Usufi

 

Usufi 

 

Imefasiriwa na Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Usufi: Asili Yake

 

 

Neno Sufi inawezekana limetoholewa kutoka neno la Kiarabu “suuf”, lenye maana ya manyoya (sufi). Hii ni kwasababu ya tabia za Sufi kuvaa makoti ya sufi, mtindo ambao wameuanzisha na kupelekea sheria za Kisufi. Imani za awali za Masufi zilikuwa na imani kwamba uvaaji wa makoti ni kujifananisha na ‘Iysah bin Maryam (Yesu). Akijibu hili, Ibn Taymiyyah amesema: “Kuna watu ambao wamechagua na kupendelea kuvaa nguo za manyoya, wakidai kwamba wanataka kufanana na al-Masiyhah bin Maryam. Lakini mtindo wa Nabiy kwetu sisi ni bora zaidi, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akivaa pamba na aina nyenginezo za nguo.” [Al-Fataawa 11/7].

 

 

Usufi unajulikana kama “Mafundisho yasiyoelezeka ya Kiislamu”, ambayo Waislamu wanatafuta mapenzi ya Muumba na elimu kupitia uzoefu binafsi wa Muabudiwa [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Mafundisho hayo yanatafsiriwa kama ni uzoefu usioeleweka wa kuwa pamoja na ushirika wa moja kwa moja kwenye uhalisi wa asili, na imani kwamba elimu ya moja kwa moja ya Muabudiwa, ukweli wa kiroho, au uhalisi wa asili unaweza kupatikana kupitia kwa uzoefu wa nafsi (kama vile unaingia kiurahisi - mara moja tu au kwa uoni tu) [Kamusi ya Merriam-Webster’s Collegiate].

 

 

Misamiati yote ya Sufi, Usufi na imani ya Kisufi hayana msingi ndani ya vyanzo vya Kiislamu vya Qur-aan na Sunnah, ukweli ambao hata wao wameukubali. Isipokuwa, Usufi asili yake ni mkusanyiko wa vitu vingi vilivyochopolewa kutoka kwenye dini nyingine chungu nzima ambazo Masufi wameingiliana nazo.

 

 

Masufi walisifika katika kipindi cha awali cha ukuaji wa Usufi kwa kujinasibisha kwao mahsusi na dhikr (kumkumbuka Allaah) na kujiweka faragha, na pia (huo ulikuwa ni) mwanzo wa matendo ya uzushi ili ‘kutia uzito matendo ya kidini’. Hata pia mwanzoni wa ukuaji wa Usufi, (na) kabla ya kujihusisha na silka za uzushi na sheria za kutengeneza, Wanachuoni walikanya mkusanyiko wa matendo ya Kisufi wenye msimamo mkali.

 

 

Imaam ash-Shaafi’iy alikuwa na maoni kwamba: “Kama mtu anafuata Usufi (Tasawwafa) mwanzo wa siku, hafikii adhuhuri ila ni mpumbavu.”

 

 

Imaam Maalik na Imaam Ahmad bin Hanbal pia walikuwa na mawazo yaliyofanana na hayo katika mwendo huu mpya uliochimbuka kutoka Basrah, Iraq.

 

 

Ingawa ilianzia kama ni hatua ya kukithirisha ‘ibaadah, lakini vitendo hivyo vilinyanyukia kupelekea kwenye uharibifu, kwani msingi wao haukutokana na dhana sahihi za dini, isipokuwa zilitokana na kuvuka mpaka wa hisia za mwanaadamu. Usufi kama ambavyo ni mwenendo wa kujikusanya, uliibuka miongoni mwa Waislamu waliokuwa Waswalihina, wenye taqwa kama ni upinzani dhidi ya kipindi kilichotapakaa cha Umayyad (661-750 Miylaadiyyah) [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Masufi walijisifu kufuata aina ya maisha yaliyochafuka ambayo yalikuwepo wakati wa karne ya tano na sita Hijriyyah na kuwalingania watu kufuata njia yao, wakidai kwamba matokeo ya tendo hili lililochafuka ni kuendana na muongozo wa amri za Mashaykh wao. Dar al-Hikmah ilianzishwa wakati wa utawala wa Khaliyfah Ma’muun, ambapo aliwaita Wanachuoni wa Roma na Ugiriki kukutana na Waislamu na ‘kujadili’ mnasaba wa nafasi zao. Hili liliweka msingi mzuri wa kuleana katika kuchanganya baina ya Uislamu na elimu ya sifa na tabia za Kipagani, (pia) kuzalisha Usufi unaofanana na fikra za Ibnu ‘Arabiy.

 

 

Bakuli Lililochanganywa

 

Kutokana na kufariki Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) na warithi wao, hapo mlango ukawa wazi kwa kuziharibu Kanuni za Kiislamu. Maadui wa Uislamu walikuwa tayari wamekwishapenya sana ndani ya vyeo vya Waislamu na kusababisha mara moja fitnah kupitia kwao kwa kueneza hadiyth za uongo na hapo hapo kuanzisha madhehebu mapya kama vile Khawaarij na Mu’tazilah.

 

 

Ni kipindi hichi ambapo Usufi ulipata msingi wa malezi yake, ulipata usaidizi kutoka kwa Watawala wenye nasaba ya Kifalme, ambao walikwenda kinyume na Uislamu hadi kufikia kwamba uchawi ulikuwa ukitumika kama ni starehe ndani ya mahkama zao, ingawa uchawi unatambulika kama ni kufr ndani ya Uislamu [Misingi ya Tawhiyd The Fundamentals of Tawhiyd, Abuu Amiynah].

 

 

Wakati wa kipindi hichi, Usufi ulipata ladha yake ya Kishia, hakika mizizi ya Usufi huu huu huko nyuma ulitokana na asili ya Shi’a (angalia baadaye). Dhana ya Kisufi na fikra ilizagaa, mfano mnamo kipindi cha Muhyiddin bin ‘Arabi, Jalaal ad-Diyn Ruumi, na Ghazaali.

 

 

Mnamo karne ya tatu ya Kiislamu, Masufi walifasiri kazi za Kigiriki kwenda Kiarabu, tafsiri ambazo zilipelekea kuacha alama isiofutika katika nyanja nyingi za Kisufi, zilizosababishia kuamini kwenye imani za Kigiriki kwamba ulimwengu wote ni Muabudiwa au kwamba kuna waabudiwa wengi iliyopelekea kukamilisha sehemu ya dhana yake ya Kisufi. Matendo ya Kipagani kama vile kuabudia watu Watakatifu, matumizi ya uchawi na kushikilia kisasi dhidi ya Mashaykh wao viliwatoa kwenye imani barabara ya vitendo vya Kiislamu na vilikuwa na mfanano mdogo kwa Uislamu uliochwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa kuchunguza dhana za kuzua za Ukristu, Uhindu, Utaustu na dini nyengine, inakuja wazi namna ambavyo Usufi ulivyo karibu na dini hizi kuliko Uislamu. Taoisti (au Daoisti) unahusiana na aina tofauti za falsafa za Kichina na dini za kimila na dhana. Mila hizi zimeiathiri Asia ya Mashariki kwa zaidi ya miaka alfu mbili na nyengine zimesambaa kimataifa.

 

 

Ukweli ni kwamba, Usufi hauna sifa chini ya “Uislamu” kwa aina yoyote itakayopangiwa, isipokuwa chini ya “Uzushi usioelezeka”.

 

 

Sharda anabainisha mifanano hii isiohitajika kwa kueleza kwamba: “Baada ya kuanguka kwa nguvu ya Waislamu wenye imani barabara katikati ya India kwa kipindi cha karne, kutokana na uvamizi wa Taimuur, Masufi walikuja kuwa huru na kutotawaliwa (tena) na Waislamu wenye imani barabara.

 

 

Hali hii, iliwapelekea kuwafanya watakatifu wa Kihindi kuwa wenzao ambao waliwaathiri kwa namna iliyo ya ajabu. Masufi walitumia Umoja (Monism) na uzushi wa uke kutoka mafundisho ya matendo ya Vaishnava Vedantiki na Bakti na Yojiki.

 

 

Kwa mujibu wa dhana ya Usufi ni kwamba; hakuna tofauti baina ya Allaah na uumbaji Wake. Vyote hivyo ni vitu vimoja, na ndipo inapopatikana hiyo kanuni ya Umoja, kuviabudia vyote hivyo ni sawa tu kwao. Kuielewa dhana ya Umoja; tofautisha na Uwili kwa kuwepo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) upande mmoja Peke Yake na uumbaji wake kwa upande wa pili. Kwa wakati huo, umaarufu wa imani za Vedantiki kwamba ulimwengu wote ni Muabudiwa au kwamba kuna waabudiuwa wengi ulistawi vyema ndani ya Masufi [S. R. Sharda, Fikra za Kisufi Sufi Thought].

 

 

Tofauti zifuatazo zinafafanua mifanano isiyo linganifu ambayo Usufi unafuata pamoja na dini nyengine:

 

 

Fikra Ya Usahihi Wa Dini Zote

 

 

 Dhana ya Usufi ya kukubalika kwa dini zote mbele ya Allaah inatokana na imani za kuzua za dini nyingine, na si Uislamu, kwani Allaah Anasema:

 

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ ﴿١٩﴾

19. Hakika Dini mbele ya Allaah ni Uislamu. [Aal-’Imraan: 19]

 

 

Chukulia kwa mfano Mabudhi: “Hakuna Budhi anayeelewa (haswa) mafundisho ya Budha mwenye fikra kwamba dini nyengine ni za makosa…. Dini zote zinatambuwa kwamba hali yake mwanaadamu hakuridhishi kuwepo kwake. Zote zinafundisha maadili ya upendo, huruma, subira, ukarimu na uwajibikaji kwa jamii na zote zinakubali kuwepo kwa namna fulani ya Mkamilifu.”

 

 

Masufi pia wanaamini hivyo hivyo: “Allaah Hatofautishi baina ya asiyeamini na faasiq (mtendaji maovu) au baina ya anayeamini na Muislamu. Ukweli (hao) wote Kwake wapo sawa… Allaah Hatofautishi baina ya kaafir na mnafiki au baina ya mtakatifu na Nabiy” [Twariyqah ya Naqshbandi The Naqshbandi Way, uk. 12, 16].

 

 

Ndani ya Al-Fusuus, Ibnu ‘Arabiy hakuacha shaka kwa mnasaba wa kujitia hatiani kwenye umoja wa dini zote:

 

 

“Jihadhari na kujiwekea mipaka katika dini maalum na kutoamini vitu vyengine vyote, kwani mambo mazuri yaliyo makubwa yatakosekana na wewe, hakika utakosa kufikia kwa elimu ya mambo kwa mfumo unaofuata. Isipokuwa kuwa tayari kukubali mifumo yote ya imani. Hii ni kwa sababu Allaah ni Aliye Juu na Mkubwa kuliko uwezo wa mtu kuweza kuamini kufikia kuacha dini nyingine. Isipokuwa zote ni sahihi, na kila mtu ambaye yupo (njia) sahihi anapata malipo, na kila mtu anayelipwa ameneemeka, na kila anayeneemeka ni mtu ambaye Yeye Amemridhia” [Ibnu ‘Arabiy, Al-Fusuus, uk. 191].

 

 

 

Ushirika Pamoja Na Muumba

 

 Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni tofauti kabisa na viumbe Vyake. Hafanani na viumbe Vyake wala Haingiliani nayo (dhana hiyo). Hata hivyo, Masufi pamoja na dhana yao iliyokwenda mrongo ya Wahdatul-Wujuud, wanaamini kinyume na dhana hii (ya Ukamilifu wa Allaah Aliye tofauti kabisa na uumbaji wake).

 

 

Ibnu ‘Arabiy, Mwanachuoni wa Kisufi ambaye kwake imetoka dhana ya Wahdat ul-Wujuud na inasifika kwao kisawa sawa, anadai kwamba kwa kuwa Sifa za Allaah zimebainishwa ndani ya Uumbaji Wake, kuabudia Uumbaji Wake ni sawa na kumuabudia Yeye: “Hivyo mtu mwenye akili timamu ni yule anayeona kila kitu ambacho kinaabudiwa ni sahihi, kwani hicho kinabainisha ukweli uliokuwemo humo. Hivyo wanaiita Vyenye kuabudiwa, pamoja na jina lake maalum, ikiwa ni jabali, au ni mti, au ni mnyama, au ni mtu, au ni nyota, au ni Malaika” [Haadhihi Hiya As-Suufiyah, uk. 38].

 

 

Hivi ndivyo Masufi walivyoenda mbali katika kufru kwa sababu ya kushabihiana kwao na falsafa za Ugiriki na Mashariki, badala ya Qur-aan na Sunnah. Kwao wao Muabudiwa si Allaah Pekee, Ambaye hakuna chengine chochote kinachoshiriki Utawala Wake, isipokuwa kwamba kila tunachokiona kutuzunguka sisi, na hadi kufikia sisi wenyewe (basi hivyo vyote vinafaa kushirikishwa na Muabudiwa)!

 

Utukufu ni wa Allaah, Aliyeeleza:

  ۚ  لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

11. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

 

Tukiangalia wapi Masufi walipopata mafundisho yao, tunaona kwamba imani hizo hizo zilizojazana: “Unapoishi kwenye nyumba ya hekima, hutoona tena kizuizi baina ya “mimi” na “wewe”, “hichi” na “kile”, “ndani” na “nje”; utakuja mwishowe, katika nyumba yako ya kweli, hali ya sivo kuwa viwili non-duality” [Kitabu cha Tibetani cha Kuishi na Kufa The Tibetan Book of Living and Dying, uk. 77].

 

 

“Mwisho, utambuzi wa kuhakikisha kwamba imani imekomaa barabara inawezekana kwa usahihi kutamkwa kwa dai la ajabu, ‘Mimi ni Shiva’ (Muabudiwa wa Kihindu)” [Moyo Ulio Na Vitatu Wa Shija The Triadic Heart of Shiva, uk. 183-4]. “Pale ninapokuwa ndani ya giza sikumbuki chochote kuhusu mwanaadamu, au Muabudiwa-mwanaadamu… Ninaona vyote na sioni chochote. Kwani nilichokizungumzia kinaondoka na kinakaa pamoja nami, ninaona Muabudiwa-mwanaadamu. Na yeye mara nyengine ananiambia: ‘wewe ni mimi na mimi ni wewe” [Angela wa Foligno: Kazi Zilizokamilika, Angela of Foligno: Complete Works, uk. 181-2].

 

 

 

Kuiharibu Tawhiyd Katika Sifa Za Allaah

 

Masufi wanakataa moja kwa moja Sifa zote za Allaah, kama vile Uso Wake, Mikono Yake, Istiwaa n.k., wakitumia maana za kimafumbo kuelezea Sifa Zake. Ingawa Swahaaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) na Taabi’iyn (Rahimahum Allaahu) waliziamini bila ya kuzifananisha na uumbaji Wake, Masufi wanasadiki Sifa Zake kuwa ni sehemu ya uumbaji Wake.

 

 

Ibnu ‘Arabiy ameenda mbali zaidi hadi kusema kwamba amemuona Allaah wakati mmoja aliporukwa na akili na akiwa na hali kama ya usingizi mzito na kuona njozi. Alieleza kwamba Allaah huyo ni mtu mwenye nywele nyeupe rangi ya shaba na sura nyeupe aliyekaa katika kiti cha Ufalme! [Angalia Bezels of Wisdom, London 1980].

 

 

Masufi wengine wanaoshabihiana na elimu hii ya dini walifuata mtiririko huo huo wa nyayo za Ibnu ‘Arabiy: “Ndani ya maandiko ya Ibnu al-‘Arabiy na Ibn al-Farid, uzuri wa milele unanasibishwa kupitia uzuri wa kike; ndani ya nyimbo maarufu za uzushi za Waislamu huko Asia Indo-Muslim, hiyo roho ni mke mpenzi, Muabudiwa anayesubiri mume kwa muda mrefu. [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Uingizwaji wa muziki ndani ya ‘ibaadah za aina yoyote, hauna ruhusa kwa mujibu wa Wanachuoni walio wengi, na unabaki kuambatanishwa nayo kwa vitendo vyengine kama vile unywaji ulevi, uzinzi na mijumuiko parties. Hata hivyo, baada ya utekaji wa Dekan chini ya Malik Kafur (c. 1310), wanamuziki wengi wa Kihindu walichukuliwa na majeshi ya kifalme na kuwekwa sehemu za Kaskazini. Kukubali kwa kanuni za Kisufi, ambapo muziki ulikuwa ni njia inayokubalika kuridhisha Muabudiwa, iliwafanya watawala Waislamu na wenye heshima zao kupanua ufadhili wao katika sanaa hii [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Muziki ulitanda katika mizani iliyo kuu katika mahkama za Mughal, wafalme Akbari, Jahangiri na Shah Jahani, na Maderweshi Wakisufi walitumia muziki kama ni njia ya kurukwa na akili na kujihisi kana kwamba wapo ndani ya usingizi na kuona njozi. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amezungumza ndani ya hadiyth iliyo refu kuhusu matokeo ya vitendo viovu sana: 

 

 

“…watakapojitokeza waimbaji wanawake wakiwa na ala zenye nyuzi, ulevi kunywiwa, na wafuasi wa mwisho wa watu hawa wanawalaani wa mwanzo, angalia wakati huo kwa kutokea upepo mkali, mtetemeko wa ardhi, kumezwa na ardhi, badiliko la umbo, mvua kubwa mno, na alama zinazofuata moja baada ya nyengine kama vipande vya mkufu vinavyoanguka kimoja baada ya chengine pindi nyuzi zake zinapokatwa.” [At-Tirmidhiy]

 

 

Ulaghai wa Kisufi unawekwa wazi kwa kuangalia maisha ya viongozi wao wanaoheshimika, Mashaykh ambao wamewekewa imani kamili ndani ya elimu iliyorithiwa na kutii kila amri yao, na hapo hapo kufananisha mafunzo ya Kiislamu yaliyo barabara dhidi ya Kisufi.

 

 

 

Bayazid Tayfur Al-Bistami

 

Bayazid anatambulika kuwa ni “miongoni mwa nyota sita zinazongaa kwenye anga za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)” [Njia ya Naqshibandi], na kiunganishi ndani ya Mfuatano wa Dhahabu wa Twariyqah ya Naqshibandiy.

 

 

Lakini bado maisha yake yalivunda kwa Shirin za aina zote. Bayazid al-Bistami alikuwa ni wa mwanzo kueneza uhalisi wa Uharibifu (fana’), ambapo Uzushi unammeza hadi kufikia kutojielewa yeye mwenyewe au vitu vinavyomzunguka. Kila kinachokuwepo kinaonekana kuyeyuka, na anahisi kuwa huru kwa kila kizuizi ambacho kitasimama katika njia yake ya kumuangalia Yule Mwenye Kukumbuka Pekee.

 

 

Miongoni mwa hali zake kama hizi, Bayazid alipiga uyowe: “Shukrani ziwe juu Yangu, kwa rehma zangu Kubwa!” Bado dhana hii haina sehemu yoyote inayoweza kupatikana ndani ya Qur-aan, wala Sunnah, wala kwa tabia za Salaf us Swaalih. Imani ya Bistami ndani ya Ushirika wa dini zote ilikuja wazi alipoulizwa suala: “Uislamu unaangaliaje dini nyengine?” Jibu lake lilikuwa: “Zote ni vyombo na njia ya Kuwepo kwa Mola Mtukufu.” Jee huu ndio ulikuwa ujumbe wa Tawhiyd alioufanyia kazi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kufuatwa na Swahaabah (Radhwiya Allaahu ‘Anhum)?

 

 

Alisifia kwamba wenye kuamini ni sawa na wasio amini, ambao Allaah Amewaeleza kuwa ni (waovu) kuliko n’gombe (Suwrah ya Al-A’raaf, Aayah ya 179) na mbwa [Aayah hii imemfananisha na mnyama wala sio ngombe kama ilivyofasiriwa, mfananisho wa mbwa unapatikana Suwrah hii hii ya A’araaf, aayah ya 176]; ni wasio amini hao hao ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitamka kwamba ameamrishwa kupigana vita hadi wale kiapo kwamba hakuna kufanya Uungu isipokuwa Allaah.

 

 

Maisha yote ya Bayazid yalienea kwenye migongano ya imani. Katika umri wa ujana, alimuacha mama yake akimtamkia kwamba hawezi kumtumikia Allaah na mama yake kwa wakati mmoja [Kumbukumbu za Watakatifu, imetafsiriwa na Dr. Bankley Behari]. Alipokuwa akitembea mitaani, mara moja alipiga kelele: “Mimi ni Muabudiwa; kwanini hamuniabudii mimi?” Alitumia muda wake akiwa amekaa huku kichwa chake kikiwa baina ya magoti, akielezea mmoja wa wafuasi wake; kwamba alifanya hivyo kwa miaka thelathini.

 

 

Cha ajabu kuliko yote ulikuwa ni utiifu wake kwa mbwa ambaye alikutana naye mara moja. Mbwa huyo kwa uwazi alikuja kukasirika kwa tabia ya Bayazid kujaribu kumuepuka, kwa hilo mbwa huyo alimdhihirishia kwa kumbwekea. Hivyo, Bayazid alijitetea: “Ewe mbwa, wewe ni mwenye kutia nuru sana, ishi na mimi kwa muda fulani” [Kumbukumbu za Watakatifu, imetafsiriwa na Dr. Bankley Behari].

 

 

 

Ibnu ‘Arabiy

 

Wakati wa kipindi cha mwisho mwa karne ya 12 na mwanzo wa karne ya 13, chini ya ushawishi wa uzushi ulio mbaya, Ibnu ‘Arabiy alitoa mfumo ambao ulizalisha ufa mkubwa baina ya Shariy’ah na Usufi, ndani ya jamii nyingi, kama vile Uislamu wa India, ambao ulikuwa na nguvu kabla ya kurithi mambo ya uzushi ndani ya Uislamu, ufa huu ulikuja kuwa mkubwa zaidi [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Muhyiddin bin ‘Arabiy huwenda akawa anashikilia nafasi ya juu miongoni mwa Madhehebu ya Kisufi, na alikuwa kinara ndani ya mgawiko wa milele baina ya Uislamu na Usufi. Alidai kupokea amri za moja kwa moja kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, ikiwemo kitabu kilicho na Hadiyth mpya kabisa ambacho hakijapatapo kuonekana wala kusikika hapo kabla. Pindi alipopokea ‘wahyi’ huu, Ibnu ‘Arabiy alikuwa anatambulika kuhudhuria mikusanyiko ya usiku night parties ndani ya Seville. Wakati mmoja katika mikusanyiko hii, alisikia sauti (ya ulevi wake kutoka ndani?) ikimwita: “Ee Muhammad, hukuumbwa kwa sababu hii.”

 

 

Alikimbia akikhofia ziara (yake aliyoifanya) makaburini, ambapo alidai kukutana na kupokea muongozo kutoka kwa ‘Iysah, Muuswa na Muhammad (‘Alayhi swalaatu was-salaam ajma’iyn). Kutoka kwenye vitabu vyake, imetumika misemo mingi mno isiyo na hesabu yenye mnasaba na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hadi kufikia kwamba Waislamu wengi sana wanaiamini kuwa ni kweli. Ifuatayo ni nukuu kutoka kwa Ibnu ‘Arabiy:

“Mtu mwenye hekima daima hatojisalimisha kwa mfumo wowote au imani yoyote, kwasababu yeye ni mwenye hekima ndani yake mwenyewe” [Shairi lisilochapishwa kutoka kwa Ibnu ‘Arabiy ‘Diwan’, imetafsiriwa na Dr. Austin].

 

 

“Vyote vilivyobaki kwetu sisi kwa mwenendo (Hadiyth) ni maneno matupu. Ni juu yetu kutafuta yana maana gani” [Makala ya Stephen Hirtenstein kuhusu Muhyiddin Ibnu ‘Arabiy: Hazina ya Huruma]. (Hii inamaanisha mshikamano wake kwenye maana na tafsiri za Baatini (undani).

 

 

“Yeye (Ibnu Rushd) alimsifu Muabudiwa kwamba kwenye muda wake amemuona mtu mmoja (Ibnu ‘Arabiy) ambaye ameingia katika kimbilio la ujinga na (sasa) ametoka nje mfano wa hivi (elimu ya tafsiri za Baatini) – bila ya mafunzo, majadiliano, uchunguzi au kusoma” [Masufi wa Andalusia, imetafsiriwa na R. W. J. Austin, uk. 23].

 

 

 

Junayd

 

Junayd alikuwa ni kiongozi wanne katika mtiririko wa Safayid ambaye alijaribu kubadili mtiririko wa nguvu za kinafsi kwenda kwenye nguvu za kisiasa. Hata hivyo, kitu ambacho kinawezekana kuwa kilikuwa hakieleweki miongoni mwa wafuasi wake ni sera zake za kijeshi zilizo mbaya, zikikusanywa pamoja na wacha Muabudiwa wa Kishia na Kisufi [Encyclopaedia Britannica].

 

 

Mwanawe wa kiume, Haydar, mwenyewe alijianzishia utawala wa Safayid na Shia Wakiislamu Wakumi na Mbili ikawa chini ya mjukuu wake, Isma’il. Inasemekana alimpiga hadi kufa mtumishi wake wa kike, ambacho alidai kwamba alikuwa akiitawala miaka yake arobaini ya matendo yake ya kinafsi [Kumbukumbu za Watakatifu, uk. 108]. Huyu aitwaye ‘Mtakatifu’, anayetegemewa kuwa ni rafiki wa Allaah, alitoa matamshi yafuatayo: “Nimemuona mwizi ambaye amenyongwa katika mti wa kuhukumiwa kifo kwa mujibu wa sheria. Nilimuinamia… kwa kuwa alikuwa ni mkweli katika nyanja aliyokuwa akiifuata.” “Yeyote anayemukhofu Allaah daima hatabasamu.” “Usahaulifu mmoja wa Muumba unaharibu ‘ibaadah ya miaka alfu”. Mansuur al-Hallaaj Mansuur ni maarufu kwa madai yake “Ana-l-Haq” (Mimi Ndie Mkweli), kutokana nayo (kauli hiyo) aliuawa kwa sababu ya kurtadi. Lakini bado anaheshimika na Masufi ingawa aliacha sheria zote zinazohusu Tawhiyd.

 

 

Inasemekana ya kwamba aliishi na vazi kama joho pamoja na nge ndani yake kwa muda wa miaka ishirini mfululizo. Alisimama Makkah bila ya viatu wala kitu chochote kichwani kwa mwaka mmoja sehemu hiyo hiyo. Wakati wa maombi yake, alikuwa akisema: “Ee Rabb! Wewe ndie Muongozaji wa wale wanaopita kwenye Bonde la Bewilderment. Kama mimi ni shujaa, nizidishie mafundisho yangu yanayokwenda kinyume na dini.” Pia alisema: “Ninakataa dini yako (Uislamu) na kukaidi ni lazima juu yangu, ingawa hilo linafichikana kwa Waislamu” [Kumbukumbu za Watakatifu, uk. 108].

 

 

 

 

Abuu Yaziyd

 

Mara moja Abuu Yaziyd aliswali swalah ya Ijumaa sehemu 24,000 tofauti. Aliwaeleza wakuu wa dini sehemu moja: “Nilikuwa ninaswali ndani ya nyumba tofauti 12,000 za kuabudia hii leo.” Walimuuliza: “Namna gani?” Alijibu: “Kwa nguvu ya Mola Mtukufu. Kama hamuniamini, waleteni watu wanione.” Walikaa na kusubiri hadi wajumbe waliporejea walisema kwamba alionekana sehemu nyingi mno. Abuu Yaziyd baadaye alisema: “Nilikhofia kusema 24,000, hivyo nilisema 12,000.” Kwa uwazi Abuu Yaziyd aliongopea, ambapo ilikuwa ni rahisi kutotaja kitu chochote hapo mwanzo.

 

 

Je, hawa ndio wakweli ambao tunaambiwa walipokea elimu ya dini yetu? Je, hawa watu wanashabihiana na mafundisho ya Uislamu? Mtu ambaye ameacha utiifu kwa mama yake, kwa ajili ya kumtii mbwa? Je, tunahitajika kufuata watu ambao wamepokea wahyi kwa kuzuru makubiri baada ya kutumia muda wao kwenye kumbi za usiku za starehe? Au mtu anayemuua mtumwa wake kwa ‘kuharibu’ ‘ibaadah zake? Kwetu sisi, Uislamu unatambau tabasamu kuwa ni sadaka, sio kukufuru kutokana na Mapenzi ya Allaah. Uislamu unazuia unyongovu kwa mtu yeyote isipokuwa Allaah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba du’a akitafuta muongozo wa Allaah, sio kuomba mafundisho yanayokwenda kinyume na dini. Na Uislamu unatufundisha ukweli, sio uongo.

 

 

 

Ushahidi Dhidi Ya Mafundisho Yao: Imani Na Matendo Yao

 

 

Hadhi Ya Shaykh Na Walii

 

 

Shaykh au Walii anapewa heshima sawa kama ile ya Utakatifu wa Katoliki, au Dalai Lama mwenyewe. Utiifu kamili unalazimishwa kwa wafuasi wake, na masuala yoyote yanatambulika kuwa ni usaliti wa imani: “Mtafutaji ni lazima ajisalimishe kwa wasia wa Shaykh na kumtii kwenye amri zake zote na maoni, kwasababu Shaykh ana uzoefu zaidi na elimu zaidi kwenye haqqiqaat, kwenye taariqat na ndani ya Shari’ah.” Na “ni lazima akubaliane na maoni ya Shaykh wake kwa ukamilifu, kama vile mgonjwa anavyomkubali tabibu” [Njia ya Naqshibandi].

 

 

Juu ya hivyo, Waislamu wanaamini kwamba kitendo chochote cha ‘ibaadah ni lazima kithibitishwe kwa Qur-aan na Sunnah tu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١١١﴾

111. Na walisema: Hatoingia Jannah isipokuwa aliyekuwa Yahudi au Naswaara. [Al-Baqarah: 111]

 

 

Na  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “muumbwa asitiiwe juu ya Muumbaji.” Shaykh huyo anapewa hadhi ya Uungu ndani ya Usufi. Sifa ambazo ni za Allaah, halikadhalika zinanasibishwa kwa Mashaykh wao. Wanaomba msaada kutoka kwao, ikiwa wamekwisha fariki au wapo umbali wa kilomita alfu kumi. Wanaamini kwamba Mashaykh wao wanaelewa kila kitu ambacho wanafunzi wao wanafikiri, na kwamba wanazungumza na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kila kipindi maalum (kiuhalisi).

 

 

 

Uharibifu wa dhana za Dhikri, Hadiyth na Qur-aan

 

Kwa vile Qur-aan na Hadiyth Sahiyh haiwezekani kubadilishwa, Masufi wakageukia kwenye ta’wiil, mfumo wa kubadili maana iliyo wazi ya aayah au Hadiyth na kupata (maana) iliyofichika. Mfumo huu uliwapatia nafasi ya kutosha na iliyo nyepesi yenye kuthibitisha dhana yoyote wanayohitaji, kazi rahisi ni kueleza kwamba aayah au Hadiyth ilikuwa na maana ya ndani ambayo Shaykh mwenyewe anaweza kuitambuwa. Ndani ya kitabu chake Ibnu ‘Arabiy, cha ‘Bezels of Wisdom’, Ibnu ‘Arabiy anawasilisha nyanja fulani kwa namna anavyotafsiri aayah zenye mnasaba wa Suwrah Nuuh kwa mtindo ulio mbaya kabisa, kwa vile anashauri maana zilizo halisi sawasawa zikipingana na zile zinazokubaliwa na Wanachuoni Waislamu.

 

 

Anawatafsiri “wakosaji,” “makafiri,” na “watenda dhambi” ndani ya Suwrah Nuuh kama ni ‘watakatifu na Wenye elimu ya kinafsi’ kuzama na kuungua moto sio kwa adhabu ya Moto, bali kwa mwako wa moto na maji ya elimu ya Muabudiwa. Ibnu ‘Arabiy ametambua kuabudia masanamu kwa watu wa Nuuh kama ni uungu takatifu. Allaah Amekataza matendo yao Akisema:

 

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا ﴿٢٣﴾

23. Wakasema: Msiwaache waabudiwa wenu; na wala msimwache Waddaa, na wala Su’waa’a, na wala Yaghuwtha, na Ya’uwqa, na Nasraa. [Nuwh: 23]

 

 

Ambapo Ibnu ‘Arabiy aliitolea maoni: “Kama wao (watu wa Nuuh) wangeliiaacha, wangelikuwa wajinga kwenye Uhalisi… kwani ndani ya kila umbo la ‘ibaadah inarudia kwenye Uhalisi, ikiwa inatambulika au laa.”

 

 

Kitendo cha kufanya Dhikr kwa njia ya maduara na kuruka au kutikisika kama vile ni wenye wazimu, pia hakipatikani haswa. Dhikr ndani ya Kiarabu cha kweli ina maana: “Kumkumbuka Allaah.” Mfumo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambao Waislamu walikubali kuwa ni bora na ndio tu unaokubalika, Dhikr yao ilihusisha kusoma Qur-aan, kujadiliana masuala ya dini pamoja na Swahaaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum), na kufanya tasbiyh katika mikono yake.

 

 

Lakini tendo la kukaa ndani ya maduara na kwa sauti ya juu au ya chini kupiga kelele “Allaah, Allaah” haukupata kufanyiwa kazi na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Salaf, na Hadiyth zote zinazoeleza kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo (kama mfano alipodhaniwa kwenda kwenye chumba, akawaambia Swahaaba kunyanyua mikono yao na kupiga kelele “Laa Ilaaha Illa Allaah”) zinakubaliwa kwa pamoja kuwa zimefanyiwa ghushi. Ibni Taymiyyah ameeleza kwamba mwendo huu umefungua mlango kwa Shaytwaani, ambapo huyo Shaytwaani ataingia kwenye mkusanyiko (kwa kuwa wamejihusisha kwenye uzushi) na kuchukua mfumo wa sura ya mtu Mchaji Allaah.

 

 

Pia ameeleza kwamba imekatazwa kutamka “Allaah, Allaah” (kila mara), kwani haijapatapo kutangazwa kuwa ni mfumo wa Dhikri, na haiambatani na neno lenye kuikamilisha (kama vile Allaahu Akbar, Subhaanahu Allaah) [Shaykhul Islaam Ibni Taymiyyah, Majmuu’ al-Fatawaah]. Halikadhalika, riwaya za Khidhri na kukutana kwake pamoja na ‘Awliyaa’, watu 40 wa Abdaali ambao daima wapo katika Ardhi na wana uwezo wa kuwa sehemu yoyote kwa kupwesa jicho tu, hizo zinatokana na tungo za Uyahudi na Ukristo, sio tamaduni za Kiislamu.

 

 

Uzushi

 

Imaam Maalik ametanabahisha: “Kile ambacho hakikuwa dini wakati wa Rasuli na Swahaba zake, Allaah Awe Radhwi nao wote, hakihitajiki kuwa ni dini leo. Yule anayeanzisha uzushi (bid’ah) ndani ya dini ya Kiislamu na kuamini kuwa ni kitu kizuri, kwa kufanya hivyo, anadai kwamba Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameusaliti Ujumbe.” Masufi wanaonekana kupendelea kwenye kutumia kiwango kikubwa mno cha mali kutetea vitendo vya uzushi, wakidai kuwa hivyo ni “uzushi ulio mzuri.”

 

 

 

Vitendo hivi vinahusisha kusherehekea kifo cha Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (kitendo kilichotokana na utawala wa Fatamidi, ambao walianzisha uzushi huu ili kupata ridhaa ya watu wengi), kusoma Qur-aan juu ya maiti na kutafuta rehma kutokana nao, na ujenzi wa misikiti yenye gharama za kupita kiasi (ingawa Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hili. Anas anasimulia kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

“Saa haitokuja kupita hadi watu washindane na kila mmoja kwenye (kujenga) misikiti.” [Ahmad, Abuu Daawud, an-Nasai’i, Ibni Maajah].

 

 

 

Sababu Zinazowafanya Hadi Leo Kuendelea Kuwepo Kwao Wakiwa Ni Wenye Kusukumwa Kiurahisi Kwenye Mambo Ya Furaha Au Huzuni

 

 

Masufi wamefikia hadi ya kuwa ni sehemu ya maisha kwa Waislamu walio wengi mpaka Waislamu wanaona taabu kukubali kwamba njia ya Kisufi ni ya makosa, na kumtuhumu yeyote anayebainisha makosa ya Kisufi kama ni mwenye itikadi kali au mfuasi wa dhehebu ‘lililopotoka’. Usufi unawaita watu kwenye hisia kuliko akili na ushahidi wa Kiislamu. Kwa mfano, ushairi na muziki ilikuwa ni mifumo maarufu zaidi kipindi cha miaka mia moja iliyopita, ambapo “mawazo ya Kisufi yalilowesha mioyo ya watu wote walioelekea kwenye ushairi” [Encyclopaedia Britannica].

 

 

 Leo, Usufi unafuatwa na makundi ya watu ambao wapo tayari kuacha nyuma matatizo ya dunia hii, badala ya kujenga uwezo wa kuyabadilisha. Usufi unatoa mwanya mzuri wa kukimbia matatizo, wafuasi wake wanaweza kuwakimbia badala ya kuwafikiria Waislamu wengine wanaopata taabu, achilia mbali kuwasaidia.

 

 

Halikadhalika, kutokana na imani za Kipagani, Usufi unafanana mno na dini nyengine, na kama tulivyotanabahisha awali wapo wastahamilivu mno, kwamba mbadiliko wa Kisufi hauhitaji kubadili kwa ukamilifu wa maisha, kama Uislamu unavyohitaji. Hivyo, Mabudda, Masikhi, Mataoisti na wazushi Wakiyahudi na Wakristo wanaotafuta njia mbadala, wanaonelea kukubaliana na Usufi, ambayo huwenda ikaongeza ukubwa wa maisha yao yaliyopita, badala ya kuutia mzizi na kuanza upya. Taoisti (au Daoisti) unahusiana na aina tofauti za falsafa za Kichina na dini za kimila na dhana.

 

 

Mila hizi zimeiathiri Asia ya Mashariki kwa zaidi ya miaka alfu mbili na nyengine zimesambaa kimataifa. Kwa wepesi, Ibnul-Jawzii anasema ndani ya Talbiis Ibliis: “Usufi ni njia ambayo mwanzo wake ulikuwa ni kuepuka moja kwa moja kujishughulisha na maisha ya kidunia, baadaye waliojiambatanisha nayo walikuja kupotea kwa kukubali kuimba na kucheza. Hivyo, wale watu wa kawaida wenye kushughulishwa na Yawmul-Qiyaamah walikuja kupendezwa nazo kwa sababu ya kuepuka maisha ya kidunia ambazo walibainisha, na watafutaji wa dunia hii pia walivutiwa nazo kwa sababu ya uwepesi wa maisha na mazungumzo hafifu ambayo walionekana kuishi.”

 

 

Usufi unawapatia wafuasi wake maisha ambayo hayajali kabisa kupigana (jihaad), siasa, hamasa ya kutafuta elimu na kuisomesha, kazi ya da’wah, na inaruhusu mtu kujipenyeza kwenye mambo ya dunia kama vile muziki, uchawi, na vitendo vyengine vilivyozuiwa.

 

 

 

Kiongozi wa Twariyqah ya Naqshibandiy ndani ya Marekani, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema yafuatayo: “Unahitajika kuwa sehemu zote, kinafsi na kiroho. Masufi wanaweza kuwapatia watu furaha kwenye maisha yao ya kiroho. Hakika, Madonna anawapatia watu namna ya furaha kwenye maisha yao ya kinafsi… Huwezi kusema kuwa yeye ni mkosa. Masufi hawakatai na kupinga – wanakubali kila kitu. Ndio maana, pale watoto wangu wanapoangalia Madonna kwenye MTV, ninasema, “Achilia nami nije na mimi niangalie pia!”.

 

 

Inatoa nguvu kwa serikali, kwa kundi lolote (lililo nje ya Usufi) lionekane lina utata na ambalo linalofikia kupata nguvu iliyo kinyume na Serikali ya Kiislamu. Wakati wa utawala wa dikteta Mustafa Kemal, ambapo chini ya utawala wake maelfu ya Wanachuoni waliuawa na vitendo vya Kiislamu kupigwa marufuku. Idhini maalum ilipatiwa kwa serikali ya Kituruki mwaka 1954, ikitowa ruhusa kwa maderweshi wa Mawlawi kutoka Konya kuonesha michezo (dances) yao ya kimila.

 

 

Ukweli ni kwamba, siku hizi wametokea kuwa na mvuto wa kawaida, wakitumbuiza duniani kote pamoja na kundi lao la Mambo Yanavyoonekana ya Muziki wa Kuzua wa Taifa la Uturuki (Turkish Mystical Music State Ensemble) [Hivi karibuni walikuja kutumbuiza nchini Australia, wakitoza $30 kwa kila kichwa. Wale matajiri tu ndio waliokwenda kuangalia maonesho ya sinema hii ya dakika 90]. Shaykh wa Naqshindandi wa Marekani amemsalimia na kupokea sifa kutoka kwa Raisi wa Marekani Bw. Bill Clinton mwenyewe. Na kwanini asipate? Kwani ‘Uislamu’ anaouchora ni wa upole na mshikamano pamoja na Makafiri.

 

 

 

Kubadilishwa Ushahidi

 

Kwa vile Qur-aan na Hadiyth tayari zinapatikana, na haziwezi kubadilishwa, Masufi wamekimbilia kwenye ujanja tofauti unaotumiwa na Wazushi wengine:

 

 

Ta’wiil, au kubadili maana iliyo wazi ya aayah au Hadiyth kuifanya kuwa ni yenye siri ya ndani ambayo ni Shaykh tu anayekubalika ndie anaweza kuielezea! Pia wanaegemea kuipatia hadhira Hadiyth za uongo, kama ile inayosema kwamba Nabii Adam (‘Alayhi swalaatu was-salaam) aling’ang’ania sana kuomba (msamaha) kwa jina la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipofanya dhambi; riwaya za Khidhri; kuibuka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwenye kaburi lake ili mtu apate kuubusu mkono wake na mengineyo. Kwasababu ya kukosa elimu, makundi ya watu yaliyo mengi yamekamatana na elimu ya Hadiyth na ‘Aqiydah, wanaamini yale wanayoelezwa, na kuzielezea riwaya hizo kwa vizazi vyengine, zikiharibiwa zaidi humo njiani.

 

 

Njia nyengine iliyo bunifu ni kwa kusifu misemo iliyoharibiwa ikikubaliwa na Masufi kutokana na Wanachuoni waadilifu. Kwa mfano, Ibni Taymiyyah amesifiwa kwamba aliwahi kuwa ni Rasuli wa mfuatano wa Qadiri na alimilikiwa, na kuzungumza maneno makubwa kuhusu Bistami na sifa zake. Lakini bado Ibni Taymiyyah ametumia muda mkubwa wa maisha yake kupigana dhidi ya mafundisho ya Kisufi, amefungwa kwasababu yao, na waziwazi bila kuficha ameeleza “… Ibnu ‘Arabiy ambaye ameandika ‘Al-Fusuus’, na watu wengine wasengenyaji wasiosadiki kuwepo kwa Muabudiwa kama vile Ibni Sab’iin na mfano wake. Hata pia wameshuhudia kwamba wao wapo sawasawa wanaoabudu na wanaoabudiwa.”

 

 

 

Maafa kwa Ummah

 

Masufi wamewaharibu Waislamu kwenye mafundisho ya Qur-aan na Sunnah na kuwapeleka katika utumwa wa Shaykh. Hivyo, Waislamu wametengwa kutokana na mafundisho ya Uislamu, na wala hawahodhi kinga kutokana na uzushi na mitego ya madhehebu ya kikafiri. Mafundisho kama: “Yeye (mfuataji) asiangalie mwengine isipokuwa Shaykh wake” hayakufanya chochote kuiziba jamii. Isipokuwa, imefanya mpira kufingirika kwa vita baina ya Madh-hab tofauti, ambayo madhehebu hayo yamepelekea kupigana, kuachana kwa kila imani tofauti, na kuswali vituo tofauti ndani ya Makkah wenyewe.

 

 

Masufi wameacha alama mbaya katika uono wa Uislamu, wakiuchora kama ni ya amani na siasa safi [Kwa ufafanuzi zaidi, soma makala ambayo inapatikana ndani ya alhidaaya; Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Kuhusu Uislamu], na mtu yeyote anayekwenda kinyume ni laghai na anatambulika kuwa ni mwenye imani kali. Kwa kuegemea kwenye Hadiyth za uongo kama vile: “Jihaad kubwa ni Jihaad’un-nafs (yaani kupigana dhidi ya nafsi) na mifano ya hiyo, Waislamu wamefanywa kuamini kwamba kazi na koo (familia) ndio Jihaad kubwa zaidi, kuliko kuisimamisha dini ya Allaah Ardhini hata kwa kutumia panga.

 

 

Bila ya shaka, Masufi wamehamasisha kuchangia sana kuanguka kwa Utawala wa ‘Uthmaan Ottoman Empire. Mawazo yao waliyoyaeneza, ukosefu wa elimu ya Shari’ah, na kuwafadhili wasio amini, yaliwahakikishia kwamba hakuna mtu yeyote atakayepingana na mabadiliko ya haraka yaliyofanywa kwenye Sheria za ‘Uthmaan. Kufikia 1880, kipindi cha Tanzimaati kilikuwa na nguvu kamili, ambapo Shari’ah ilitupwa kwa kutumika Sheria za Uingereza (isipokuwa ndani ya mazingira maalum kama vile adhabu za hadd), juu ya hivyo, pingamizi chache zilisikika [Ulimwengu wa Kiislamu, New Jersey, 1991].

 

 

Wakati ambapo makundi ya watu yalishughulika kwenye ujenzi wa misikiti ya gharama iliyochupa mipaka na kuzunguka katika maduara (wakifanya dhikr), Utawala wa ‘Uthmaan uliangushwa na Masonsi na matokeo yake kuchanwa chanwa. Hatima ya Kisufi tokea ilipoibuka awali, ilikuwa ni kuangamiza na kuharibu, kwasababu ya kufru zake kinyume na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah. Walizidisha kidogo kidogo na walizua kidogo kidogo, lakini athari yake ilikuwa ni kubwa mno. Hivi sasa Usufi umeibuka kuwa ni jumuiya ya wenye kujiweza wakiengeza ‘ibaadah na Zuhdi zenye kupelekea katika Ukafiri na Uzushi.

 

 

Kusema kweli, Uislamu unatutosha, na ni Shaytwaan peke yake anayependelea kutugeuza mbali na dini yetu, kutufanya kuchupa mipaka hadi kuangukia kwenye mitego yake. Njia pekee muafaka ya kumuepuka Shaytwaani ni kukamatana kwa nguvu zote kile amabcho kimeachwa nyuma yetu na Nabiy wetu mpenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Qur-aan na Sunnah, kama inavyoeleweka na kuaminika na kufanyiwa kazi na watu bora waliopata kuishi: Salaf-us-Swaalih (Rahimahum Allaahu), Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) na wale waliofuata nyendo zao.

 

 

 

Share