Vipi Nabii Musa Alizungumza Na Allaah?

SWALI:

ASALAM ALAYKUM

Swali?  Maneno ya Allaah hayana sauti wala helufi, sasa ni kwa vipi Nabii wa Allaah ambae ni MOUSA Juu yake amani alikuwa akizungumza na Allaah?

NB: Haya maswali ninayo kuulizeni ni kwamba hata mimi nimeulizwa maswali haya ndio na mimi ninakuulizeni.

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu suala hilo la Itikadi (‘Aqiydah). Msingi wetu mkubwa wa kuelewa na kufahamu mambo yetu yote katika nyanja zote za kimaisha ni Qur-aan na Sunnah za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo, tungependa kueleza mambo fulani kabla ya kuja katika swali lenyewe ambalo nimeulizwa na ndugu yetu.

Muislamu anaamini yale aliyonayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) miongoni mwa Majina Yake Mazuri na mema na Sifa Zake za juu wala Muislamu hamshirikishi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na mwingine asiyekuwa Yeye katika Majina na Sifa hizo. Muislamu hayafanyii taawili (tafsiri) Majina hayo na Sifa hizo, wala hafananishi Sifa za Allaah na sifa za viumbe  Vyake kwa kusema vipi Allaah ana uhai na vipi Allaah Anazungumza, Anaona na Kusikia, hayo kufanywa na Muislamu ni muhali na hayatakiwi.

Muislamu anathibitisha kwa Allaah yale Aliyojithibitishia Mwenyewe na akayathibitisha Mtume Wake miongoni mwa Majina na Sifa Zake. Muislamu anamkatalia Allaah Sifa Alizozikataa Mwenyewe na akazikataa Mtume Wake, za kuepukana na kila aibu na upungufu kwa ujumla na kwa mchanganuo. 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amejisifu Mwenyewe kwamba Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona, Mjuzi, Mwenye hekima, Mwenye Nguvu, Mpole, Mwenye kusamehe, Anzungumza, Ana mikono, Ana uso na kadhalika. Yeye Amezungumza na Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) na Amelingana sawa sawa juu ya Arshi Yake. Sifa ya kusikia na kuzungumza ni Yake kwani Amesema kuhusu hilo: “Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona” (42: 11) na “Mitume hawa tumewatukuza baadhi yao juu ya baadhi. Katika wao kuna ambaye Amesema naye Allaah, na baadhi yao Amewatukuza daraja nyingi” (2: 253).

Hayo wamekiri wanazuoni wema wa kale na wa sasa kuanzia kwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) juu ya Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) bila kuzipa tafsiri potofu, au kuzikanusha au kuzitoa katika dhahiri yake. Kwani haikuthibiti kuna Swahaba yeyote aliyeipa tafsiri potofu Sifa miongoni mwa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) au kuipindisha au kuipinga au akasema kuwa dhahiri yake sio iliyokusudiwa. Bali walikuwa wanaamini maana inayofahamika kutoka katika Sifa hiyo kama ilivyo, na wanaichukulia dhahiri yake, hali wanaelewa kuwa Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) sio sifa za viumbe Wake.

Imaam Maalik aliulizwa kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): “Ar-Rahmaan, Mwingi wa Rehema, Aliye juu ya Kiti cha Enzi” (20: 5). Akasema: “Kulingana (Kuwa Kwake juu ya kiti cha enzi) maana yake inaeleweka, na namna ya kulingana (kuwa Kwake juu ya ‘Arsh) huko hakueleweki na kuliulizia hilo ni uzushi”.

Imaam Ash-Shaafi‘iy alisema: “Nimemuamini Allaah na kilichokuja kutoka kwa Allaah kama Alivyokusudia Allaah na nimemuamini Mtume wa Allaah, na kila kilichokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah, kama alivyokusudia Mtume wa Allaah”.

Imaam Ahmad alikuwa akisema kutokana na kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo kuwa: “Hakika Allaah Anateremka kwenye mbingu ya dunia, na kwamba Allaah Anafurahi, Anacheka, Anaridhia, Anaona karaha na Anapenda, alikuwa akisema: ‘Tunayaamini, na tunayakubali, si kwa namna wala kwa maana fulani’. Anakusudia kuwa sisi tunaamini kuwa Allaah Anaona, naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake tofauti na viumbe Vyake. Lakini hatuelewi namna ya kushuka Kwake, wala kuona Kwake, wala kulingana Kwake, wala maana hasa ya hayo. Bali maana yake hiyo tunaiacha katika ilimu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa Aliyoyasema na Aliyomletea Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hatumpingi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala hatumpi sifa zaidi ya zile Alizojisifia Mwenyewe na Alizosifiwa na Mtume Wake bila ya mpaka wala kikomo, nasi tunaelewa kuwa hakuna kilicho mfano Wake Naye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona”.

Kuhusu ibara yako: “Maneno ya Allaah hayana sauti wala herufi” hayana uthibitisho wowote bali Qur-aan ipo wazi kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alizungumza na Muusa (‘Alayhis Salaam) kama tutakavyoona hapa chini. Neno hili ambalo limetumika la kuzungumza limetumika sehemu nyingi katika Qur-aan. Miongoni mwayo ni mnyama ambaye atazungumza na watu kabla ya Qiyaamah: “Na itakapowaangukia kauli juu yao, Tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana yakini na Ishara Zetu” (27: 82).

Na kuhusu Siku ya Qiyaamah, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuelezea kuwa kila kitu kitazungumza: “Leo Tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma” (36: 65).

Ama kuhusu Maryam, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuelezea kuwa Malaika alimwambia aseme yafuatayo pindi anapokuja kwa watu wake: “Basi ule na unywe na litue jicho lako. Na kama ukimuona mtu yeyote (akakuuliza habari ya mtoto huyo) mwambie: ‘Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Allaah Mwingi wa rehema ya kufunga, kwa hivyo leo sitasema na mtu” (19: 26).

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) naye Anatueleza kuwa Yeye Amezungumza na baadhi ya wateule Wake: “Mitume Tumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine. Miongoni mwao wako ambao Allaah Alisema nao” (2: 253).

Na tena: “Na Tuliwapelekea Wahyi Mitume Tuliokuhadithia habari zao zamani na Mitume ambao hatukukuhadithia. Na Allaah Akamsemeza Muusa” (4: 164).

Na Amesema, “Na alipofika Muusa katika miadi Yetu, na Mola wake Mlezi Akazungumza naye” (7: 143).

Qur-aan pia inatuelezea mazungumzo baina ya Allaah na Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam): “Basi alipofika (Muusa) akaitwa: ‘Ewe Muusa!’ ‘Bila shaka Mimi ndiye Mola wako. Basi vua viatu vyako hakika wewe uko katika bonde takatifu la Tuwaa. Nami Nimekuchagua (wewe kuwa Mtume) basi yasikilize unayoletewa Wahyi’. …Na ni nini kilichomo mkononi mwako wa kuume, ewe Muusa? Muusa akasema: ‘Hii ni fimbo yangu…’” (20: 11 – 37).

Haya ni mazungumzo marefu baina ya Allaah na Nabii Aliyemchagua, Nabii Muusa. Hapana shaka kwa yeyote yule kuwa mazungumzo yanakuwa ni sauti ambapo mmoja anasema na mwengine anasikia.

Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘Alayhi wa Sallam) alipokwenda katika safari yake ya Mi’iraaj katika sehemu ya usiku alikuwa pia ni mwenye kuzungumza na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na kupokea maagizo ya Swalah za faradhi ambazo tunazitekeleza sasa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anazungumza na wateule wake, Manabii kwa njia kadhaa kama Alivyotuelezea hilo katika Qur-aan Tukufu. Anasema Aliyetukuka: “Na haikuwa kwa mtu kwamba Allaah Anasema naye ila kwa ilhamu (anayotiwa moyoni) au kwa nyuma ya pazia au humtuma Mjumbe (Jibrili); naye humfunulia (humletea Wahyi) kiasi anachotaka kwa idhini Yake; bila shaka Yeye ndiye aliye Juu, Mwenye hikima” (42: 51).

Ibara kwa nyuma ya pazia ina maana kusikilizishwa sauti inatoka kwa Allaah pasina kumuona Allaah.

Kitu ambacho hatujui wala hatuwezi kuleta taawili (kugeuza maana yake) au kufananisha ni sauti hii inakuwa vipi kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Hakuna chochote mfano Wake” (42: 11).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share