002-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Historia Fupi Ya Mwandishi Wa Kitabu

 

 

Historia Fupi Ya Shaykh Al-Albaaniy

 

 

(Historia hii fupi ya Shaykh nimeitoa katika kitabu nilichoandika kuhusu maisha ya Shaykh kiitwacho Shaykh Al-Albaaniy – Mwanachuoni Wa Karne Ambacho kinapatikana katika tovuti ya www.alhidaaya.com na karibuni kitachapishwa in shaa Allaah)

 

Abu ‘Abdillaah Muhammad Saalim Sa’iyd Baawaziyr

 

Al-Imaam, Al- Muhadith, Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy

1332 H-1420 H – 1914 M-1999 M 

  

Jina Lake: Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy

Nasaba Yake: Al-Albaaniy (Kajulikana kwa jina la Al-Albaaniy kwa sababu asili yake ni mtu wa Albania)

Kun-Yah Yake: Abu ‘Abdir-Rahmaan (Baba ya ‘Abdur-Rahmaan’)

Wake Zake: Alioa wake wanne; watatu wa mwanzo walimzalia watoto, na wa nne ‘Ummu Al-Fadhwl’ hakujaaliwa kuzaa, na ndiye aliyeishi naye hadi alipofariki dunia.

Watoto Wake: Aliruzukiwa watoto 13; 7 wa kiume na 6 wa kike. Wa kiume ni: ‘Abdur-Rahmaan, ‘Abdul-Latwiyf, ‘Abdur-Razzaaq, ‘Abdul-Muswawwir, ‘Abdul-Muhaymin, Muhammad na ‘Abdul-A’alaa. Wa kike ni: Aniysah, Aasiyah, Salaamah, Hassaanah, Sakiynah na HibatuLlaah.

 

Mwanachuoni Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy Al-Albaaniy ni mmoja kati ya Ma’ulamaa wakubwa wa Kiislam katika zama hizi. Anahesabika kuwa ni Mwanachuoni wa Hadiyth maarufu kabisa katika fani ya elimu ya Jarh na Ta’adiyl.[1]

Shaykh Al-Albaaniy vilevile ni hoja katika elimu ya Mustwalahul-Hadiyth.[2] Na Wanachuoni wamemsifu na kuelezea kwamba kwa elimu yake hiyo, karejesha kumbukumbu za zama za kina Imaam Ibn Hajr Al-‘Asqalaaniy, Ibn Kathiyr na Wanachuoni wengine wakubwa wa fani hiyo.

 

Alikuwa na kumbukumbuku ya hali ya juu katika kuhifadhi vitu kichwani na mengine mengi. Kumbukumbu inayotukumbusha wema waliotangulia kama kina Ibn ‘Abbaas, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliofuatia kama Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Ash-Shaafi’y, Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam Ibn Kathiyr, Imaam An-Nawawiy na wengine (Allaah Awarehemu wote).

 

 

 

Kuzaliwa Na Kukua Kwake

 

 

Alizaliwa mwaka 1332 H – 1914 M katika mji wa Ashkodera ambao kwa wakati huo ulikuwa mji mkuu wa Albania huko Ulaya Mashariki na ukoo wake ulikuwa maskini. Baba yake aliyeitwa Shaykh Nuuh An-Najaatiy alihitimu katika chuo cha Shari’ah huko Istanbul, Uturuki, na kurejea kwao akiwa Mwanachuoni. Lakini baada ya mfalme Ahmad Zogo kutwaa madaraka ya nchi na kuendesha utawala wa nchi hiyo kikomunisti ikabidi baba yake (Shaykh Al-Albaaniy) ahamie Damascus, Syria. Wakati huo Shaykh Al-Albaaniy alikuwa na umri wa miaka tisa.

 

Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy alianza masomo yake ya awali katika madrasah ya Al-Is’aaf Al-Khayriyah hapo Damascus na kuendelea hadi alipomaliza na kuwa msimamizi wa chuo hicho hadi yalipoanza mapinduzi dhidi ya Ufaransa nchini humo. Madrasah hiyo ikakumbwa na maafa ya moto yaliyosababishwa na vurugu na machafuko katika vita hivyo. Baba yake akaamua kumuachisha masomo na akaanza kumsomesha yeye mwenyewe. Alimwekea ratiba kali ya masomo ambayo ni; Qur-aan, Tajwiyd, Swarf, Fiqh (ya Kihanafi, yaliyokuwa madhehebu ya baba yake aliyekuwa Mwanachuoni mkubwa wa madhehebu hayo). Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia masomo mbalimbali ya Dini na lugha kutoka kwa Wanachuoni wakubwa na Mashaykh waliokuwa marafiki wa baba yake kama vile Shaykh Sa’iyd Al-Burhaaniy ambaye alimsomesha masomo ya balaaghah na lugha.

 

 

 

Kujifunza Kwake Elimu Ya Hadiyth

 

 

Alitunukiwa shahada ya juu ya elimu ya Hadiyth kutoka kwa Shaykh Raaghib At-Twabbaakh, Mwanachuoni mkubwa wa Halab katika wakati huo. Hapo ni wakati alipokutanishwa naye kupitia Shaykh Muhammad Al-Mubaarak ambaye alimjulisha Shaykh At-Twabbaakh umahiri wa kijana huyo (Al-Albaaniy) katika elimu ya Hadiyth. Baada ya Shaykh At-Twabbaakh kumjaribu na kuthibitisha hilo mwenyewe, akamtunuku shahada (Ijaazah). Shahada hiyo si pekee, bali pia alipata kwa Wanachuoni wengine wakubwa wa Hadiyth kama Shaykh Bahjatul Baytaar (ambaye isnaad yake inafika hadi kwa Imaam Ahmad bin Hanbal).[3]

 

Aliingia kwenye fani ya Hadiyth akiwa na umri wa miaka ishirini. Aliathirika sana na tafiti mbalimbali za Muhammad Rashiyd Ridhwaa, Mwanachuoni wa Misr wakati huo. Tafiti hizo zilikuwa katika jarida la Al-Mannaar. Anasema Imaam Al-Albaaniy: “Nilichokimulika mwanzo miongoni mwa vitabu, ni vile vya visa vya lugha ya kiarabu, kama vile; Adhw-Dhwaahir, ‘Antarah, Maalik as-Sayf na vinginevyo kama hivyo. Kisha nikazama katika vitabu vya visa vya kijasusi vilivyotarjumiwa katika lugha ya Kiarabu. Siku moja nikapita katika vibanda vya kuuza vitabu na macho yangu yakaangaza kwenye jarida moja liitwalo Al-Mannaar na katika kupekuapekua ndani yake nikakutana na makala ya kitafiti ya Rashiyd Ridhwaa akikielezea kitabu cha ‘Ihyaa ‘Uluum ad-Diyn cha Abu Haamid al-Ghazaaliy, akitaja mazuri yaliyomo ndani ya kitabu hicho na kasoro zake. Kwa mara ya kwanza nikakutana na aina kama hii ya uchambuzi wa kielimu. Nilivutika sana na uchambuzi sampuli hiyo na ukanifanya nisome toleo zima la makala hiyo. Kisha nikawa nafuatilizia maudhui za uchambuzi wa Hadiyth wa Mwanachuoni Al-Haafidh Al-‘Iraaqiy alioufanya kwa Hadiyth zilizomo ndani ya kitabu Ihyaa ‘Uluum ad-Diyn. Sikutosheka hadi ikabidi nimuombe muuza duka aniazime jarida hilo kwa kuwa sikuwa na uwezo wa fedha wa kulinunua!

 

Hapo ndipo ilipoanza safari ndefu ya kusoma vitabu mbalimbali. Nikatoa nakala ya maudhui hiyo iliyofanyiwa uchambuzi wa kina katika jarida hilo”

 

Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia kwa baba yake elimu ya kutengeneza saa hadi akawa fundi mzuri maarufu kwa kazi hiyo. Ikawa ndiyo kazi iliyompatia rizki yake. Alikuwa fundi na hapo hapo mtafutaji elimu. Hali hiyo ikaendelea hivyo hadi alipoamua kutenga siku mbili tu za kufanya kazi ya kutengeneza saa, na siku zote zilizobaki zikawa ni za kutafuta elimu. Elimu hiyo alikuwa akiichukulia katika maktaba kubwa ya mji huo wa Damascus iliyoitwa Adhw-Dhwaahiriyah ambapo alikuwa akitumia siku nzima kusoma na kutafiti. Alishughulishwa mno na kusoma hadi akawa anasahau hata kula. Kilichokuwa kinakatisha utafiti na masomo yake ni vipindi vya Swalah tu. Mwishowe, wahusika wa maktaba hiyo wakamuamini na kuamua kumpa funguo zake awe anatumia maktaba wakati wa ziada, na akawa daima ni mtu wa mwisho kutoka na kufunga mwenyewe.

 

Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) zilikuwa zina athari kubwa sana katika maisha ya Shaykh kielimu na kiutendaji. Zikamuelekeza katika Manhaj (Njia, mwenendo) Sahihi; ambao ni kuchukua kutoka kwa Allaah (Qur-aan) na Mtume Wake (Sunnah) tu. Akipata usaidizi wa ufahamu wa vyanzo hivyo viwili vikuu kutoka kwa Maimaaam Wanachuoni katika wema waliotangulia (As-Salafu as-Swaalih) bila kuwa na ta’aswub (kasumba) ya kumshabikia yeyote miongoni mwao au kumponda yeyote, bali msimamo wake ulikuwa ni kuchukua haki popote ipatikanapo na kutoka kwa yeyote.

 

Kwa sababu hiyo, aliyaacha na kuyaweka pembeni madhehebu ya Kihanafi aliyokulia nayo na aliyosomeshwa na baba yake. Baba yake (Allaah Amrehemu), alikuwa akivutana naye sana juu ya masuala hayo ya kimadhehebu, kwani baba yake alikuwa ameshikilia kwa nguvu sana msimamo wa Kihanafi na hataki kusikia mingine hata iliyokuwa sahihi katika masuala mengine. Shaykh alijaribu sana kumfahamisha baba yake kuwa anapaswa kufanyia kazi Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) endapo itathibiti usahihi wake, na kuacha ya wengine wote kama hayawafikiani na maneno ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

 

Wanafunzi Wake Maarufu

 

Wanafunzi wake ni wengi sana na walio maarufu katika Mashaykh ni hawa ambao baadhi yao wako hai hadi leo:

Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi’iy (Yemen)

Dkt. ‘Umar Sulaymaan Al-Ashqar (Jordan)

Shaykh Saalim Al-Hilaaliy (Palestina)

Shaykh Hamdiy ‘Abdul-Majiyd

Shaykh Muhammad ‘Iyd ‘Abbaasy

Shaykh Muhammad Ibraahiym Shaqrah (Jordan)

Shaykh ‘Aliy Khushshaan

Shaykh Muhammad Jamiyl Zaynuu (Saudi Arabia)

Shaykh ‘Abdur-Rahmaan ‘Abdus-Swamad

 

 

 

Vitabu Vyake

 

Maktaba za Kiislam zimeneemeka kwa vitabu vingi vya Shaykh hususan vile vikubwa vyenye mijalada mingi vya ‘Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah’ na ‘Silsilat al-Ahaadiyth adhw-Dhwa’iyfah wal-Mawdhuw’ah’ na kitabu chake cha Swalah kiitwacho ‘Swiftatus Swalaatin Nabbiy[4] ambacho kimepokelewa kwa nguvu sana na wasomaji pande zote za ulimwengu, haswa vijana. Ni mojawapo ya vitabu vizuri na muhimu sana katika mafunzo ya Swalah kama ilivyoswaliwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Kadhaalika, Shaykh ana vitabu maarufu sana vya Hadiyth vyenye kuvifanyia sharh, tahkiki, na hata kubainisha yale ya sahihi na ya dhaifu ndani ya vitabu hivyo, kama alivyofanya kwenye vitabu Sunan At-Tirmidhy, Sunan Ibn Maajah, Sunan Abi Daawuud n.k. Vilevile ana mijalada mingi ya vitabu kama tutakavyoona hapo chini kwenye orodha fupi. Vilevile ameweza kutoa vitabu vya kufafanua na kusahihisha vitabu maarufu vya Wanachuoni wakubwa wa karibuni kama vitabu Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah’ kilichokuwa ni masahihisho ya Hadiyth zisizo sahihi katika kitabu cha Shaykh Sayyid Saabiq kitwacho Fiqhus-Sunnah’, na ana kitabu cha Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal Haraam ambacho ni usahihisho wa Hadiyth zilizomo katika kitabu cha Dr. Yuusuf Al-Qaraadhwaawiy kiitwacho Al-Halaal Wal Haraam Fiyl Islaam’.

 

Kazi zake za uandishi kuhusu masuala ya Hadiyth zinazidi zaidi ya mia.

 

Baadhi Ya Vitabu Vyake Vilivyoenea Sana Ni:

 

1- Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (Mijalada 1-11)

 

2- Silsilatul Ahaadiyth Adhw-Dhwa’iyfah wal Mawdhuw’ah (Mijalada 1-14)

 

3- Al-Irwaa Al-Ghaliyl (Mijadala 1-9)

 

4- At-Targhiyb wa At-Tarhiyb (Mijalada 1-4)

 

5- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Abi Daawuud (Mijalada 1-4)

 

6- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan At-Tirmidhiy (Mijalada 1-4)

 

7- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Ibn Maajah (Mijalada 1-4)

 

8- Mukhtaswar Swahiyh Al-Bukhaariy

 

9- Mukhtaswar Swahiyh Muslim

 

10- Sharhu Al-‘Aqiydah Atw-Twahaawiyah

 

11- Ahkaam Al-Janaaiz

 

12- At-Tawaswul: Anwa’uhu wa Ahkaamuhu

 

13- Kitaabu As-Sunnah

 

14- Swalaatu At-Taarawiyh (Qiyaamu Ramadhwaan)

 

15- Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah

 

16- Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal-Haraam

 

17- Adaabu Az-Zafaaf[5]

 

18- Swifatu Asw-Swalaatin-Nabiy[6]

 

 

 

 

 

 

 

Fadhila Na Mema Yake

 

 

 

Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) alikuwa ni mwenye kufuata mwenendo wa wema waliotangulia (Salafus-Swaalih), akifuata mwenendo wao na tabia zao, na yakawa macho yake yanafuata kilichosemwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na Mtume Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Alikuwa hastahi katika haki, akiitangaza haki katika vitabu na mihadhara yake. Hii ni sifa ya nadra sana kuipata katika ulimwengu wa leo, ambao wengi hawapendi kusema haki kwa kuchelea kuwaudhi wengine au kupoteza kukubalika. Shaykh alikuwa akijirudi pindi alipokutana na dalili sahihi inayokwenda kinyume na kauli yake, na aliacha kauli yake na kufuata dalili hiyo iliyosihi bila kuangalia imetoka kwa nani. Kuna baadhi ya Hadiyth alizokuwa akiitakidi kuwa sahihi kwa elimu yake, na baadaye zikambainikia au akatanababishwa kuwa si sahihi, akawa anajirudi haraka na kukubali na kuzitaja katika vitabu vyake.

 

 

 

 

 

 

 

Elimu Yake Na Athari Yake Kwa Watu

 

 

 

Shaykh alikuwa katika daraja ya Al-Haafidh (Mwanachuoni wa Hadiyth aliyehifadhi Hadiyth laki moja (100,000) pamoja na mnyororo wa wapokezi wake na mutuunzake (maneno ya kila Hadiyth). Hayo yanaelezwa na Shaykh ‘Ashiysh aliyemuuliza suala hilo na Shaykh akakataa kumjibu kwa unyenyekevu na kutotaka kujifakharisha, alichojibu baada ya kukazaniwa sana swali hilo, alijibu kwa Aayah hii: ((Na neema yoyote mliyonayo inatoka kwa Allaah)) [An-Nahl: 56].[7]

 

 

 

Katika wasia wake Shaykh alitoa hadiya maktaba yake ya vitabu na kazi zake za uandishi kukitunuku Chuo Kikuu Cha Madiynah Al-Munawarah kama alivyosema katika wasia wake: “Nimeiachia maktaba yangu – vyote vilivyomo, vikiwa ni vilivyochapishwa tayari, au nakala, au kazi nilizoziandaa kuchapishwa; kwa maandishi ya mkono wangu, au ya mwengine aliyeniandikia – kwa kuipa maktaba ya Jaami’atul-Islaamiyah (Chuo Cha Kiislam) kilichopo katika mji wa Madiynah. Kwa sababu ni kumbukumbu nzuri kwa chuo hicho wakati nilipokuwa huko nikifundisha, kwa kulingania kwake kwa msingi wa Kitaab (Qur-aan) na Sunnah kwa kufuata mwenendo (Manhaj) wa wema waliotangulia (Salafus-Swaalih)”.[8]

 

 

 

Alikuwa mtu wa kawaida sana, mnyenyekevu asiye na makuu na asiyetofautishwa na watu wengine ila kwa vitendo na maongezi yake ya kielimu.

 

 

 

Katika kipindi cha maisha yake, alifanya tafiti nyingi na kuzichambua taqriban silsilah 30,000 za wasimulizi wa Hadiyth (isnaad), akiwa ametumia kiasi cha miaka 60 ya umri wake kusoma na kupitia vitabu vya Sunnah na kuwa karibu navyo kwa muda wote huo, na mawasiliano ya nyanja hiyo, na pia kuwa karibu na Ma’ulamaa wa elimu hiyo.[9]

 

 

 

 

 

 

 

Sifa Njema Walizotoa Ma’ulamaa Kwa Mujaddid Wa Zama Hizi Shaykh Muhammad Naaswir-Ud-Diyn Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Bin Baaz [Aliyekuwa Mufti Wa Saudi Arabia] (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Sikumuona mtaalamu wa Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katika enzi yetu ya leo chini ya qubah la mbingu kama Mwanachuoni mkubwa Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Aliulizwa kuhusu Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) isemayo:

 

((Allaah Hutuma kwa Ummah huu Mwanachuoni katika kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya dini Yake)).[10] Aliulizwa ni nani mpiga msasa wa karne hii? Akajibu: Ninadhani Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ndiye mpiga msasa wa zama hizi. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

 

 

 

 

Mwanachuoni Shaykh Muhammad Ibn Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Yale niliyoyajua kuhusu Shaykh na ambayo ni kidogo wakati nilipokuwa nakutana naye, ni kuwa yeye ana shime ya hali ya juu ya kutumia Sunnah na kupiga vita bid’ah; sawasawa katika ‘Aqiydah au matendo. Ama kwa kusoma kwangu vitabu vyake, hakika nimemjua vyema kwa hayo. Ana elimu kubwa ya Hadiyth kwa upande wa Riwaayah na Diraayah. Allaah Amewanufaisha watu wengi kutokana na yale aliyoyaandika kwa upande wa elimu, mfumo na mwelekeo katika taaluma ya Hadiyth. Hii ni faida kubwa sana kwa Waislam. Himdi ni za Allaah. Ama kwa upande wa uhakiki wake wa kitaaluma katika fani ya Hadiyth, basi hayo hayasemeki. 

 

 

 

 

 

Mwanachuoni Mfasiri Shaykh Muhammad Al-Amiyn Ash-Shanqiytwiy (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Al-Haddaah anasema:

 

“Hakika Mwanachuoni mkubwa Ash-Shanqiytwy anamtukuza Shaykh Al-Albaaniy utukuzo wa kushangaza. Anapomuona anapita nailhali yeye yuko katika darsa yake katika Msikiti wa Madiynah, kasha husimamisha darsa lake, husimama na kumsalimia kwa ajili ya kumuheshimu”.

 

 

 

 

 

Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-’Abaadiy (Allaah Amhifadhi)

 

 

 

Bila shaka Shaykh Al-Albaaniy, alikuwa ni katika Ma’ulamaa wa kipekee walioumaliza umri wao katika kuitumikia Sunnah, kuitungia vitabu, kulingania kwa Allaah Mtukufu, kuinusuru ‘Aqiydah ya kisalafiya, kuipiga vita bid'ah, na kutetea Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Yeye ni katika Ma’ulamaa wazuri wenye sifa za kipekee. Sifa zake zimeshuhudiwa na watu maalumu na wa kawaida. Hakuna shaka kwamba kumpoteza Mwanachuoni kama huyu, ni katika misiba mikubwa inayowapata Waislamu. Allaah Amlipe kheri nyingi kutokana na juhudi zake kubwa na Amweke katika Pepo Yake pana.

 

 

 

 

 

Mufti Wa Zamani Wa Saudia Mwanachuoni Shaykh Muhammad Bin Ibraahiym Aal Shaykh (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Amesema kuhusu Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu): “Yeye ni mwana Sunnah, mpiganiaji haki, na mwenye kupambana na watu wasiofuata haki”.

 

 

 

 

 

Mwanachuoni Shaykh Muqbil Al-Waadi'iy (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Hakika katika taaluma ya Hadiyth, hakuna mtu kama Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Na Allaah Amenufaisha kwa elimu yake na vitabu vyake mara nyingi zaidi kuliko yale wanayoyafanya wale wenye hamasa na Uislam pasi na elimu ya kutosha, na wasio na msimamo. Ninaloliamini na ambalo ni deni kwangu mbele ya Allaah ni kuwa, Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni katika waipigao msasa Dini na wanasadikishwa na neno la Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

((Allaah Hutuma kwa Ummah huu mwanzoni mwa kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya Dini Yake)).[11]

 

 

 

 

 

Mwanachuoni Wa Hadiyth India, Shaykh ‘Abdus-Swamad Sharafud-Diyn (Allaah Amrehemu)

 

 

 

Katika moja ya barua walizokuwa wakiandikiana na Shaykh Al-Albaaniy katika masuala ya kitafiti ya Hadiyth, alikiri kuwa Shaykh Al-Albaaniy alikuwa Mwanachuoni mkubwa wa Hadiyth.

 

 

 

 

 

Waziri Wa Masuala Ya Kiislamu, Al-Awqaaf, Ulinganio Na Uongozi Shaykh Swaalih Bin ‘Abdil-‘Aziyz Bin Muhammad Aali Shaykh

 

 

 

Alisema: “Shukrani ni za Allaah kwa hukumu Zake na uwezo Wake ((Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea)).[12] Hakuna shaka kwamba kumpoteza Mwanachuoni Mkubwa Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni msiba. Yeye ni katika Wanachuoni wakubwa wa Ummah na mabingwa wa Hadiyth. Kwa Ma’ulamaa hao (Shaykh Al-Albaaniy), Allaah Mtukufu Ameilinda Dini hii na Akaieneza Sunnah kupitia kwao…”

 

 

 

 

 

 

 

Kipindi Cha Mwisho Cha Maisha Yake Na Kifo Chake

 

 

 

Shaykh (Allaah Amrehemu) hakutulia kutafuta elimu hadi umri wa miaka 86, akisoma, akifundisha, akielimisha, akiandika vitabu, akiandika barua kwa Wanachuoni wenzake kuwapongeza, kuwanasihi, kuwakosoa makosa ya vitabuni mwao au fatwa zao. Hadi umri huo hakuwa akiacha kutafiti masuala ya Hadiyth, akipangua sahihi na dhaifu na za kutungwa, aliweza kugawa vitabu vingi vikubwa vya Hadiyth kama vya Maimaam Abu, Dawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na wengineo, akaweza kuvigawa Sahihi zake na Dhaifu zake na kuwasaidia kuwarahisishia wenye elimu na wanafunzi katika uandishi na tafiti zao.

 

 

 

Shaykh anakumbukwa sana kwa kazi hiyo iliyosaidia Ummah leo hii, na kuuamsha kujua Hadiyth sahihi na dhaifu na pia kuwafanya wengi wawe karibu na kuifuatilizia elimu ya Hadiyth na sayansi yake.  Aliyafanya yote hayo – kwa sababu moyo wake ulikuwa umefungamana nayo hayo kwa mapenzi ya juu – na hakuacha hadi taqriban miezi miwili ya mwisho ya maisha yake, alipokuwa dhaifu akiugua kitandani. Pamoja na magonjwa mazito yaliyomdhoofisha sana na kutotoka kitandani, hakuacha kusoma wala hakupoteza kumbukumbu zake, akiwa anamjua kila aliyekwenda kumtazama, akimuita kila mmoja kwa jina lake! Hadi Allaah (سبحانه وتعالى) Alipoirejesha roho yake na akamfisha katika nyakati za mwisho za Alasiri, siku ya Jumamosi, tarehe 22 katika mwezi wa Jumaadah Al-Aakhirah, mwaka 1420 H sawa na 10-02-1999 M huko ‘Ammaan, Jordan.

 

Wanachuoni, watafuta elimu, wanafunzi, na watu wa kawaida wote waliathirika sana na kifo cha Shaykh. Taarifa za kifo chake zilipowafikia Waislam, majonzi yalienea pote na wengi kuhisi kuwa ile elimu na yule ‘Mujaddid’ (Mkarabati wa Dini) wa zama hayupo nao tena. Mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa huzuni, kwa kutanguliwa na kifo cha Mwanachuoni mkubwa wa zama hizo hizo ambaye alikuwa Mufti wa Saudia wa wakati huo, Shaykh Al-‘Alaamah ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdullaah bin Baaz, na baada yao kufuatiwa na kifo cha Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn, Mashaykh wengine wakubwa waliofariki katika mwaka huo ni, Shaykh Swaalih bin 'Aliy Ghaswuun, Shaykh 'Aliy Twantwawiy, Dkt. Mustwafaa Az-Zarqaa, Shaykh Mana'a Al-Qahtwaan na Shaykh 'Atwiyah bin Muhammad Saalim (Allaah Awarehemu wote hao na Awaweke katika pepo Yake Tukufu).

 

 

 

Abu ‘Abdillaah (1432 H – 2011 M)

 

 

 

 

 

 

[1] Ni fani ya Hadiyth inayohusiana na uaminifu wa wasimulizi wa Hadiyth na inakusanya habari zao zinazothibitisha uaminifu au udhaifu wa hao wasimulizi.

[2] Sayansi ya Hadiyth

[3] Hayaatul Al-Albaaniy, Muhammad Ash-Shaybaaniy. Al-Albaaniy mwenyewe anayaeleza hayo pia kwenye vitabu vyake Mukhtaswar Al-’Uluww’ na Tahdhiyrus-Saajid.

[4] Kitabu hiki kimeshatafsiriwa na mwandishi kwa lugha ya Kiswahili na kinapatikana maeneo mbalimbali kwa jina “Sifa Ya Swalah Ya Mtume ”.

[5] Kitabu hiki kilishatafsiriwa na mwandishi wa Historia hii ya Shaykh na kinapatikana kwa jina “Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotwaharika.” Chapa za mwanzo kimetawanywa bure na shukurani zote ni Zake Allaah.

[6] Kitabu hiki kimeshatafsiriwa na mwandishi kwa jina “Sifa Ya Swalah Ya Mtume” na chapa za mwanzo zimetawanywa bure na himidi zote Anastahiki Allaah.

[7] Shaykh Husayn Al-’Awaaishah, Swafahaat Baydhwaa Min Hayaati Shaykhina Al-Albaaniy, uk. 40.

[8] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-’Aswr, uk.78.

[9] Abu Hudhayfah: 20 Points Regarding Shaykh al-Albaanee

[10] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-’Iraaqiy na wengineo.

[11] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-’Iraaqiy na wengineo.

[12] Al-Baqarah: 156.

 

 

Share