Mume Hampi Matumizi Wala Kumsaidia Kwa Lolote Afanyeje?

 

SWALI:

mimi nina mume lakini hanipi matumizi kabisa na pesa anayo je nikimuacha ni mbaya manake hataki kuniacha na tuna mda wa miezi sita toka tuowane na mimi namtimizia kila kitu lakini hanisaidii kwa lolote je nifanye nini? Asanteni ndugu zangu waislam

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu aliyeuliza swali lakehili kuhusu talaka. Ni masikitiko kuona kwamba ndoa ambayo inaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi kuvunjika baada ya miezi peke yake.

Yaonyesha kwa hakika kuwa tunahitaji katika jamii yetu malezi ya kijamii kwa kiasi kikubwa. Tatizo hili huenda limeanza kuanzia katika majumba ya wazazi wetu nasi tukayarithi kwa ujumla wake. Kisha tatizo jengine linakuja katika mas-ala ya kuchagua mchumba. Hapa huwa tunakosea sana kiasi ya kwamba hatuchaguani kwa maadili ya Kiislamu, hivyo huwa tunashindwa baada ya kuoana kuishi pamoja. Kwa hiyo, pindi posa inapokuja kwa sababu za kidunia huwa tunakubali kuingia katika majukumu ambayo hatuko tayari kuwa nayo.

Mbali na hayo, hatufundishwi majumbani kwetu namna ya kuishi na mume au mume kuishi vyema na mke. Kwa ajili hiyo huwa linapotokea tatizo huwa mara moja kutaka ima kuacha au kuachwa bila ya kuchukua hatua zifaazo. Katika maisha ya wanandoa ni wajibu na si ihsani kwa mume kumpatia yote anayohitajia mke katika mambo ya dharura na msingi wa maisha kama chakula, malazi, matibabu na kadhalika. Ikiwa mume hataweza kumtimizia hayo basi inafaa amuache mkewe kwa wema au mke kuomba talaka kupitia kwa Qaadhi ikiwa mume hataki kuitoa hiyo talaka.

Ama kwa mujibu wa hayo uliyotuelezea tunaweza kukupatia ushauri ufuatao:

  1. Awali ya yote, swali Swalah ya Istikhaarah kumtaka Allaah Aliyetukuka ushauri kuhusu mume wako na lipi lenye kheri nawe, talaka au kubaki naye.

  1. Jaribu kuzungumza na mumeo kinaganaga kama mume na mke kuhusu haki zako hizo ambazo umewekewa na sheria.

  1. Ikiwa hatokujibu chochote au hatobadilika katika kipindi fulani basi chukua hatua ya pili kwa kuitisha kikao. Kikao chenyewe kitakuwa baina yako, mumeo, mwakilishi (wawakilishi) wako na wake. Lau mnataka suluhu na maafikiano basi Allaah Aliyetukuka Atawasahilishia kupata hayo.

  1. Ikiwa hatua ya pili haikuleta natija basi itabidi uende kwa Qaadhi ili umuelezee yanayojiri kwa ajili ya kupata ufumbuzi. Lau upo sehemu ambayo hakuna Qaadhi basi utakwenda kwa Shaykh muadilifu ambaye atawasikiliza nyote wawili na kutoa uamuzi kulingana na sheria ya Kiislamu.

Katika kila hali tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie jambo lako hilo na Akupatie tawfiki ya kuweza kuelewana na kuishi pamoja katika nzuri ya masikilizano.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share