Kiwango Gani Cha Mahari Atoe Mume Asiyejiweza?

 

SWALI:

 

Ndugu zangu waislamu, namshukuru Allah (S.W) kwa kuniweza kuwasiliana na waislamu wenzangu wa Alhidaya na nawaombea kila la kheri katika kazi yenu nzuri munayo ifanya na Inshallah Mungu atawazidishia na awaingiza katika nuru yake. Amin.

 

Mimi nina mchumba ambaye yuko tayari kunioa, ana mke na watoto na ni maskini ni mahari gani ammbayo nikimuitisha yatakuwa ni ubora kwake na kwangu. Mamangu yuwanisisitiza niseme anipe furniture kama mahari lakini kila nikiiangalia hali yake natatizika, nahitaji msaada wenu na Inshallah Mungu atawalipa kwa nia zenu nzuri katika dini hii yetu ya kiislamu. 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Tufahamu dada yetu kuwa mahari hayana kiwango chochote kilichowekwa na sheria. Mahari huwa yanategemea na mke na pia uwezo wa mume anayeoa. Kwa kuwa hiyo ni haki ya mke, yeye (yaani wewe) ndiye mwenye kusema anachotaka. Hata hivyo, mke anaposema mahari makubwa na mume akawa hana uwezo inakuwa ni shida kwake kuweza kutoa na ndoa hiyo huenda isiweko. Kwa kuwa hayo mahari ni haki yako unaweza kusema kile ambacho mwanamme anaweza kukupatia bila taabu hata kama ni pete ya chuma.

 

Tuelewe kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Wanawake wengi watukufu wenye baraka ni wale wenye mahari yaliyo madogo" (Ahmad, al-Bayhaqiy na al-Haakim).

 

Kwa hiyo, nasaha yetu kwako ni kuwa uyafanye mahari yako kwa kiwango ambacho atamudu atakayekuwa mumeo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share