Du’aa Gani Asome Ili Apasi Mtihani Darasani?

SWALI:

 

Naomba muniandikie dua ambayo itanisaidia mie wakati ninapoingia chumba cha kufanyia mtihani iwe rahisi kwangu kufanya mtihani wangu darasani bila ya kubabaika na kujibu maswali yote bila ya matatizo. Jazakakumul llah khaira

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du’aa ya kusomwa mtu anapoingia chumba cha mtihani.

 

Ni muhimu katika kila jambo kumtanguliza Allaah mbele, lakini pia tuna muongozo mzuri kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa tuwe wenyewe kwanza tunafanya juhudi na maandalizi kisha ndio tunamtegemea Allaah, na si kutawakkal bila ya kujishughulisha wala kuhangaika. Ni kama mfano wa yule mtu aliyemwacha ngamia yake nje bila kumfunga na kusema katwakkal kwa Allaah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamfahamisha kuwa amfunge ngamia wake na kisha atawakkal.

 

Hivyo, unapaswa kwanza usome vizuri na kujiandaa maandalizi kabambe kwa mitihani yako na huku ukimuomba Allaah Akusahilishie. Na ukiwa umejiandaa vyema na mitiuhani yako, basi utajikuta kwenye chumba cha mitihani ukiwa katika hali ya kujiamini na bila wasiwasi kabisa.

 

Hakika ni kuwa wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukuwa na mitihani ambayo ipo kwa wakati huu wetu. Watu walikuwa wanapata elimu kwa wahyi uliokuwa ukiteremka na mafunzo aliyokuwa akiyatoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa wale waliokuwa na matatizo ya kuhifadhi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe alikuwa akiwaombea kwa Allaah Aliyetukuka ili wapate ufahamu.

 

Nasi tunaweza kupata du’aa za jumla ambazo kwayo unaweza kumuomba Allaah Aliyetukuka Akufanyie wepesi.

 

 

Katika Qur-aan:

 

رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي  وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي  وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي يَفْقَهُوا قَوْلِي

Rabbishrah Liy Swadriy Wayassir Liy Amriy Wahlul 'Uqdatam-Mil-Lisaaniy Yafqahuu Qawliy.

Ee Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu, Na unifanyie nyepesi kazi yangu. Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu (Taha 25 – 28) 

 رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا   

 

Rabbi Zidniy 'Ilmaa

Mola wangu nizidishie elimu [Twaaha 114]

Katika Sunnah ni du’aa ambayo mtu anapokabiliwa na jambo gumu:

 

اللّهُـمَّ لا سَـهْلَ إِلاّ ما جَعَلـتَهُ سَهـلاً، وَأَنْتَ تَجْـعَلُ الْحَـزَنَ إِذا شِـئْتَ سَهـْلاً

Allaahumma laa sahla illa maa Ja’latahu sahlan, wa Anta Taj’alul-hazna idhaa shi-ita sahla.

 

“Ee Allah hakuna jepesi ila Ulilolifanya jepesi, Nawe Unalifanya gumu jepesi ukitaka”

 

 

“Ee Mwenyeezi Mungu hakuna jepesi ila Ulilolifanya jepesi, nawe unalifanya gumu kuwa jepesi Ukitaka.”

 

Pia itakuwa ni jambo muhimu kwako kuamka usiku kuswali Swalah ya Tahajjud na kumuomba ndani yake kuhusu hilo na kutumia fursa katika nyakati ambazo du’aa zinakubaliwa kama unapofunga Swawm na hasa wakati wa kufungua, baina ya Adhaan na Swalah ukamuelekea Allaah kwa du’aa. Pia unaweza kuwaambia wazazi na marafiki zako wakuombee kuhusu hilo. Na mahali pazuri pa kuomba ni pale wakati unaposujudu ndani ya Swalah yako na pale kabla ya kutoa Salaam kama alivyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Tunakuombea nasi kwa Allaah Aliyetukuka Akusahilishie mitihani yako na Akufanye ni mwenye kupita, Amiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share