Kuwa Na Mahusiano Ya Muda Na Mwanamke Kwa Ajili Ya Kumuoa Kwa Vile Anasoma Bado - Sheria Inasemaje?

SWALI:

 

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Je uchumba unatakiwa kudumu kwa muda gani. Yaani kima cha juu cha muda ambacho watu wanaweza wakahusiana kama wachumba ni muda gani? Kwa sababu kuna baadhi wanaweza wakawa wanasoma au msichana anasoma kidato cha pili au tatu kisha anajitokeza mtu anasema atamuoa akimaliza shule baada ya mwaka au miaka miwili. Sheria inasemaje?


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uchumba na muda wake.

 

 

Ama kuhusu hilo la uchumba halina muda maalumu, yote ikitegemea jinsi mtakavyokubaliana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi aalihi wa sallam) alimposa mama wa Waumini ‘Aa’ishah (radhiya Allaahu ‘anha) akiwa Makkah lakini walianza kukaa pamoja kama wanandoa walipohamia Madiynah. Muda uliopita katika uchumba ni takriban miaka mitatu.

 

Hata hivyo, ni lazima wachumba wadhibiti kanuni za sheria. Hiyo ni kumaanisha kuwa sio umechumbia basi wakati wowote unaweza kuzungumza naye, ukatoka naye kwenda unapotaka kwenda, au kukaa naye faragha. Ikiwa hapana budi unataka kumuona ni lazima uende kwao na awepo mmoja wa Maharimu zake katika mazungumzo yako na yeye, ima awepo baba yake, mama yake, au ndugu zake waliobaleghe sio watoto wasiofahamu kinachoendelea.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share