Wanawake Kufanya kazi Katika Nyumba Za Wazee Wanaume Na Kuwahudumia

SWALI:

 

Asalama alaykuom khehe mimi nina swali moja, eti mti akiwa anafanya kazi katika nyumba ya wazee  ni lazima utawakosha na kuwavalisha nguo sasa mimi ni mwislamu wa kike jee inafaa kumshuhulikia mzee wa kiume kwa kumkosha na kumvalisha kama ilivyo kazi yangu, sina zaidi naona kujibiwa swali langu.


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Inatakiwa mwanzo tufahamu kuwa Uislamu una kanuni zake ambazo zinafaa zifatwe kila wakati isipokuwa katika hali fulani tu. Tujue kuwa jukumu la kuwatazama wazazi wanapokuwa wazee ni la watoto wake ambao wanafaa wawafanyie wema kama wao walivyolelewa wakiwa wadogo. Haya mas-alah ya kuwapeleka vizee katika nyumba za wazee si katika maadili mema ya Kiislamu bali ni utovu wa tabia na wema.

 

Suala la mwanamke kufanya kazi, ni suala ambalo linahitaji udharura mkubwa na vidhibiti vya kishariy'ah. Mwanamke kazi zake zinapaswa zaidi kuwa nyumbani kwake. Allaah Mtukufu Anasema:

 

((Na kaeni majumbani kwenu)) [Al-Ahzaab: 33].

 

Kadhaalika, ikiwa mwanamkie atafanya kazi nje ya nyumbani kwake, basi iwe kazi isiyo ya mchanganyiko wa wanawake na wanaume.

 

Vilevile jambo hili hata kama ingekuwa mwanamke ana dharura kubwa ya kufanya kazi na akatekeleza vidhibiti vilivyowekwa katika shariy'ah, bado isingefaa kwake kazi hiyo, kwani shariy'ah imekataza watu kutazama nyuchi za wengine, wakiwa jinsia moja au tofauti. Hivyo, hata ukisema hutomtazama lakini utamshika, na bado hutoruhusiwa kwani utakuwa ni mwenye kushika sehemu ambazo zinaweza kukupatia hisia nyengine hivyo kukufanya kutumbukia katika kidimbwi cha maasiya. Wala si sababu kusema kuwa huyu kizee hana matamanio nami sitomtaka au kumtamani.

 

Uislamu umeweka kinga nyingi mbalimbali ili mtu asiingie katika madhambi. Hilo halifai, na pia katika kazi hiyo haswa katika nchi za kimagharibi kuna kuwatayarishia hao vizee vyakula, na wengi hula nguruwe na hata kunywa pombe, na hayo yote anapaswa mwenye kuwatazama kuwaandalia. Kwa hiyo, kazi hiyo haifai.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share