Ndoa Bila Ya Radhi Ya Mama Inajuzu?

 SWALI:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Je ndoa ambayo mama hakuiruhusu ifungwe inahesabika na Allaah (SW) kama ni ndoa?

 

 

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

 

Ndoa katika Uislamu ni Ibadah kama Ibadah nyingine yoyote ile. Ibadah zote zina masharti ambayo yakitimia basi Ibadah hiyo imekuwa sahihi na sawa machoni mwa sheria. Ikiwa ipo sawa machoni pa sheria basi huwa imemridhi Allaah Aliyetukuka.

 

Miongoni mwa masharti ya kusihi ndoa ni kama yafuatayo:

 

1.  Idhini ya walii kwa mfano baba, ikiwa hayupo jamaa wa baba wa karibu anashikilia mahala pake kama babu, kakake shakiki na mfano wao.

2.  Kupatikana mashahidi wawili waadilifu

3.  Kuridhika kwa msichana au mwanamke (wewe mwenyewe).

4.  Mume kukupa mahari utakayoridhia au muliyokubaliana.

Ikiwa ni mwanamme basi sharti la kwanza huwa halipo kwani yeye hahitaji walii, walii huwa ni wa mwanamke anayeolewa.

Baada ya kusema hayo, inafaa ifahamike kuwa ndoa ni kujenga mahusiano baina ya familia mbili. Kwa hiyo, kizazi kinachozaliwa kinatakiwa kiwe ni chenye kufungamana baina ya upande wao wa baba na mama. Inakuwa dhiki kwa wajukuu ikiwa hawataweza kwenda kuwazuru bibi zao kwa kuwa ndoa yao haikuridhiwa na mama wa bwana au bibi harusi.

Ni muhimu kwa wanandoa wajenge mahusiano mazuri baina ya familia hizo mbili. Kwa kifupi ndoa ambayo inapingwa na mama inakuwa sahihi maadamu masharti yote yamepatikana lakini huwa haipendezi kwani unavunja uhusiano na mtu aliye muhimu katika maisha yako.

Nasaha yetu ni kuwa ikiwa msichana anaolewa na mama amekataa ajaribu njia zote za kumkinaisha kuwa chaguo lake ni la sawa kama kumtumia watu wake wa karibu na watu amabo anawatambua na kuwaamini. Kufanya hivyo kunaleta mahusiano mema baina ya familia mbili hizo.

Na Allaah Anajua zaidi 

 

Share