Aliyeposa Kisha Akahutumiwa Kuwa Kambaka Mtoto

SWALI:

 

Asalaam alayku ama baada ya kumshuru Allah Subuhana Huwataala na kutakia rehma Mtume wetu Muhammad Salallah Alayhi Wasalaam. Napenda kuwatakia kila la kheri waislamu wote wa ujumla.

 

Swali langu lipo hapa me nina jamaa yangu alikuwa nataka kufunga ndoa na jamaa mmoja hivi yaani huyo bwana harusi ni jamaa yao. Sasa ikawa harusi bado kama wiki 2 hivi. Ikatujia habari kuwa bwana harusi amebaka mjukuu wa shangazi yake. Sasa wengine wanasema ni kweli na wako wanaosema si kweli. Yeye mwenyewe anasema si kweli yeye anamuachia Mungu tu na yupo tayari kula kiapo kwa kosa hili hajafanya. Sasa me swali langu lipo hapa. Kuna hukumu gani katika dini yetu. Je, huyu dada anaweza kuolewa nae au laa maana ndio harusi imevunjika na katika familia yao wako wanaosema bora aolewe nae na wako waosema arudishiwe pesa zake. Je hukumu yake na huyo bint alibakwa ni mke wa mtu na anasema kuwa anamuekea kisasi hata siku yoyote yeye atamlipizi. Je, nini hukumu yake hapa? Naomba utsaidie.


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu posa, harusi na kubaka. Hakika mara nyingi huwa tunajitia katika shida kwa kushindwa au kutotaka kufuata maagizo ya kisheria. Kitendo cha uzinzi (zinaa) si kitendo kidogo katika sheria yetu na sheria hakuacha mlango huo kwa dhana na fikra zetu. Mwanzo tayari kuna utata kama huyo bwana harusi amefanya kitendo hicho au hakufanya. Yeye mwenyewe anasema hajafanya, hivyo inatakiwa tuwe na dhana nzuri kwake.

 

Ama katika sheria, kitendo cha zinaa ni lazima kishuhudiwe na Waislamu wane, waadilifu, walio baleghe na wenye akili timamu. Ikiwa itakuwa wamepatikana hao, tatizo na utata wote utaondoka. Ikiwa hakuna ushahidi huo basi huyo kijana hana hatia yoyote. Tunaomba kila mmoja awe ni mwenye kusoma tafsiri ya Suratun Nuur (24): 1 – 10, kwa maagizo na mafunzo mengi ndani yake.

 

Kuondosha utata, huyo bwana anaweza kuozeshwa huyo msichana. Na ikiwa familia ya msichana pamoja na msichana mwenyewe amekuwa hataki tena kuolewa na huyo kijana, inabidi harusi hiyo ivunjwe na huyo kijana arudishiwe pesa zake na pia uhasama usiwepo.

 

Kwa kuwa sisi tuko mbali hatuwezi kusema zaidi ya hayo. Kwa kupata ufumbuzi wa hayo, inabidi kesi hiyo ipelekwe kwa Qaadhi kama wapo sehemu mnayoishi. Ikiwa hawapo basi pateni Shaykh mwadilifu ili aweze kuwatatulia hayo mengine.

 

Twawatakia kila la kheri katika kupata suluhisho kwa hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share