Nani Aliyesulubiwa Badala ya Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam)?

SWALI:

 

Assalaam alaykum,

 

Bismillahi Rahman Rahim.

 

Namshukuru ALLAH kwa yote na kumtakia rahma na salam Mtume (SAW). Naomba kuuliza kuhusu hii dhana ya kifo cha Nabii Issa (AS) Walionayo wenzetu.

 

Nimekuwa naulizwa swali hili mara nyingi na kwa kweli sina jawabu la kuridhisha. Je ni kweli Issa (AS) alikamatwa, kuteswa na kuuwawa? Na kama sio, nani aliye sulubiwa msalabani? Naomba msaada wenu ktk hili.

 

Wabillahi tawfiq. Assalaam alykum


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusulubiwa kwa 'Iysa ('Alayhis Salaam). Hakika ni kuwa Qur-aan iko wazi kabisa kuwa Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam) hakushikwa, hakusulubiwa wala hakuuawa. Allaah Aliyetukuka Anatuelezea:

 

"Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuua Masihi 'Iysa, mwana wa Maryam, Mtume wa Allaah - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini. Bali Allaah Alimnyanyua Kwake, na hakika Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima" (4: 157-158).

 

Aayah hizo mbili zilizo juu zinatubainishia wazi kuwa Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam) hakuuliwa bali walifananishiwa mtu mwingine kwa sura zake. Katika Injili ya Barnaba (Gospel of Barnabas) inatueleza kuwa huyu aliyefananishwa na Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam) ambaye alisulubiwa ni Juda Iskariot ambaye alikuwa ni mfuasi wake lakini akamsaliti kwa maaskari wa Kirumi. Hata hivyo, Allaah Aliyetukuka Hamuacha Mtume Wake ashikwe, Akamgeuza huyu Juda alipoingia katika pango alilokuwemo Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam). Huyu ndiye aliyesulubiwa.

 

Ama Biblia ambayo ipo mikononi mwetu sasa ina utata mkubwa sana kuhusu suala hilo lakini pia inaonyesha kuwa aliyesulubiwa si 'Iysa bali ni mtu mwengine kabisa. Sababu ambazo zinatufanya tuseme hivyo ni zifuatazo:

 

1.   Paulo anasema kuwa yeye anakufa kila siku (1 Wakorintho 15: 31). Hii ina maana anateseka kila siku. Tufahamu kuwa kabla ya kukamatwa kwa Yesu, Biblia inatuarifu kuwa aliswali na kumuomba Mungu amuondoshee kikombe hicho (yaani umauti) kulingana na matakwa yake (Mungu) {Mathayo 26: 39, Marko 14: 35-36) na Luka 22: 42-43}. Na katika Luka tunaelezwa kuwa Malaika alitumwa kumtia nguvu. Je, maombi ya 'Iysa (au Yesu katika Biblia) yalijibiwa? Tunafahamishwa kuwa Yesu alisikilizwa maombi yake kwa ajili ya kumcha Mungu (Waebrania 5: 7). Maombi ya mtu mwema yanasikilizwa (Yakobo 5: 16). Na ni maneno yake (Yesu) aliyosema kuwa omba, nawe utapewa (Mathayo 7: 7-10). Kama tulivyoona hapo juu kuwa Yesu aliomba, naye bila shaka alikubaliwa.

 

2.  Yesu alikuwa hai kama alivyotabiri. Yesu alimwambia Maria Magdalene: "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa baba …" (Yohane 20: 17). Yesu anaulizwa kuhusu ufufuo, naye anajibu kuwa miili iliyofufuliwa huwa kama Malaika (Luka 20: 34-36). Yesu anawatokea wanafunzi wake na kuwaambia wampapase mikono yake kuwa ndiye yeye naye akachukua kipande cha samaki na kula (Luka 24: 36-42).

 

3.   Na ikiwa kweli Yesu alikufa msalabani basi yeye ni Nabii wa uwongo na aliyelaaniwa. Yeyote anayetundikwa mtini amelaaniwa na Mungu (Kumbukumbu la Sheria 21: 22-23). Amelaaniwa anayetundikwa kwenye mti (Wagalatia 3: 13).

 

 

4.   Wakristo wanaamini kufa na kufufuliwa kwa ajili ya kufuata mafundisho ya Paulo (Matendo 17: 18). Ufufuo wa Yesu ni kulingana na Injili ya Paulo (II Timetheo 2: 8).

5.  Yesu alitabiri aliokolewa kuuliwa (Mathayo 23: 39, Yohane 7: 32-36, 8: 21-29 na 16: 32-33). Yesu hakika hakusulubiwa kabisa (Wagalatia 3: 1).

 

6.  Na hakika Yesu anatuhakikishia kuwa Mungu anamsikiliza yeye daima (Yohane 11: 41-42).

 

7.  Yohane anatueleza kuwa Yesu hakuvunjwa miguu yake bali alichomwa mkuki na hapo damu ikatoka (Yohane 19: 32-34). Kutokwa kwa damu inaonyesha kuwa alikuwa bado yu hai.

 

8.     Na dalili nyingine zipo lakini tutosheke na hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share