Uhakikisho Wa Kuvunjika Wudhuu Katika Swalah

 

SWALI: 

Nini au vipi kujua kuwa umetokwa na upepo na udhu wako unakuwa umevunjika? Nimesikia kuwa usikie sauti; hii sijafahamu, je ina maana usikie kwa sauti kubwa kuwa upepo umekutoka? Pia nitashukuru kupata maelezo ya upepo na harufu mbaya.

Jazzakallahu Khayr



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Hakika ni kuwa hakuna utata wowote kuhusu kutokwa na upepo kwani sehemu ya kutokwa na upepo huo unafahamika. Ipo sehemu moja pekee ambapo upepo unapotoka basi wudhuu huwa umetenguka (umevunjika). Sehemu hiyo ni ya nyuma ambapo upepo unapotoka inabidi mtu achukue wudhuu upya.

Kuna wakati mwingine sauti inasikika tumboni mwa Muislamu lakini kusikika huko hakuna wasiwasi wowote naye anaweza kuendelea  na Swalah yake.

Ama kwa yanayovunja wudhuu ni pale upepo unapotoka katika utupu wa nyuma ikiwa upepo wenyewe una harufu au la. Pia sauti inapotoka katika sehemu hiyo ikiwa sauti yenyewe inasikika au upepo wenyewe unatoka bila sauti.

Jambo hili linaweza kuhisiwa na mhusika mwenyewe kwani yeye ndiye mwenye kuhisi hayo na sio mwingine. Kwa hiyo, hayo yanapomkumba yeyote inabidi avunje swalah ikiwa yumo ndani yake ili akachukue wudhuu na ikiwa hayuko katika Swalah inabidi achukue wudhuu upya kabla ya Swalah atakayoswali.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share