Kadanganya Kabila Lake Apate Kukubaliwa Posa

SWALI:

 

Salaam Aleykhum,

Kama mtu kadanganya kuhusu kabila lake na kaposa kwa kutumia kabila lingine ili aweze kumpata msichana, na hali kuwa alijua wazi kwamba kama akisema kabila lake la ukweli asingepewa msichana, sasa siku ya ndoa akiwa ameenda kuonana na wazazi wa mwanamke je wakikataa kufungisha ndoa je itakuwa dhambi, kwani yeye kijana ni mwislaam mzuri ila anajua fika asingepewa msichana, hivyo katumia watu ambao wamesema uwongo kuwa huyo kijana ni mdogo wao, wao hawajali utajiri kwani hata wao waliopeleka posa ni maskini kihali, lakini wazazi wa msichana wanajali sana kabila yaani nasaba yao. Kwa upande wa dini italeta madhara kama tukikataa kumuozesha msichana?

wasalaam

Bella

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu posa na ndoa. Hakika ni kuwa jamii yetu ya Waislamu dunia nzima ina matatizo makubwa kuhusiana na mas-ala ya ndoa na kijamii kwa ujumla kwa sababu ya kuacha mafunzo mema ya Dini yetu. Ukabila umevamia sana hadi ya kwamba ile misingi ya kumuoza mvulana tuliyopatiwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haitiliwi maanani na wazazi pamoja na watoto wao. 

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo wa kwamba tutazame vijana wenye Dini na maadili, lakini muongozo huo umetupwa pembeni. Kwa sababu ya tatizo hilo, ndio vijana kama huyo ameona kuwa adanganye kuhusu kabila lake ili mradi apate kuozwa msichana kama ulivyoandika. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya:

Si katika sisi anayeita katika utaifa (ukabila)…” (Abu Daawuud).

Na tena:

Uacheni huo kwani ni uvundo” (Tafsiyr Ibn Kathiyr, Suratul Munafiquun).

 

Allaah Aliyetukuka Ametuwekea msingi mkubwa sana:

Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye Mcha Mungu zaidi katika nyinyi” (49: 13).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

Hakuna ubora wa Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu; wala ya mweupe juu ya mweusi ila kwa Taqwa (Ucha Mungu)”.

 

Bila shaka yoyote kuwa waliokwenda kumposea huyo kijana wamekosa na hiyo si tabia wala maadili ya Kislamu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati mmoja aliulizwa:

Je, Muislamu aweza kuwa muongo”. Akajibu: “Hapana” (Ahmad).

 

Mbali na kuwa katika Hadyith hiyo hiyo aliulizwa je, Muislamu aweza kuwa muoga na mzinzi, naye kasema ndio. Hivyo inatuonyesha ubaya mkubwa sana katika kusema uongo.

 

Huku kudanganya kunaweza kuwa sababu ya wazazi kukataa ndoa hiyo isifungwe. Kwa hilo wanaweza kupatiwa nguvu na sababu yenyewe ni ya kimantiki, wakajiuliza: Ikiwa huyu kijana au walioleta posa walisema uongo ni kitu gani ambacho hawezi au hawawezi kufanya?

 

Ilikuwa Kiislamu, waseme ukweli, mbali na kuwa kabila si muhimu, na ikiwa wazazi walikataa basi Uislamu umempatia njia kijana na msichana ikiwa pia maeridhika kufuatilia hadi kufika lengo. Amefanya haraka, na mara nyingi haraka na utovu wa tabia huleta hasara. Jambo la busara kwa wao, ni kwenda na kurekebisha hilo kabla udongo haujazidi maji.

 

Ama kwa upande wa Dini haitaleta madhara ikiwa wazazi watakataa lakini ingekuwa busara kwa sababu mmejua hilo mkae na kijana mumpatie nasaha kwa muono wa Kiislamu ili jambo lisitokee tena.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share