Kunyofoa Au Kunyoa Au Kuchonga Nyusi Ni Kulaaniwa na Allaah

 

Kunyofoa Au Kunyoa Au Kuchonga Nyusi Ni Kulaaniwa na Allaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali La Kwanza:

 

Sheikh, Asaalam-aleiakum

 

Swala langu mimi nimeolewa mimi toka zamani sipendi kutowa nyusi najuwa kuwa ni dhambi lakini nilipoolewa natowa lakini sio ile kuonesha sana lakini hata hivyo sipendi lakini mume wangu anapenda nitowe na mimi mpaka nangombana na yeye  kuwa sitaki kutowa hivyo natowa kwa sababu yake. Jee ikiwa natowa kwa sababu yake sio kwa watu jee nimusikilize yeye niendelee kutowa? Naomba unijibu. Shukuran

 

Swali La Pili:

 

Je, kunyoa nyusi ni kupata laana ya Allah?.

 

Swali La Tatu:

Kunyoa nyusi kwa mwanamke inajuzu? Niliwahi kumuuliza Shekhe mmoja akaniambia kuwa inafaa kuzitengeneza.

 

Mimi nikamuuliza mbona kuna Hadiyth inasema kuwa " Amelaaniwa yule wenye kunyoa nyusi na mwenye kunyolewa ..............."  Shekhe huyo akanifahamisha yakuwa hadithi hii wengi hawaifahamu maana yake, akaendelea kusema " Zamani Wanawake wa kureshi walikuwa wakinyoa nyusi zote na kutia wanja kwa mtindo waupendao lakini sio kuzitengeneza. Kufanya hivo ni katika kujiweka safi kwa mwanamke na hasa kama atafanya kwa ajili ya mumewe na pia akifanya hivo mwanamke anatakiwa aufunike uso wake au ashushe shungi lake kuzifunika zile nyusi zake wasizione wale wasiomstahikia.

 

Mimi nikawa ninafanya hivo na wezangu waliponiuliza nami nikawafahamisha kama vile nilivyouliza lakini la kushangaza Nilipokutana nae tena huyo Shekhe katika mazungumzo tu akawa anasema kuwa "Haifai kunyoa nyusi na akawa anasisitiza kauli ileile ya kuwa "Wamelaaniwa wenyekufanya hivo" mimi nikamwambia mbona wewe uliniambia yakuwa inafaa jinsi kadhaaaaa . akasema mimi sikusema hivo wala sikimbuki lakini hadithi iko wazi kabsaaaaaaaaa.

 

Kwanza naomba nifafanuliwe zaidi juu ya Hadithi hiyo kama inafaa au laa.  Pili nifanye nini kwani na mimi niliwafahamisha wenzangu kuwa inafaa.

 

Swali La Nne:

 

Mwanamke kutengeneza nyusi kwa ajili ya harusi ni dhambi??

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Maswali matatu hayo tutajaribu kuyajibu hapa yote kwa umoja.

 

Kunyoa nyusi au kuzichonga ni haramu, sawa ikiwa ni kwa kujipodoa kwa ajili ya mume, au kwa kujipamba mwanamke binafsi.

 

Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasema:

 وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ

Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7]

 

Na katika jumla ya mambo aliyotukataza Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kunyoa nyusi.

 

عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال ((لعن الله الواشمات والمستوشمات والنامصات والمتنمصات والمتفلجات للحسن المغيرات خلق الله ((البخاري و مسلم))

Kutoka kwa 'Abdullahi bin Mas'uud (Radhwiya Allahu 'anhu) kwamba: ((Allaah Amewalaani watu wenye kuwachanja wenzao (tattoo) na wenye kuchanjwa, na wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wenye kunyolewa na wenye kuchonga meno yao (kama kufanya mwanya) kwa ajili ya kujipamba kubadilisha maumbile ya Allah)  [Al-Bukhaariy Hadiyth Namba 5948 na Muslim Namba 2125]

 

Ama nini cha kufanya, baada ya kuwa mlikuwa ni katika wafanyao hivyo? Jukumu lenu ni kurejea kwa Allah kwa kufanya toba ya kweli, sambamba na kuwalingania dada zenu wengine waachane na mwenendo huo, kwa lugha nzuri na mawaidha mema.

 

Jambo hili la kumuasi Allah na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakika halikutiliwa mkazo na dada zetu kabisa. Na mara nyingi linapokemewa kwa dada zetu wao hawalioni kama ni jambo la maana kukatazwa, wengine hulazimishwa japokuwa wao hawataki na waume zao kama ilivyo hali ya muulizaji wa kwanza. Ama wengine  husema "Lakini si najipamba kwa ajili ya mume wangu" au "Mume wangu anapenda nitoe nyusi" au "Itakuwaje nyusi zinijae nisizitoe?" na mengi husemwa ambayo yanadhihirisha kutotilia mkazo jambo hili ovu la kuasi amri.  Amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((لا طاعة لمخلوق في معصية الخالق))  رواه أحمد وهو صحيح

"Hakuna kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba". [Ahmad ikiwa sahiyh]

 

Vile vile: 

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((على المرء المسلم السمع والطاعة فيما أحب وكره إلا أن يؤمر بمعصية، فإن أمر بمعصية فلا سمع ولا طاعة))   رواه مسلم

Kasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) ((Muislamu inampasa asikie na atii katika anayoyapenda na anayoyachukia isipokuwa anapoamrishwa katika maasiya. Anapoamrishwa kufanya maasiya basi asisikie wa kutii)) [Muslim]

 

وقال:(( لا طاعة في معصية الله إنما الطاعة في المعروف))  رواه مسلم

Na kasema (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam): ((Hakuna kutii katika kumuasi Allaah, ama kutii ni katika mema)) [Muslim]

 

Tuchukue mfano mwema aliotuonyesha pia Abu Bakr wakati wa ukhalifa wake:

 

وقال أبو بكر رضي الله عنه حين بويع بالخلافة:"أطيعوني ما أطعت الله فيكم، فإن عصيته فلا طاعة لي عليكم"   

"Nitiini nitakapomtii Allah kwenu, na nitakapomuasi basi msinitii"

 

Muislamu inampasa atambue kuwa kumtii kiumbe katika maasiya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) haitomsaidia kitu akhera kwani huko yatakuja ni majuto tu na adhabu na pia hata kiumbe unachomtii inampasa na yeye amche Allah na akhofu adhabu siku ya Qiyaamah kwani ajue kuwa kumuamrisha mwenziwe katika maasi au kutomkataza basi yeye atamuombea apewe adhabu mara mbili na juu ya hivyo atamuombea laana kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

 

يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾ وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾

Siku zitakapopinduliwa nyuso zao motoni, watasema: Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Rasuli. Na watasema: Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia. Rabb wetu! Wape adhabu maradufu, na walaani laana kubwa. [Al-Ahzaab: 66-68]

 

Hivyo hakuna mmoja atakayemfaa mwenzake katika kuamrishana au kuridhishana katika maasi.

 

Pia ndugu zetu wa kike wajihadhari sana na baadhi ya wanaojiita Mashekhe wanapoulizwa kama ilivyo katika hali ya muulizaji wa tatu, akamjibu kwanza inafaa, kisha mara ya pili akakanusha. Bila shaka huyo hakuwa na elimu ya kutosha kuweza kutambua katazo lililokuja katika Hadiythi hiyo ya kulaaniwa mwanamke mwenye kunyoa nyusi.

 

Anapotaka Muislamu kuuuliza Swali la dini hasa linalohusu mambo ya haram na halali na yenye hatari kama hii, ni bora kumtafuta Shaykh mwenye elimu hasa ya dini ili asije kupata Fatwa itakayompotoza badala ya kumuongoza, na kisha bila ya kujua naye Muislamu akawapa wenzake Fatwa hiyo kama alivyofanya bila ya kujua muulizaji wa Swala la tatu.

 

Inampasa muulizaji wa Swali la tatu naye arudie kuwakanya aliowapa Fatwa hiyo isiyo sahihi na awafahamishe vilivyo, naye arudi kwa Mola wake na kuomba Maghfirah.

 

Tuwe na tahadhari na baadhi ya mashekhe kwani kuna wanaohalalisha hilo kwa sababu itikadi yao potofu inaruhusu mwanamke kunyofoa nyusi kwa ajili ya mumewe! Wajiulize hao wanaoambiwa hivyo na hao wenye itikadi hizo, ikiwa atanyofoa au kunyoa nyusi kwa mumewe, je, pindi akitoka nje atazuiaje wale wasio maharimu zake kuwaona bila nyusi zao na hali wenye itikadi hizo hawavai Niqaab? Hata ikiwa wataamua kuvaa Niqaab, maadam ni jambo limeshaharamishwa, hivyo haliwezi kuhalalika kwa vijisababu kama hivyo vya kumrembea mume au kuvaa Niqaab ukitoka n.k.

 

Kwa manufaa zaidi tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Kuzinyoa Nyusi Za Katikati Zilizozidi Sana Na Kuungana

 

Mwanamke Anayetoa Nyusi Ambaye Keshalaaniwa, Ibada Yake Inakubaliwa?

 

Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 2

 

Kutoa Nywele Za Uso Na Za Mwilini

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share