Moto 'An-Naar'

 

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Baada ya kusoma kuhusu Pepo, leo tutazama upande wa pili ambao ni moto. Tutazame habari zake na balaa zake.

 

Katika Qur-aan na Hadiyth kumetajwa moto kuonesha mazingira mabaya watakayoshukiwa watu waovu, Waliompinga Allaah na kuendesha maisha yao ya hapa duniani kinyume na kanuni na taratibu alizoziweka Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

 

Maisha ya motoni ni kinyume na maisha ya Peponi ambayo picha yake tumeshaiona. Tunafahamishwa katika Qur-aan kuwa motoni kuna Daraja au Milango saba, na kila mlango iko sehemu iliyogawanywa.

 

“Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipoahidiwa wote. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. [Suratu-Al-Hijr:43-44].

 

Daraja hizi za moto zimepewa majina kama tusomavyo katika Qur-aan:

 

 

Jahannam:

 

Katika Aayah nyingi jina hili limetumiwa, Kama jina la ujumla la maisha ya Motoni. Kama katika baadhi ya Aayah hizi Allaah Aliyetukuka Anasema:

“Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu” [Al-Anbiyaa: 98].

“…kisha Tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam, wapige magoti (hapo)” [Maryam: 68].

 

 

Lahab: Moto wenye muwako mkubwa kabisa.

 

“Atauingia Moto wenye mwako”. [Suratul-Masad: 3].

 

 

Hutwamah: Moto wa kuvunja vunja-Moto uliowashwa kwa ukali.

 

“Hasha! Atavurumishwa katika Hutwamah”. [Suratul-Humazah: 4].

 

 

Sa’iyra: Moto mkali wa kuunguza.

 

“Basi wapo miongoni mwao waliyoyaamini, na wapo walioyakataa. Na Jahannam yatosha kuwa ni (Sa’iyra) moto wa kuwateketeza”.  [Suratun-Nisaa: 55].

 

 

Saqara: Moto unaobabua.

 

“Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar”. [Suratul-Mudaththir: 26].

 

 

Jahiym: Moto mkali.

 

Na Jahiym itadhihirishwa kwa wapotovu”. [Suratush-Shu’araa: 91].

 

Basi bila ya shaka mtaiona Jahiym”. [Suratut-Takaathur: 6].

 

 

Haawiyah: Moto uokwao kwa ukali.

 

Huyo maskani yake yatakuwa Moto wa Haawiyah”. [Suratul-Qaari’ah: 9].

 

 

Wakosaji wataingia katika aina hizi za Moto kulingana na makosa yao. Kwa ujumla aina yoyote ya moto ulioandaliwa kwa ajili ya makafiri hata ukiwa na daraja ya chini namna gani, Utakuwa ni mkali usio na mfano na usiovumilika hata kwa  muda mfupi sana kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anavyotufahamisha:

 

“Hakika hiyo (Jahannaam) ni kituo kibayana mahali (pabaya kabisa) pa kukaa (hata kwa muda mfupi.” [Suratul-Furqaan: 66]

 

Pia tuone anavyotufahamisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kiwango wa adhabu ya motoni.

 

Nuuman bin Bashiyr amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema; “Hakika atakayekuwa na adhabu nyepesi kabisa katika wakazi wa motoni ni yule atakayekuwa na viatu vya moto, Kwa moto huu, (wa miguu utachemsha ubongo wake kama maji yachemkavyo kwenye birika). Haitaonekana kuna kiwango cha chini kabisa cha adhabu.” (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

 

Kwa ujumla moto wa adhabu alioandaa Allaah (Subhaananu Wa Ta’ala) kwa watu waovu ni mkali sana.

 

Ndani ya mazingira ya motoni patakuwa na miti michungu, Na mti maarufu kwa uchungu ni “Zaqquum”. Tunapata maaelezo kamili ya mti wa “Zaqquum” ambao umeenea katikati ya Jahannam na watakaostahiki kuula ni katika Aayah zifuatazo:

 

“Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqquum?

 

Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa waliodhulumu.

 

Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Jahannam.

 

Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashetani.

 

Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.

 

Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.[Asw-Swaffaat: 62-67].

 

 

Pia katika mazingira ya motoni patakuwa na nyoka na n’ge wakubwa wenye sumu kali watakaowauma wakazi wa humo kama sehemu ya adhabu yao kama tunavyo fahamishwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

‘Abdullaah bin Haarith bin Jaazin amesimulia kuwa  Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa: “kuna nyoka huko motoni wakubwa kama ngamia, Mmoja wao akikuuma mara moja uchungu wake hubakia kwa miaka arubaini. Kuna nnge huko motoni wakubwa kama nyumba, Mmoja wao akimuuma mtu uchungu wake utabakia kwa muda wa miaka arubaini.” [Ahmad].

 

Kwa vyovyote itakavyokuwa maisha ya motoni yatakuwa magumu sana kwa wakazi wake. Chakula chao kitakuwa cha moto wa kuunguza kila kitu tumboni, Mavazi yao yatakuwa ya moto, Kinywaji chao cha moto kitakachochemsha matumbo yao kama maji yachemkavyo kwenye sufuria ya shaba. Picha halisi ya mazingira ya motoni, Maisha ya wakazi wake na sifa zinazowafanya wastahiki kuingia humo. Tutazame baadhi tu ya Aayah hapa:

 

“Nao husema (kwa maskhara): Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi.

 

Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi.

 

Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.

 

Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu.

 

Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.” [As-Sajdah: 12-14].

 

 

Na katika Suratun-Nabaa tunaona:

 

“Hakika Jahannamu inangojea!

 

Kwa walio asi ndio makaazi yao,

 

Wakae humo karne baada ya karne,

 

Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji,

 

Ila maji yamoto sana na usaha,

 

Ndio jaza muwafaka.

 

Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu.

 

Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu.

 

Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika.

 

Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu!” [An-Nabaa: 21-30].

 

 

Na katika Suratul-Fajr:

 

“Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

 

Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!

 

Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

 

Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.” [Suratul-Al-Fajr: 23-26].

 

Kama tunavyoona Aayah hizi kwa ujumla zinatilia mkazo wale watakaostahiki adhabu ya motoni ambao ni wanaadam na majini waovu walioendesha maisha yao hapa duniani kwa kibri kinyume na utaratibu uliowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Ndugu katika Iymaan, tujilinde na adhabu hiyo kali kabisa ya moto, adhabu isiyo na mfano na moto usioweza kulinganishwa na moto wa aina yoyote uliopo hapa duniani. Tujikinge sisi na familia zetu kwa kufanya ‘amali njema zitakazomridhisha Allaah (Subhanaahu wa Ta’ala) na tuzitekeleze kwa njia safi na sahihi kama tulivyoelekezwa kwazo na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Tunamuomba Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Atukinge na adhabu ya moto, sisi na vizazi vyetu na Waislam wote kwa ujumla, Aamiyn.

 

 

Share