Bima (Insurance) Inakubalika Katika Uislamu?

SWALI:

 

Assalam aleikum. Nilikuwa nauliza suala kuhusu insurance katika uislam je ni ipi hukumu yake na ni yapi mchango wa wanavyuoni wa kisalaf?


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu bima (Insurance). Hakika ni kuwa wanazuoni wa kisalaf waliopo kote duniani kuanzia wale waliopo Arabuni na hata wale wa Afrika Mashariki kama Kenya wametoa maelekezo kuwa bima ya kibiashara (commercial) ni haramu kwa Muislamu. Na katika hizo ni bima ya gari, nyumba, maisha na kadhalika. Uharamu wake ni kuwa ndani yake kuna Gharar (uongo), riba, Qimaar (kamari) na kuuza deni kwa deni. Moja tu kati ya hizi zikipatikana katika kitu chochote hukifanya kuwa haramu. Na katika bima nukta hizi nne zinapatikana.

 

Kwa dharura ambayo ipo katika mataifa yenye masharti kuwa lazima mtu ili aruhusiwe kuendesha gari au kuwa na nyumba awe na bima hapo sheria inamruhusu lakini atatakiwa achukue ya chini kabisa.

 

Mfano ni kuwa katika bima ya gari na vitu vinginevyo huwa ipo ile ambayo ni comprehensive, fire and theft na third party. Katika hali hiyo Muislamu anafaa achukue ile ya third party. Bima ambayo inaruhusiwa kisheria ni ile ya kushirikiana (Co-operative insurance).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share