تزَودْ من التقوى فإنكَ لا تدري ... إذا جنَّ ليلٌ هلْ تعيشَ إلى الفجر؟

 

Zidisha taqwa  kwani hujui

Usiku utakapokufunika, je, utaishi hadi Alfajiri?

 

فكمْ من صحيحٍ ماتَ من غيرِ علةٍ ... وكمْ من عليلٍ عاشَ حينًا من الدهرِ

Kwani wangapi waliokuwa na siha zao wamekufa bila ya maradhi

Na wangapi walio wagonjwa wameishi miaka?

 

وكمْ من صغارٍ يرتجى طولَ عُمْرَهْم ... وقدْ أُدْخِلَتْ أجسادَهُمْ ظُلمَة القبرِ

Na wangapi miongoni mwa wadogo wametumainiwa maisha marefu

Na miili yao imekwishaingia katika kiza cha kaburi

 

 

وكمْ من عرُوسٍ زَينوها لِزَوجها ... وقدْ قُبضَتْ أَرْواحَهُم ليلةَ القدرِ

Na bi harusi wangapi  amepambwa kwa ajili ya mume wake

Na roho zao zimechukuliwa usiku wa Laylatul-Qadri?

 

وكمْ من فتىَ أمسى وأصبحَ ضاحكًا ... وقدْ نُسِجَتْ أكفَانَهْ وَهوَ لا يدري

Na vijana wangapi wameamka huku wanacheka

Kumbe huku sanda yao inaandaliwa ilhali yeye hajui

 

 

ﻭﻛﻢ ﺳﺎﻛﻦٍ ﻋﻨﺪ ﺍﻟﺼﺒﺎﺡ ﺑﻘﺼﺮﻩ ... ﻭﻋﻨﺪ ﺍﻟﻤﺴﺎﺀ ﻗﺪ ﻛﺎﻥ ﻣﻦ ﺳﺎﻛﻦ ﺍﻟﻘﺒﺮ

Na wangapi asubuhi walikuwa katika maqasri yao wakikaa

Na jioni yakawa makazi yao ni kaburi?

 

 

فكن مخلصا واعمل الخير دائما...لعلك تحظى بالمثوبة والأجر
Basi kuwa mwenye ikhlaasw na utende mema daima

Huenda ukawafikishwa kupata thawabu na jazaa

 
وداوم على تقوى الله فإنها...أمان من الأهوال فى موقف الحشر

Na dumisha taqwa ya Allaah Kwani hiyo 

ni amani itakayokulinda na hali siku ya mkusanyiko (Qiyaamah)

 

 

8. Nataka Kufuata Fesheni, Nikivaa Hijaab Nitaoneka Sijaendelea!

 

Jibu:

 

Je, Rabb wako sio bora kuliko fesheni? Je, hujui kwamba mwenye vazi la hijaab anapendeza zaidi kulikoni anayejishauwa kwa vazi lisilo la sitara? Tena asiyevaa vazi la hijaab anadharaulika mbele ya watu khasa wanaume ndio wa kwanza kumdharau.

 

9.  Nataka Kuiga Watu Wa Magharibi

 

 

Jibu:

 

Nani anaemheshimu mwanamke zaidi? Uislaam au wale ambao hawawezi kuuza kitu bila ya kuweka picha ya mwanamke aliye kuwa tupu? Wao ndio wamempa mwanamke heshima au wamemdhulumu? Au Uislaam uliomheshimu mwanamke na kumpa daraja za juu na  kumstiri kutokana na kudhulumiwa? Na wanawake wangapi wa ki Magharibi wanaingia Uislamu sasa na wakafuata Uislamu kikamilifu, sasa je wewe dada yetu unataka kuwafundisha hawa ndugu zetu wapya kuwa hijaab haina umuhimu katika Dini yako?

 

 

10. Sitaki Kuvaa Hijaab Kwa Sababu Naogopa Nitaivua

 

 

Jibu:

 

Kwanini ee dada huvai vazi la hijaab huku  umetia niyyah madhubuti na huku unamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akuthibitishe nayo? Kuvua hijaab ni dhambi, na pia utakuwa umeonyesha mfano mbaya kwa wanawake wa kiislamu wengineo na wale wasio waislaam ambao huenda wakataka kuingia katika Uislaam.

 

 

11. Naona Hayaa Kwa Marafiki Na Watakayonisema.

 

 

Jibu: 

 

Ee Dada, je hutaona hayaa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Siku ya Qiyaamah?   Je, unakhiari uwaonee hayaa viumbe kwa kumuasi Aliyekuumba?
 

 

'Amali Za Kutenda Ambazo Zitakuwa In Shaa Allaah Ni Sababu Zitakazo Mwoongoza Mwanamke Wa Kiisilamu Kuthibitika Katika Vazi La Hijaab:  
 

 

1-Kuandamana na wanawake wenye taqwa wanaojisitiri na wenye elimu ya Dini.

 

2-Kuhudhuria darasa za Dini, kusikiliza mawaidha na kusoma makala za Dini.

 

3-Kuomba du’aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akuthibitishe katika Dini Yake.     

 

 

Masharti ya hijab ipasavyo katika Shariy’ah  ni kama yafuatayo:

 

1. Jilbaab liwe refu la kukufunika mwili mzima mpaka miguu, na kama halikufunika miguu basi mwanamke avae soksi.  

 

 

2.  Jilbaab liwe pana na sio lenye kuonyesha umbo, yaani lisiwe lenye kubana popote mwilini.  

 

 

3.  Jilbaab liwe zito na si jepesi la kuonyesha mwili.

 

 

4.  Jilbaab lisiwe na marembo yoyote yale ya kuvutia.

 

 

5. Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya makafiri.

 

 

6.  Jilbaab halitakiwi liwe ni katika mavazi ya fakhari.

 

 

7. Wanawake kutokuvaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.

 

  

8.    Kutotia manukato.

 

 

 WabiLLaahi At-Tawfiyq

 

 

Share