003-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Utangulizi Wa Kitabu

 

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

 

UTANGULIZI WA KITABU

 

 

Sifa njema zote ni za Allaah Aliyefanya Swalah kuwa ni fardhi kwa waja Wake na kuwaamrisha kuitekeleza ipasavyo; Aliyeambatanisha kufaulu na furaha kutokana na unyenyekevu katika Swalah; Aliyefanya kuwa ni kigezo cha Iymaan na kufr; na aliyeifanya ni kizuizi cha mambo machafu na vitendo viovu.

 

Swalah na Salaam zimshukie Mtume Muhammad ambaye Amefunuliwa na maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ 

((Nasi Tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri))

 Na ambaye ametekeleza kikamilifu kazi hii. Swalah ilikuwa ni jambo muhimu kabisa aliyowaeleza watu kwa kauli na vitendo, hata aliwahi kuswali mara moja katika minbar akisimama, akirukuu na kusujudu, kisha akasema: ((Nimefanya hivi ili mnifuate na mjifunze Swalah yangu)). Ametuwajibisha tumfuate anavyoswali kwa kusema: ((Swalini kama mlivyoniona nikiswali)). Amebashiria pia kuwa atakayeswali kama anavyoswali, atakuwa katika ahadi ya Allaah kwamba Atamuingiza katika Pepo, akisema: ((Swalah tano ambazo Allaah (عزوجل) Amezifaradhisha. Atakayefanya wudhuu wake vizuri, akaziswali kwa wakati wake, na kutimiza rukuu zake, sujudu zake na unyenyekevu, ana dhamana kutoka kwa Allaah kwamba Atamsamehe, lakini asiyetekeleza hana dhamana kutoka kwa Allaah, Akipenda Atamsamehe au Akipenda Atamuadhibu))

 

Swalah na amani pia ziwafikie jamaa zake na Maswahaba zake Waswalihina waliotuletea ‘Ibaadah yake (صلى الله عليه وآله وسلم), na Swalah, kauli na vitendo vyake  na wakavifanya hivyo kuwa ni madhehebu na mfano bora kwao wa kufuata; na wale watakaofuata nyayo zao hadi siku ya Qiyaama.  

 

Nilipomaliza kusoma kitabu cha Swalah katika At-Targhiyb wat-Tarhiyb cha Al-Haafidhw Al-Mundhiry (رحمه الله) na kuwafundisha ndugu zetu miaka minne iliyopita, ilidhihirika kwetu umuhimu wa nafasi ya Swalah katika Uislamu; na thawabu, neema na fadhila zinazowasubiri watakaoitekeleza na kuiswali sawa sawa; na kwamba yote inatofautiana, kutegemea ukaribu wa Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Hii ndivyo ilivyoashiriwa katika usemi wake: ((Hakika mja huswali Swalah ambayo haandikiwi kitu ila sehemu ya kumi, au ya tisa, ya nane, ya saba, ya sita, ya tano, robo, thuluthi au nusu yake)). Hivyo nikawakumbusha ndugu kwamba haiwezekani kutekeleza Swalah ipasavyo au hata kuikaribia ila tutambue maelezo ya sifa ya Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), ikijumuisha namna ya kuiswali, mfumo wake, du'aa na adkhkaar zake, kisha tufanye jitihada kutumia elimu hiyo katika utekelezaji kwa makini, hapo ndipo tutaweza kuwa na tamaa kwamba Swalah zetu zitatuzuia na mambo machafu na vitendo viovu na ndipo tutaandikiwa thawabu na baraka zilizotajwa katika usimulizi mbali mbali.

 

Lakini, maelezo kwa urefu juu ya vipengele vyote hivi vya Swalah sio wepesi kutekelezwa na watu wengi siku hizi, hata Maulamaa wengi kwa sababu ya kujihusisha na kujiwekea mipaka ya madhehebu fulani. Lakini kwa yeyote mwenye kujali na kusaidia katika ukusanyanji na utafiti wa Sunnah zilizotakasika, atajua kwamba katika kila madhehebu kuna Sunnah ambazo hazipatikani katika madhehebu mengine; juu ya hivyo, katika kila dhehebu kuna usemi na vitendo ambavyo havipatikani dalili za usahihi wake kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).  Mengi hayo hupatikana katika usemi tu wa Maulamaa waliofuatia, wengi wao tunaona kwamba wanahusisha haya kwa Mtume. Ndio maana Maulamaa wa Hadiyth (Allaah Awalipe wote vyema) wametoa vitabu vya Takhriyj kuhusu vitabu maarufu vya Maulamaa waliofuatia, wakielezea daraja ya kila Hadiyth iliyotolewa humo: mfano kama ni 'Swahiyh' au 'Dhaifu', au 'Imezushwa'. Mifano ya vitabu hivi vya Takhriyj ni: 'Al-‘Inaayah fiy Ma'rifah Al-Ahaadiyth Al-Hidaayah na At-Twuruq wal-Wasaail fiy Takhriyj Ahaadiyth Khulaaswah Ad-Dalaail cha Shaykh 'Abdul-Qaadir bin Muhammad Al-Qurayshiy Al-Hanafiy; Naswb Ar-Raaayah li Ahaadiyth Al-Hidaayah cha Haafidwh Zayla'iy, na mukhtasari yake ya Ad-Diraayah cha Haafidhw Ibn Hajr Al-Asqalaaniy ambaye pia ameandika Talkhiys Al-Habiyr fiy Takhriyj Ahaadiyth Ar-Raafi'iy Al-Kabiyr;  kuna vingi vingenvyo, kuvitaja vyote vitazidisha urefu wa maelezo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

[1] Suratun-Nahl: 16: 44

[2] Al-Bukhaariy na Muslim – itafuatia baadaye kikamilifu

[3] Al-Bukhaariy na Ahmad

[4] Maalik, Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan. Hadiyth Swahiyh iliyobainishiwa kuwa Swahiyh na Maimamu wengi. Nimeitoa takhriyj yake katika Swahiyh Abi Daawuud (451, 1276)

[5]  Swahiyh – Imekusanywa na Ibn Al-Mubaarak katika Az-Zuhd (10/21/1-2), Abu Daawuud na An-Nasaaiy ikiwa na isnaad nzuri; Nimetoa takhriyj yake katika Swahiyh Abi Daawuud (761).

 

[6] Abul-Hasanaat Al-Laknawiy kasema katika An-Naafi' Al-Kabiyr Liman Yutwaali' Al-Jaami' As-Swaghiyr (Uk. 122.3) baada ya kuvikadiri vitabu vya Fiqh ya Hanafiy na kutaja vipi vya kutegemea na vipi visitegemewe: "Yote hayo tuliyosema kuhusu daraja zinazohusika za ukusanyaji huu unahusiana na yaliyomo katika mas-ala ya Fiqhi; lakini ama yaliyomo kuhusu Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), hazihusiki kwani vitabu vingi ambavo Mafuqahaa wanatagemea vimejaa uzushi wa Hadiyth, achilia mbali hukmu za Maulamaa. Ni dhahiri kwetu kutokana na uchambuzi mpana kwamba ingawa waandishi wake walikuwa ni mahodari lakini hawakuwa makini katika kunukuu usimulizi".

 

Si Maulamaa wa Hadiyth wala hawakutoa hizi Hadiyth kutoka kwa wakusanyaji wa Hadiyth".

Ash-Shawkaaniy pia alitaja Hadiyth hii katika Al-Fawaaid Al-Majmuu'ah Fil Ahaadiyth Al-Mawdhwuu'ah ikiwa na maneno yaliyofanana, kisha akasema (Uk. 54): "Hii imezushwa bila shaka – sijaipata hata katika mkusanyo wa Hadiyth za Uzushi! Bali imekuwa ni maarufu baina ya wanafunzi wa Fiqh katika mji wa San'aa katika karne yetu, na wengi wameanza kuitekeleza. Sijui nani aliyewazushia. Allaah Awahizi waongo".

 

[7] Maneno ya Imaam An-Nawawiy (رحمه الله) katika Al-Majmuu' Sharh Al-Muhadhdhab (1/60) yanaweza kujumuishwa kama ifuatavyo: "Maulamaa watafiti wa Hadiyth na wengineo wamesema kwamba ikiwa Hadiyth ni dhaifu, haitotajwa kuwa: 'Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)kasema/katenda/kaamrisha/kakataza….' Au ibara yoyote nyingine inayotaja uhakika, bali itasemwa: 'Imeripotiwa/imenukuliwa/imesimuliwa kutoka kwa…' au ibara zingine zinazodokeza shaka. Wanasema kuwa ibara za uhakika huwa ni Swahiyh na Hadiyth Hasan na ibara zenye shaka huwa ni nyinginezo. Hii ni kwa sababu ibara zinazotaja uhakika zina maana kwamba yanayofuatia ni Swahiyh, hivyo zinatumika kwa hali ya Usahihi pekee, au sivyo itakuwa ni kumzulia (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Jambo hili limepuuzwa na Mafuqahaa wengi wa zama zetu, bali Maulamaa wengi wa nidhamu yoyote, isipokuwa Muhaddithiyn wenye ujuzi. Huu ni uzembe wa kuchukiza kabisa, kwani mara nyingi hutaja Hadiyth Swahiyh: 'Imeripotiwa kutoka kwake kwamba…' Na kuhusu Hadiyth dhaifu: 'Amesema' na: 'Fulani na Fulani ameripoti...' Hivi sio sawa kabisa". 

 

Laknawiy akaendelea kusema: "Kutegemea Hadiyth hii ambayo inapatikana katika vitabu vya uradi na du’aa ni uzushi, nimeandika insha fupi ya kitaalamu na dalili inayoitwa 'Kuwakanusha Ndugu Kutokana Na Uzushi Wa Ijumaa Ya Mwisho Ya Ramadhaan'. Humo nimetoa nukta ambazo zitamulika akili na zitazibua masikio, hivyo isome, kwani ni ya thamani katika maudhui hii na ni ya ubora wa hali ya juu.

 

Marudio ya Hadiyth za uongo kama hizo katika vitabu vya Fiqhi vimeharibu uaminifu wa Hadiyth nyinginezo ambazo hazikunukuliwa kutoka katika vitabu vya Hadiyth vinvayotegemewa. Maneno ya 'Aliy Al-Qaariy yameashiria haya. Muislamu lazima apokee Hadiyth kutoka kwa watu ambao ni wataalamu katika fani hii, kama usemi wa zamani wa Kiarabu unavyosema: "Watu wa Makkah wanajua njia za milima yao vizuri" na "Mwenye kumiliki anajua vyema vilivyomo nyumbani mwake".

 

[8] Tanbihi ya Mchapishaji

Katika mlango huu, kuna kazi ya mwalimu wetu pia mwandishi wa Irwaa' Al-Ghaliyl Fiy Takhriyj Manaar As-Sabiyl katika Mijalada 9, na Ghaayah Al-Maraam fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal-Haraam, takhriyj ya Ahaadiyth zinazopatikana katika kitabu cha Dkt. Yuusuf Qaradhwaawiy 'Halali Na Haramu Katika Uislamu' (ambacho kina Hadiyth nyingi dhaifu).

 

Share