Inafaa Kusujudu Unapomkumbuka Allaah?

Inafaa Kusujudu Unapomkumbuka Allaah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalamu alaikum

Napenda kuuliza hivi je inafaa kama mtu yu watembea kisha ukamkumbuka Allaah   kisha ukasujudu palepale kwa ajili yake. wabilah taufiq

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisujudu alipowasomea makafiri Quraysh Suwratun-Najm na alipofika mwisho wa Suwrah alisujudu pamoja na Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na Maquraysh wote wakasujudu juu ya mchanga mpaka wengine kwa kukosa nafasi wakasujudu juu ya migongo ya wenziwao. Na hivyo ndivyo ipasavyo unaposoma Aayah zenye Sajdah kutokana na Hadiyth:

 

Kutoka kwa  Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu ‘Anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema: ((Anaposoma mwana Adam (Ayah) ya kusujudu kisha akasujudu, shaytwaan atajitenga na kulia, atasema: “Ole wake (akijiambia yeye), ameamrishwa (mwana Aadam) kusujudu akasujudu na ana Pepoo, nami niliamrishwa kusujudu nikaasi na nina moto)) [Muslim, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Na hali nyengine ya kusujudu ni ile hali ya kuwa mtu yu juu ya kipando kinachokwenda kama walipokuwa Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Katika hali hiyo unatoa ishara ya kusujudu kwa kuinamisha kichwa na huko kutakuwa sawa kabisa.

 

Kadhalika pindi upatapo habari ya furaha au habari njema unaweza kusujudu kama shukurani kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  kama alivyofanya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma). Na kusujudu huko  waweza kusujudu popote bora pawe hapana najisi juu yake ikiwa unasujudu barabarani au kiwanjani au ofisini.

 

Ama kusujudu unapomkumbuka tu Allaah Subhaanah wa Ta’aala hatukupata dalili yake, hivyo ni vyema kutokusujudu. Bali kumkumbuka Allaah ('Azza wa Jalla)  ni aina ya ‘ibaada ya kutafakari, na ina thawabu nyingi, hivyo inatosha kujipatia thawabu kila unapomdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) .

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share