Anaweza Kuzungumza Na Kuonana Na Aliyemposa?

 

SWALI:

a/a swali langu ni vp muislamu mwanamume akiwa ataka kuposa mke, dua gani ataka aombe, je aruhusiwa kuzungumza nae ama kumwona? shukran

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya posa. Ama kuhusu posa hakuna du’aa maalumu inayofaa kuombwa na anayekwenda kuposa. Kitu ambacho anafaa afanye ni kuswali Swalah ya Istikhaarah ili kumuomba Allaah Aliyetukuka Amuelekeze katika lililo la kheri kama aendelee na posa yake au aivunje. Baada ya Swalah hiyo ya rakaa mbili kuna du’aa maalumu aliyotufundisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo utaipara kwenye kiungo hiki:

Swalah ya Istikhaarah

Mume Muislamu amepewa ruhusa kumuona mchumba wake kabla ya kwenda rasmi kumposa. Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuambia Mughiyrah bin Shu'bah (Radhiya Allaahu 'anhu): "Je, umemtazama?" Mughiyrah akasema: "Hapana". Akaambiwa: "Nenda kamtazame, kwani hilo linakupatia nguvu kuwa na mahaba na maafikiano baina yenu" (an-Nasaa'iy kwa Isnadi iliyo Sahihi).

 

Ama kuzungumza naye kabla ya Nikaah yenyewe itakuwa haifai kwani hiyo ni njia moja ya kuendelea katika uzinzi. Ikiwa posa imekubaliwa na upande wa mke, utakuwa na ruhusa kuzungumza naye na kumuona lakini si faragha bali anatakiwa mchumba wako awe na aliye maharimu wake. Kwa mfano, ukaenda nyumbani kwao akawa yupo peke yake, itabidi usikae naye hadi awe pamoja na babake, mamake au ndugu yake mkubwa ili kusiwe na faragha baina yenu wawili. Kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu ambao si maharimu kukaa pamoja faragha kwani wakifanya hivyo basi shetani ni watatu wao. Na Shetani atafanya hila zote kuwatumbukiza kwenye maasi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share