Umuhimu wa 'Aqiydah

 

Chanzo: ‘Aqiydah (Mambo ya Iymaan) Kwanza ...Laiti Kama Wangalijua

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaarifu Mu’aadh bin Jabal, wakati alimpomtuma kwenda nchi ya Yemen, “Wewe unakwenda kwa watu Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitaab) Basi jambo la kwanza kuwalingania liwe kumuabudu Allaah. Kama wakilikubali hilo, ndio kisha uwataarifu kwamba Allaah amewajibishia juu yao sala tano wakati wa usiku na mchana.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hadiyth hii iko wazi kabisa. Na haihitaji maelezo mengi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katumia kanuni hii katika uilinganizi wake wa kuwaita watu ndani ya Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa katika mji wa Makkah kwa muda wa miaka kuminatatu akiwafunza watu iymaan na kuwaelimisha Maswahaba zake juu ya nukta hii na kusahihisha iymaan za watu. Huu ndio mfumo waliokuzwa nao Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Jundub bin ‘Abdillaah Al-Bajaliy akasema, “Tumejifunza iymaan na kisha tukajifunza Qur-aan nayo ikatuongezea iymaan yetu.”

 

'Abdullaah bin ‘Umar alisema, “Sisi tuliishi wakati ambapo mmoja wetu atafunzwa iymaan kwanza kabla ya kufunzwa Qur-aan na wakati Surah zikiteremka tulijifunza ni nini kilichoruhusiwa na nini kilichopigwa marufuku na kipi kilichokatazwa na kipi kilichoamriwa na upi unapaswa kuwa msimamo wetu juu yao. Lakini nimeona watu wengi waliofunzwa Qur-aan kabla ya iymaan. nao huisoma kutoka mwanzo wa Kitabu hadi mwisho wake pasi na wao kufahamu nini imeamrisha na nini imekataza na bila ya kuufahamu msimamo wao juu yake. Anakuwa kama mtu ambaye anayezitupa tende (yaani, hafaidiki na kuisoma kwake Qur-aan)."

 

Hiyo ndio njia ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyowaleya nayo Maswahaba wake: Iymaan kwanza kisha Qur-aan.

Hii ni sawa na kile Imaam Abu Haniyfah alichosema: “Elewa Dini kwanza (yaani Tawhiyd) kisha ndio uelewe sayansi yake (yaani Shari'ah).”

 

Iymaan lazima isahihishwe kwanza, kisha ndio yafuate mambo mengine ya Dini.

 

Na Imaam Ash-Shafi'iy akasema, “Yakuwa ni bora mja akutane na Allaah kwa kila aina ya dhambi isipokuwa shirki kuliko kukutana na Allaah hali ya kuwa amezusha jambo katika Dini.”

 

Neno Al-‘Aqiydah asili yake imetokana na neno ‘aqada. Katika lugha ya Kiarabu, panasemwa, “Aqada Al-Habl” kumaanisha wakati kamba imefungwa imara. Na, “’Aqada Al-Bay’” (Mkataba wa Mauzo)” au “Makubaliano ya bei” wakati mtu anapoidhinisha mkataba wa mauzo au makubaliano. Na Allaah Anasema katika Qur-aan,

 

“Na wale ambao mmefungamana nao ahadi (‘aqadat), basi wapeni sehemu yao.” [An-Nisaa: 33].

 

Na vilevile Allaah Anasema,

 

“Allaah Hatokuhisabuni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuhisabuni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mliyoifunga thabiti (‘aqadtum).[Al-Maaidah: 89].

 

“Na timizeni Ahadi ya Allaah mnapoahidi, na wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha." [An-Nahl: 91].

 

Mfano wa mtu kusema ‘Aqadtu juu ya jambo ni kumaanisha yakuwa moyo wake umekita juu ya hicho alichokidhamiria.

 

Kwa hiyo, Al-‘Aqiydah au Al-I’tiqaad kulingana na Wanachuoni wa Kiislamu ni: iymaan imara iliyokita ndani ya moyo wa mtu pasi na kutetereka au kuwa na shaka yoyote. Na inaoondosha dhana, shaka au wasiwasi.

 

Imaam Abu Haniyfah kaliita somo hili adhimu Al-Fiqh Al-Akbar (Ufahamu ulio Adhimu) na ndio ufahamu wa Dini. Aliita sayansi ya shari’ah; ufahamu wa sayansi.

Wanachuoni wengi wa Kiislamu hulitumia neno Tawhyid kwa mambo yote ambayo mtu lazima ayaamini. Hii ni kwa sababu kilicho muhimu zaidi katika mambo yote ni msingi wa Tawhyid uliomo ndani ya maneno, “Hakuna anayestahili kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah (Shahaadah).”

 

Tawhiyd, kulingana na wao, inaweza kugawanywa katika makundi mawili: Tawhiyd ya utambuzi na uthibitisho na Tawhiyd ya makusudio na matendo.

Tawhiyd ya utambuzi na uthibitisho ni Tawhiyd ya Upweke wa Muumbaji na Tawhiyd ya Majina Yake na Sifa (yaani Yeye ni Mpweke na Ndie Muumba na ni Mpweke katika Majina na Sifa Zake).

Tawhiyd ya makusudio na matendo ndio Tawhiyd ya Uuluwhiyyah yaani hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah (yaani, Yeye Pekee tu Ndiye Anayestahili kuabudiwa).

 

Wanatheolojia ‘Kalaamiyyuwn’ - na nini kitachokujuza wewe hao wanatheolojia ni wepi? – Wameliita somo hili adhimu “mzizi wa dini” na wakaiita shari’ah “matawi ya dini.” Hii ni istilahi yao. Sisi hatuafikiani nao katika jambo hili lakini hapa si pahala pake pa kulijadili. Wote wameipatia jina au kivumishi kulingana na mahitaji yao.

Lakini ni jina gani Qur-aan imelipa jambo hili?

Qur-aan imeliita jambo hili kwa jina la Iymaan. Allaah Anasema katika Qur-aan:

Na hivyo ndivyo Tulivyokufunulia (Wahyi) kwako roho katika Amri Yetu. Hukuwa unaelewa nini Kitabu, na wala (nini) Iymaan, lakini Tumeijaalia (kuwa) Nuru, Tunamhidi kwayo Tumtakaye kati ya waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kwenye Swiraatwim-Mustaqiym  (njia iliyonyooka).” [Ash-Shuwraa: 52]

 

Kwa ujumla moyo wa Muumin lazima uwe thaabit kuhusu “nguzo” hii ya iymaan. Lakini mtu hatoitwa Muumin tu kwa kujua na kuelewa nguzo hizi lakini ni lazima aridhiye na atekeleze kile kinachoelezewa, katika Hadiyth ya Jibriyl, kama ndio Uislamu. Iymaan, kwa namna hii, inajumuisha Uislamu.

 

Kama Iymaan ingekuwa inatosha kwa mtu kujua ukweli katika moyo wake tu, basi kuna tofauti gani baina yake na shaytwaan au Fir’awn (Kumbuka: Shaytwaan alikuwa mwenye elimu kubwa juu ya Mola wake lakini aliangamizwa kwa sababu ya kiburi chake na wivu. Na Fir’awn, ingawa yeye alidai Uungu, alijua kwamba Mungu wa kweli  ni Allaah na kwamba hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Yeye. Allaah Anasema:

 

“(Muwsaa) Akasema: “Kwa yakini umekwishajua kwamba hakuna Aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi kuwa ni dalili za kuonekana dhahiri.” [Al-Israa: 102]. - Ingawa walijua ukweli, hawakukubali kuielekeza ‘ibaadah yao kwa Allaah Pekee).

 

Katika Hadiyth ya Jibriyl, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alielezea nguzo za hii iymaan ambayo kila mwanaadamu lazima aamini, na alipoulizwa, “Ni nini Iymaan?”, Alisema, “Ni kumuamini Allaah na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Wake na Siku ya Mwisho na Kheri na Shari vyote vinapatikana kwa Qadari ya Allaah.”

 

Ni lazima kwa kila mtu kuzijua nguzo hizi na kujifunza ufahamu ulio sahihi na kuamini katika ufahamu wa wema wetu waliotangulia walivyofahamu na kuamini, kwa namna walivyofahamu wao kutoka kwa Maswahaba wa Mtume  (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wale wote waliowafuata katika njia hiyo. Hii inajumuisha pamoja na ma-Imaam wanne, na Sufyaan Ath-Thawriy, Sufyaan bin 'Uyaynah, ‘Abdullaah bin Al-Mubaraak na wengine sawa na wao, kama vile Muhammad bin Isma’iyl’ Al-Bukhaariy, Muslim bin Al-Hajjaaj, Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah na Al-Haafidhw Ibn Al-Qayyim. Na Wanachuoni wote walio sawa nao katika ufahamu ambao waliofuata mwenendo  ule ule katika kufahamu na kuziamini nguzo hizi.

 

Huu ni wajibu wa kwanza juu kiumbe mwenye dhima. Hakuna tofauti ya maoni juu ya suala hili miongoni mwa wasomi ambao maoni yao yanastahiki kufuatwa. Imaam Abu Haniyfah kasema: “Kuelewa iymaan ni bora kuliko ufahamu wa sayansi.” Alichokusudia katika usemi huu kuwa; Iymaan ni Tawhiyd na sayansi ni Shari’ah. Kwa hiyo katanguliza ufahamu wa Tawhiyd kabla ya mtu kufahamu Shari’ah.

 

Na Shaykh Al-Islaam Al-Haruwi Al-Answaariy (Aliyefariki 481 H) amesema katika mwanzo wa kitabu chake ‘I’tiqaad Ahl As-Sunnah’: “Wajibu wa kwanza juu mja ni maarifa juu ya Allaah. Hii inathibitishwa na Hadiyth ya Mu’aadh, wakati alipoambiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Wewe unakwenda kwa watu Watu wa Kitabu (Ahlul-Kitaab) Basi jambo la kwanza kuwalingania liwe kumuabudu Allaah. Kama wakilikubali hilo, ndio kisha uwataarifu kwamba Allaah amewajibishia juu yao sala tano wakati wa usiku na mchana.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Kutokana na  uadhimu wa nguzo hii ndio Maulamaa wakubwa wa Kiislamu wameitanguliza. Tafakari, kwa mfano, kile Imaam Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy alivyofanya katika kitabu chake Al-Jaami’ Asw-Swahiyh, ambayo ni kitabu sahihi zaidi baada ya Kitabu cha Allaah, Utaweza kuona kwamba kutokana na elimu yake ya kina na ufahamu wake wa Dini hii. Imaam huyu mkubwa alianza kitabu chake kwa “Mwanzo wa Ufunuo” na kisha ikifuatiwa na mlango juu ya iymaan, na kufuatiwa na mlango juu ya maarifa. Kama kwamba alikuwa akimaanisha (Allaah Amrehemu), kwa uhakika wajibu wa kwanza juu ya mwanaadamu ni iymaan na njia ya kuifikia iymaan ni maarifa. Na chanzo cha iymaan na maarifa ni ufunuo. Hivyo, alianza kwa kuonyesha jinsi ufunuo ulivyotokea na namna ulivyokuwa. Kisha akafuatia kutaja iymaan na maarifa. Utaratibu huu si ajali; na kwayo ametutengenezea baadhi ya nukta muhimu.

 

Hii ni jumla ya kile ambacho tunataka kukutaarifuni na kwayo ndio tunapaza sauti zetu juu. kipaumbele cha kwanza ni suala la ‘Aqiydah. Iymaan na maarifa ni njia ya kuifikia. Na chanzo cha maarifa na iymaan ni Kitabu na Sunnah.

 

Share