001-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Utangulizi Wa Mfasiri

 

Utangulizi Wa Mfasiri

 

 Alhidaaya.com

 

 BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym

 

 

Hakika shukurani ni Zake Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa), tunamshukuru Yeye, na kumtaka msaada, na tunamuomba Yeye msamaha. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atulinde na shari za nafsi zetu na ubaya wa matendo yetu. Anayeongozwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hakuna wa kumpoteza, na anayepotezwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi hakuna wa kumuongoza.

 

Na nashuhudia kuwa hakuna apasaye kuabudiwa ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Ni Mmoja tu Asiye na mshirika. Na nashuhudia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja Wake na ni Mjumbe Wake. Swalah na Salaam za Allaah zimshukie yeye, jamaa zake, Swahaba zake, na wote waliotangulia kwa wema hadi siku ya mwisho.

 

Ama ba’ad,

 

Namshukuru tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuniwezesha kukamilisha kazi hii kwa Lugha ya Kiswahili, kazi ambayo naamini sana kuwa itawanufaisha sana Waislam wazungumzaji wa lugha hii na kuweza kuwasaidia kupata mafunzo sahihi ya 'Ibaadah hii adhimu ambayo itakuwa ni jambo la kwanza kabisa kwa mja kuulizwa kwalo siku ya Hesabu.

 

Umuhimu wa kitabu hiki ni mkubwa sana, haswa kwa kuwa ni kitabu kilichoelezea ‘Ibaadah hii ya Swalah kwa mapana na marefu na kwa dalili sahihi zilizothibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kitabu kwa mwenye kutaka kujua ilivyokuwa Swalah ya kipenzi chetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) kama alivyosema: (Swalini kama mlivyoniona nikiswali) [Al-Bukhaariy]. Basi anapaswa kuwa nacho kwenye nyumba yake.

 

Hiki ni kitabu cha Swalah kilichoenea na kuuzika kwa wingi sana labda kuliko vitabu vyote vya Swalah vilivyowahi kuandikwa. Ni kitabu chenye mauzo makubwa katika nchi za Kiarabu kwa mujibu wa wachapishaji wa kitabu hicho. Hali kadhalika kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kimeuzwa na kinaendelea kuuzika kwa wingi katika nchi za Ulaya na haswa Uingereza. Nimeonelea manufaa hayo yasiwaenee tu wenye kuzungumza Kiarabu na Kiingereza pekee, bali na jamii yetu ya wazungumzao Kiswahili.

 

Swalah ina fadhila kubwa sana, hivyo kukosa kuswali ni kosa kubwa. Swalah ni 'amali ya kwanza itakayokaguliwa Siku ya Qiyaamah na ndio ufunguo wa Jannah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

’Amali ya mwanzo atakayoulizwa Muislamu Siku ya Qiyaamah kuwa kaitekeleza–na kaitekeleza vilivyo–ni Swalah. Ikiwa aliitekeleza vilivyo basi kunatarajiwa atafaulu. Ikiwa hakuitekeleza au kaitekeleza, lakini sivyo ndivyo, basi itatazamwa Swalah za Sunnah, kama alizitekeleza vilivyo. Ama ikiwa hana hata Sunnah au kaitekeleza sivyo ndivyo, basi keshapata khasara’ [Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Funguo za kufungulia milango ya Jannah ni Swalah” [Muslim].

 

Ubaya wa kuacha Swalah ni mkubwa sana kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلاَةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا  

Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni. [Maryam: 59].

 

Na kadhalika Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) kwa kutaja habari za wasioswali pindi watakapoulizwa sababu yao ya kuwepo motoni:

 

 مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾ قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾

 (Watawauliza):  Nini kilichokuingizeni katika motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Muddaththir: 42 -43].

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kizuizi kilichoko baina ya mtu na ukafiri ni Swalah” [Muslim].

 

Kadhalika akaeleza ubaya wa mtu kutokuswali na kumfananisha na kafiri: “Tofauti baina yetu Waislamu na wasio Waislamu ni Swalah”  [Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Baada ya kujua masuala hayo muhimu kutoka katika Kitaab na Sunnah, ndivyo vilevile tutaona umuhimu wa kuijua ‘Ibaadah hiyo vilivyo ili tuweze kuitekeleza ipasavyo. Na kwa mintarafu hiyo, tutaona kuna ulazima wa kupata mafunzo hayo kutoka katika chanzo kilichokamilika kwa dalili thaabit kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake. Na ndio nikakichagua kitabu hiki kukitafsiri ili kumuwezesha Muislam mwenye kusoma Kiswahili anufaike na aweze kuinoa na kuiboresha Swalah yake ili aweze kufikia makusudio yaliyotajwa katika Aayah na Hadiyth mbalimbali nilizotanguliza hapo juu, na pia ili aweze kuepukana na sifa na adhabu nilizotangulia kutaja.

 

Nisiwe mbakhili wa fadhila na mchache wa shukurani kwa wale waliotoa mchango wao mkubwa kabisa katika kazi hii tukufu. Nawaombea wote malipo kamili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yanayotokana na kazi hii, bila kukosa thawaab za wale wote watakaonufaika kutokana na ‘amali hii.

 

Shukurani zangu za dhati na du’aa zangu ni kwa dada yangu Ummu Iyyaad ambaye kwa juhudi zake zisizo mithali kazi hii imeweza kukamilika na pia ushirikiano wake mkuu wa dhati. Pia Al-Akh 'Abdullaah Mu'awiyyah na Al-Akh Fayswal ‘Abdul-‘Aziyz, kwa kujitolea wakati mkubwa kuipitia kazi hii. Pamoja na ndugu yangu mpenzi Sa’iyd Baawaziyr kwa kupitia vilevile na kuchangia maoni mbalimbali. Bila kusahau mchango mkubwa wa upitiaji na mawazo wa Al-Akh Muhammad Faraj As-Sa’ay. Hali kadhalika Al-Ukht Ummu ‘Abdir-Rahmaan kwa mchango wake.

 

Na shukurani nyingi kwa tashji’i kubwa na uvumilivu wa hali ya juu kutoka kwa mke wangu Ummu ‘Abdillaah ambaye amenisaidia kwa kiasi kikubwa na amenipa fursa ya kutosha ya kushughulika na majukumu haya matukufu bila kuchoshwa wala kuvunjika moyo. Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amlipe yeye na wote duniani na Akhera. Aamiyn

 

 

Abu ‘Abdillaah Muhammad Baawaziyr

 

Swafar 1429 H – Februari 2008 M

 

 

Share