Kazi Ya Kinyozi Inafaa Kwa Kuwakata Nywele Wanawake?

SWALI:

Kila sifa njema inamstahiki Allaah Subhaanahu wata'alaa Allaah ambaye ame tupa dini Nzuri ya Kislaam.Sala Na Salaam Zimshukie juu ya Mtume Muhammad Aleyhi Salaatu Wassalaam.

 Assalaamu Aleykum,

Swali langu ni kama ifuatayo.Mimi ni kijana ninaye fanya kazi ya Kinyoozi sasa katika kazi yangu ya kinyoozi kunakuwa na watu wa jinsia tofauti katika Nchi zetu za Africa Mashariki wanawake na wanaume Je nina Ruhusiwa Kuwa Nyoa Wanawake na wasichana wa schooli?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Tunashukuru kwa swali lako. Asli katika kazi yo yote yenye kutolewa huduma kwa watu wa jinsia tofauti ni kuwa hukumu ya Kiislamu ni kuwa hairuhusiwi kwako kuwapa huduma wanawake madamu wewe ni mwanamume kama unaamini Allaah na Siku ya Mwisho, kama kuna dharura ni hukumu tofauti vyenginevyo utakuwa unakwenda kinyume na mafundisho ya dini yako.

 

Je nina ruhusiwa kuwa nyoa wanawake na wasichana wa schooli? Katika Uislamu mwanamke hatakiwi nywele zake zionekanwe isipokuwa na mumewe au Mahaarimu wake, kwani nywele ni katika uzuri wake, na katika Uislamu mwanamke hatakiwi anyoe nywele zake isipokuwa kama kuna dharura ya kufanya hivyo, kwani hata katika ibaada kubwa ya Hijja wanawake huwaruhusiwi kunyoa nywele zao bali hutakiwa wapunguze nywele zao kiasi kidogo tu, wakati wanaume hutakiwa wapunguze au wazinyowe zote.

Hivyo huruhusiwi kuwanyoa nywele wanawake hata wasichana kwani wao pia ni wanawake.

Kwa kuwa suala linahusiana na saloon na kinyozi tungependa tufaidike zaidi katika yenye kuhusiana na saloon na kinyozi.

Kusuka nywele: Mwanamume kusuka nywele ni kujifananishana na mwanamke kwani wao ndio wanotarajiwa kusuka na ndio katika jamii yetu ilivyo, hivyo kinyozi kama utakuwa unasuka pia wanaume utakuwa unakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu kwani utakuwa unatoa msaada katika kuwafananisha wanaume na wanawake na hilo limelaaniwa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

 

“Amewalaani Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaume wenye kujifananisha na wanawake na wanawake wenye kujifananaisha na wanaume” Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Mavazi, mlango wenye kujifananisha na wanawake na wenye kujifananisha na wanaume.

Kunyoa ndevu haifai: Mwanamume Muislamu anatakiwa awe anafuga ndevu na kunyoa masharubu sio kinyume chake; hivyo basi kwa kuwa wewe ni kinyozi bila shaka yoyote wako wanaokuja kutaka uwanyoe ndevu na uwachonge masharubu na haya yamekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alicho amrisha ni kufuga na kuzikuza ndevu na sio kuzinyoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

“Wakhalifuni washirikina (muwe tofauti na wanavyofanya) wacheni ndevu zenu na punguzeni masharubu yenu – na katika riwaya nyingine -: kupunguza masharubu ni katika fitrah (maumbile ya asli – Uislam -) Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Mavazi, mlango wa kukata kucha.

Na Ahaadiyth za kuamrishwa kufuga ndevu ni nyingi mno.

Kweli unyozi ni kazi yako lakini pia usisahau kazi yako ya asili ambayo imeasisiwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuendelezwa na kila anayempenda, kazi ya kuwalingania wateja Waislamu kwa kuwaeleza hayo uliyoyapata na kuwakataza bali kuwawekea wazi kuwa wewe kinyozi lakini unapenda uwe na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya Qiyaamah hivyo hautakuwa tayari kutekeleza alichokikataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama kitakutilia kipato kikubwa, vyenginevyo elewa kuwa utakuwa unachangia katika kuipinga na kuikebehi bali kuibeza amri ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wenye kuibeza au kuipinga amri yake Qur-aan inawatahadharisha kwa kusema hivi:

“ …. Basi nawatahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu iumizayo.” An-Nuur: 63.

Kunyoa/ kupunguza nywele na kuziacha baadhi yake kama mitindo iliyopo sasa watu hunyoa kama kunguru kichwa chote hunyolewa na kuachwa nywele nyingi sehemu moja kama vile utosini na kadhalika haifai; hii ni katika mtindo inayopendezeshwa na washirikina kwa Waislamu hasa waliofitinishwa na mchezo mpira na muziki; huwa wanawaiga wachezaji na wanamuziki katika kila kitu likiwemo hili la mitindo ya kunyoa nywele zao, hiyvo ieleweke kuwa haifai kwani yamekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

“Kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza Al-Qaza’; akasema: nikamuuliza Naafi’ ni nini Al-Qaza’? Akasema: kunyoa baadhi ya kichwa cha mtoto na na kuacha baadhi yake (panki) Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango kuchukiwa kwa Al-Qaza' (kunyoa panki)’.

 

Na katika yenye kufungamana na saloon pia kunakuwa na watu wa jinsia tofauti ni kuwapamba na kuwatengeneza wanawake hasa nyakati za harusi na hili haramu pia, kwani katika kumtengeneza mteja huwa unalazimika kumgusa kichwa, kidevu, mashavu na kadhalika na ikiwa mteja ni mwanamke basi unakuwa unakwenda kinyume na amri ya dini na mwenye kukuletea mkewe au  mtoto wake wa kike kwa kazi hiyo huwa anakutakia shari katika Akhera yako na mume mwenye kumpeleka mkewe katika saloon ya wanaume ili atengenezwe au apambwe huwa miongoni mwa wenye kuitwa Dayyuuth (mtu asiye na wivu na machafu yanayofanywa kwa mkewe) na huyu haingii Peponi.

 

Kunyoa nyusi haifai: katika yenye kufungamana na saloon na kinyozi pia hili na halifai kufanywa na pia kuunganisha nywele ni katika yaliyokatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama mume anapendezewa haifai mwanamke kunyoa nyusi wala kuunganisha nywele zake kama ilivyothibiti katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

Amewalaani Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Mwenye kuchonga nyusi na mwenye kuwachonga wenzake nyusi, mwenye kuunganisha nywele na mwenye kuwaunganisha wenzake nywele, mwenye kupiga chapa (tattoo) katika mwili na mwenye kuwapiga wenzake chapa katika mwili, na wenye kuchonga meno kwa ajili ya uzuri  - na katika riwaya - kutoka kwa bibi Asmaa amesema alikuja mwanamke kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nina mtoto wangu bi harusi amefikwa na maradhi nywele zake zimenyonyoka, je niziunganishe? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Amemlaani Allaah mwenye kuunganisha nywele na mwenye kuwaunganisha wenzake nywele -” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha mavazi na mapambo, mlango wa uharamu wa kuunganisha nywele.

Hivyo tunakunasihi ndugu yetu kinyozi, uchunge mipaka ya Allaah na Mtume Wake katika kazi yako na uwe na msimamo thabiti katika dini yako na Allaah Akujaalie uweze kujiepusha na makatazo na haraam zote hizo ambazo zinahusiana na kazi yako hiyo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share