Hukmu Ya Kuishi Na Mume Asiyeswali Wala Kufanya Ibada Yoyote

SWALI:

amani juu yenu alhidaaya nyote, MWENYEENZI MUNGU awajaze kheri inshaalla, mimi nimeolewa miaka 15 iliyopita na alhamdulilah nimepata watoto wanne, lakini maisha yangu si ya furaha kwani mume wangu hafanyi ibada hata moja, haabudu hata  sala, zaka, apenda muziki na mpira tu nimemaliza mbinu zote nimeshindwa, ila nashukuru Allah watoto wote wamenifuata mimi na mashaalla wamekuwa watoto wazuri sasa yeye nimfanyeje? Nimemaliza hila zote.

Wabilahi taufiq

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Hakika ni kuwa haya ni matatizo ambayo yamewakumba wanandoa kwa kiasi kikubwa katika jamii yetu. Suala hili tumelielezea katika maswali mengi yanayotujia kuhusu matatizo na changamoto wanazokumbana nazo wanandoa.

 

Tatizo hili linapatikana kwa kuwa mvulana au msichana wakati wa harusi hawatazami yale yaliyosemwa na Uislamu kuhusu suala la uchaguzi. Zile sifa zilizoelezwa na Uislamu kuhusu uchaguzi huwa tunazipuuza na hivyo kukumbana na matatizo hayo baada ya nikaha (Nikaah). Mara nyingi huwa hatujali katika uchaguzi wetu kutazama maadili ya Kiislamu na dini unapopeleka posa au kuposwa. Bali kutazama vigezo vingine, nasaba, uzuri  au cheo cha mtu na hivyo mwisho wake ni kudhalilishwa na Allaah Aliyetukuka. Ni muhimu kwa kila msichana au mvulana kabla ya kuolewa au kuoa kumchunguza mchumba wake kabla kuingia katika ahadi ya kukaa pamoja kama wanandoa.

 

Bila shaka tatizo hili tayari ulilolitaja limetokea na tusigange yaliyopita bali yajao. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa linalotokea usiseme kama ningefanya kadhaa ingetokea kadhaa, bali sema limekadiriwa na Allaah na Atakalo Hufanya. Hakika lau hufungua mlango wa shetani (Muslim).

 

Dini ni nasaha na bado tunaona ipo haja na umuhimu wa wewe kuzungumza naye tena kama mumeo. Tunaona njia zifuatazo zinaweza kukusadia:

 

  1. Zungumza naye ana kwa ana na kinaganaga bila kusita na kuficha ili mupate ufumbuzi. Ikiwa haukupatikana, basi
  2. Jaribu kutumia marafiki zake wanaosikilizana naye ili wamueleze hayo.
  3. Itisha kikao baina yako, yake na wawakilishi wako na wake. Wawakilishi wanaweza kuwa ni wazazi wenu, walezi, au jamaa wa karibu wa kila upande. Ikiwa suluhu haikupatikana, basi
  4. Peleka mashtaka yako kwa Qaadhi au ili asikilize kila upande na baada yake atoe uamuzi. Ikiwa hakuna Qaadhi basi tafuta Shaykh muadilifu, mwema na mcha Mungu.

 

Jiwekee muda kwa kila kipengele huku ukiwa na shauku kubwa kuwa mumeo naye aongoke na kuingia katika Dini kikamilifu. Pia usisahau kumuombea kwa Allaah Aliyetukua Amuongoe katika njia nyoofu. Kwa juhudi hizo huenda Allaah Aliyetukuka Akakusikiliza kwani Yeye Mwenye kujibu maombi yetu kwa njia tofauti.

 

Baada ya kufanya hayo yote na ukawa hujafanikiwa basi itabidi uepukane na mume huo kwani si kheri nawe. Tufahamu kuwa tofauti baina ya Uislamu na ukafiri ni Swalah. Hakika ni kuwa huku kuacha kutoa Zakaah kwa makusudi pia ni kutoka katika Uislamu. Na tunakumbuka Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipigana na watu walliokataa kutoa Zakaah kwa sababu aliamini kuwa kufanya hivyo ni kuritadi.

 

Kwa hivyo, mume anayeacha kuswali na kutoa Zakaah na pia kufanya Ibadah nyingine si kuishi naye.

 

Ama kuhusu maasi mengine kama kusikiliza muziki, sio maasi ya kumtoa Muislamu katika dini yake, bali anapata dhambi kutokana na kiasi cha maasi yenyewe. Pindi atakapotimiza fardhi zake hizo, basi unaweza kuchukua hikma ya kusema naye kwa uzuri katika jambo hili na mpatie makala ifuatayo atambue dhambi na athari zake:

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

 

 

Tunamuomba Manani Akupatie subira na uvumilivu wa hali ya juu na Amrekebishe mumeo awe ni Muislamu mwema pamoja na wengine kama yeye.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share