Kwa Nini Mawe Yataingizwa Motoni

SWALI:

Assalaam Alaykum

Kwanza natoa shukrani zangu za dhati kwa kazi kubwa mnayo ifanya kuelimisha Umma jazaa yenu munitaipata kwa Mwenyezi Mungu Amiin.

Swali, Mwenye-enzi Mungu anasema Jahannam kuni zake zitakua Watu na Mawe

- Mungu atuepushe huko Amiin, Kwanini Mawe yataingizwa Motoni - yamefanya kosa gani?

Ahsanteni

 

 


 

JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Anaposema Allaah سبحانه وتعالى kuwa mawe yatakuwa motoni haina maana kwamba mawe yameonewa kuingizwa motoni, kwani mawe sio katika vitu vyenye roho yaani sio viumbe. Bali ni vitu vinavyotumika kupatikana faida fulani kama nyenzo nyinginezo na faida zake mbali mbali.

Lakini Allaah سبحانه وتعالى  Ametaja katika Aayah ifuatayo kuwa kuni za moto zitakuwa ni watu na mawe kwa vile hao watu walikuwa wakichonga masanamu kutokana na mawe na kuyaabudu. Ndio maana Anasema kuwa Atawaingiza wao pamoja na hayo mawe yao ziwe kama ni kuni za kuchochoea moto wa Jahannam.

((إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ))

((Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Allaah ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu)) [Al-Anbiyaa: 98]

Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما amesema  ni : 'kuwaka (moto)' [Al-Qurtubi 11:343]

 

'Kuni za Jahannamu' ina maana kwamba kuni za moto.

Mujaahid, Ikrimah na Qataadah wamesema: "Ni mafuta".

Adh-Dhwahaak amesema: "Mafuta ya Jahannam ina maana ni kile kinachotumbukizwa ndani yake" [At-Twabariy 18:536 – Tafsiyr Ibnu Kathiyr 6:500] 

Na hii pia ni rai ya wengineo [At-Tabariy 18:536 katika Tafsiyr ya Ibnu Kathiyr 6:500]

Na ndio maana pia Allaah سبحانه وتعالى Anasema katika Aayah nyingine,

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ))

((Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allaah kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa)) [At-Tahriym  6]

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share