Ulimi Ndio Chanzo
‘Abdun-Naaswir Hikmany
Kawaida ya daktari ni kutibu wagonjwa wakati fundi wa computer ni kutengeneza computer. Iwapo mmoja wao atavamia nyanja ya mwenziwe hatoweza kuona ndani na ghafla anaweza kuharibu kila kitu.
Chukulia mfano wa fundi aliyeingia ndani ya chumba cha operation, au daktari aliyefungua computer; wote hawatojua kinachoendelea. Hivyo kila mmoja ana nyanja yake maalum na yampasa aitumie kwa maadili mazuri na kuiheshimu.
Ndivyo ilivyo kwa mwanaadamu juu ya viungo vyake vya mwili. Kila kiungo kina kazi yake maalum na yamlazimu kuvitumia kwa uadilifu. Aangalie Muislam namna ulimi unavyofanya kazi. Ni kiungo kisichohitaji kupatiwa petroli au dizeli ili kipate kufanya kazi wala si kiungo kinachotaka malipo ya alfu za dola kila mwezi. Kiungo ambacho maskini amepatiwa na tajiri hali kadhalika.
Basi na atupe jicho
Ulimi ndio utangulizi na muhtasari wa kila ovu. Zinaa inaanzia hapo na biashara za haramu zatangulizwa hapo. Unapokosa kudhibitiwa ulimi, ndio hutokezea mifarakano baina ya watu; rangi nyeupe ikafanywa nyeusi, dari likageuzwa sakafu na Muumini akavurumishiwa ukafiri. Hiyo yote ni kazi ya ulimi tu! Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
"… na ndimi zao zinasema uongo…" [16: 62].
Tuyakumbuke maneno ya Imaam An-Nawawy aliposema:
"Mjuwe kuwa mtu hapaswi kuzungumza isipokuwa lile lenye manufaa..." Badala ya kujilazimisha kuzungumza yenye faida, Waislam wa leo tumekuwa ni wepesi wa kusema uongo. Na hakuna msaada anaopatiwa Muislam kusema uongo
'Nipo karibu nakuja…' 'subiri dakika tano tu…' 'nipo hapa mtaa wa….' Ukitanabahi ni muda wa saa umepita nduguyo bado hajafika. Huo muda unaoahidiwa mara nyengine wavuka masafa ya kutoka Marekani kwenda Afrika Kusini, tena bila ya hata kuambiwa 'cancelled'. Maana utamsubiri hadi itaingia jioni, uende zako na kesho yake asitokee. Afadhali ya ndege utaandikiwa 'cancelled'.
Waislam tunalichukulia jambo hili ni la masikhara mno na dhihaka ya hali ya juu. Kila sekunde na kila neno linawekwa ndani ya kitabu ambacho tutapatiwa Siku ya Hisabu. Je umewahi kufikiria
“Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao, kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.” [24: 24].
Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Uchafu wa ndimi zao wasababisha watupwe Motoni kifudifudi…"
Ni lazima kwa Waislam, iwapo wanataka usalama mbele ya Muumba, waudhibiti ulimi. Kwani huo ndio msingi wa tabia njema.
Ulimi ndio chanzo, wengi Waislam wamefarikiana.
Ndimi zimejaa uozo, hadi ndugu kukhasimiana.
Simu zinaleta mzozo, uongo humo umejazana.
Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.
Badili yako mawazo, kumkumbuka wako Rabana.
Mukhofu Mwenye uwezo, Akinena kun fayakuuna.
Wewe sie mwanzo, utakufa shaka hapana.
Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.
Ulimi waleta maangamizo, duniani zahma zimejazana.
Yakamate yale mafunzo, aliyotuachia Mtume al-amiyna.
Hakufanya uongo gumzo, uzushi hakupatapo kunena.
Uchunge ulimi wako, Allaah Akupatie hifadhi.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha

Kali kweli nakiri,ULIMI
Kali kweli nakiri,ULIMI ninakubali,
Unayo nyingi hatari,Na madhila ya katili,
Kaumu tuna viburi,Tuna zitupa Amali,
ULIMI tukiuchunga,Kheri ALLAH atatupa.
Mbali nao ulimi,Jeuri hasa chanzo,
Ulimi mimi sisemi,Ingawa kunena funzo,
Quran haina uvumi,Ya nena pasi salizo,
Waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Tuki kikumbuka kifo,Nyoyo zitapata Hofu,
hata kilala fofo,Utayakwepa machafu,
Nalililo jifo,kwako utaomba wongofu,
Waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Fikiri sana umma,Wapi tuliko tokea,
UDONGO safi yasema,Quran inatongoa,
Maji dhalili nakama,Pia imeelezea,
waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Mawaidha yamenena,Kwa Haya na Hadithi,
Mifano pia twaona,Yalo wakuta Walithi,
twajifanza kutoona,Tunatenda Uhabithi,
Waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Tumkumbuke RABUKA,Kwa makanyo Allahuma,
Hatakama ni kucheka,Makatazo yanasema,
Nyoyo twafunga mateka,Nafsi tunazichoma,
Waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Kifo tukikikumbuka,Akili tutawanayo,
Tutahofu kupotoka,Kutenda yaliyo payo,
Na uongo kuropoka,Hofu tutakuwa nayo,
waja twasahau KUFA,Hili hasa ndilo chanzo.
Hizi ni zangu fikira,Kifo kama tukishufu,
Hata aliye fukara,Tajiri takuwajifu,
KABURI inabakora,Tutende yenye wongofu,
WAJA TUKUMBUKE KUFA,TUJAZE HOFU KWA ALLAH.
Salamu ndugu
Salamu ndugu Ramadhani,
nazifikisha kwa mapana.
Namuomba wetu Maanani,
Atuengeze ufahamu kwa kina,
Nakubali uliyoyaweka ukumbini,
Ukweli hakika umenena.
Haitokuwa maana kusoma,
Bila ya kuyatenda.
Tutakosa zake Rehma,
Mola Tukiacha kumpenda.
Ufunguo ulio salama,
Qur-aan Sunnah kuisoma.