Ikiwa Majini Ni Viumbe Dhaifu Vipi Wamuingie Binaadamu Bila Ya Kuweza Kupona?

 

Ikiwa Majini Ni Viumbe Dhaifu Vipi Wamuingie

Binaadamu Bila Ya Kuweza Kupona?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatul-allah wabarakatu.

 

Nimesikia kuwa majini ni viumbe dhaifu kuliko binaadamu na tunawaogopa bure tu, sasa suala langu linakuja pale tunapoona baadhi ya watu wanaugua maradhi ya mashetani (kupanda jini kichwani) baadhi ya walimu na masheikh wetu wanasema hakuna maradhi ya aina hii na mimi huko nyuma nimepata ku sikia kwamba, maradhi hayo yapo na yanatibika. Na kwa kusema hayo ni kutokana na mwalimu wangu kunipa hadithi ya kisa cha Nabii Sulaiman Bin daoud alokuwa Rasuli na Mfalme kwa viumbe vyote kwa wakati huo kwamba alipata kuwauliza majini kuhusu wanavyomuingia binaadam na kumpoteza au kumpatia maradhi na dawa gani itumike wao hutoka na wakampatia majibu kwa kumpa baadhi ya aayah za Quran au sura kwamba zikisomwa hizi sisi hutoka na kumuacha huyo mtu. Jee lipi lina ukweli kati ya haya kuhusu maradhi hayo, yapo au hayapo, na kisa hiki ni sahihi au si sahihi?

 

Wabillah Tawfiq.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu kwa swali lako kuhusu majini na mashaytwaan. Suala la majini kuwa ni dhaifu halina utata katika shariy'ah, kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا﴿٦﴾

Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu. [Al-Jinn: 6].

 

Hiii hofu waliyokuwa nayo wanaadamu ndio iliyowafanya wao kuwaogopa majini na hivyo kuingia katika madhambi ya wazi.

 

Ama kuhusu mtu kuugua maradhi kwa kuingiwa na shaytwaan ni wazi kwani hata Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanyiwa sihri na Myahudi, Labiyd mpaka Allaah Aliyetukuka Akawatuma Malaika kuja kumpatia ponyo na hivyo amri ya kusoma Mu’awwadhatayn (Suwrah ya 113 na 114) ili kumkinga yeye na huo uchawi. [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na hilo pia lipo wazi kabisa kama Anavyosema Allaah Aliyetukuka:

فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ 

Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; [Al-Baqarah: 102].

 

Kwa ajili ya kuwepo tatizo hili la mtu kukumbwa na jini au shaytwaan ndio Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatufunza njia za kujikinga na shari lao. Kwa kuwa maradhi hayo yapo bila shaka yana tiba kutoka katika Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama yalivyopatikana katika vitabu vya Hadiyth.

 

Ama kuhusu kisa ulichotolewa na mwalimu wako kuwa tatizo hilo halipo, kisa hicho kina mashaka. Kisha kuna mgongano baina ya maelezo uliyoandika. Hebu tutazame yafuatayo:

 

  1. Hicho kisa ni dalili kinyume na alivyotaka huyo mwalimu, kwani Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-salaam) aliwauliza majini jinsi wanavyomuingia mtu au kumpatia maradhi.
  2. Kisha wakaulizwa majini kuhusu dawa nao wakatoa. Je, dawa hutolewa kwa asiye mgonjwa?
  3. Kuwa dawa aliyopatiwa Nabiy ni kisomo cha Qur-aan si sawa hata kimantiki kwani wakati huo Qur-aan ilikuwa haijateremshwa. Tufahamu kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja takriban miaka 1500 baada ya kuaga dunia Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis- salaam).

Hivyo, kisa cha mwalimu wako kinaunga mkono kuwa magonjwa hayo yapo. Na pia kurekebisha ibara uliyosema: “Nabiy Sulayman Bin Daoud alokuwa Rasuli na Mfalme kwa viumbe vyote kwa wakati huo”, sio sawa kwani tunafahamu kuwa Manabii wote walitumwa kwa watu wao isipokuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alitumwa kwa walimwengu wote. [Al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa mukhtasari tunasema kuwa ugonjwa huo upo na una tiba yake kulingana na Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share